NA DIRAMAKINI
WACHEZAJI, viongozi pamoja na benchi la ufundi la timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC) leo wamezuru katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,hayati Dokta John Joseph Pombe Magufuli nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita.


KMC FC ambayo imeweka kambi wilayani Chato tangu Aprili 18, mwaka huu ikiwa ni mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar,uliopigwa Aprili 17,mwaka huu katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, inaendelea kutambua mchango mkubwa ambao hayati Dkt.Magufuli aliouonesha kwenye sekta hiyo enzi ya uhai wake.

“ KMC tunatambua mchango mkubwa ambao hayati Dkt.Magufuli aliufanya enzi ya uhai wake katika sekta hii ya michezo, hivyo ndio mana tukaona wakati huu ambao timu ipo huku Kanda ya Ziwa tufike nyumbani kwake kuzuru pamoja na kusalimia familia yake, lakini pia kufika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi ambapo kimsingi tumepata mapokezi makubwa na tunawashukuru kwa hilo.
"Lakini pia wakazi wa Chato wameonesha kufurahishwa na uwepo kwa KMC, kwani wakati wa mazoezi wamejitokeza kwa wingi kuwasapoti wachezaji na hii kwetu kama timu tumechukua kama sehemu ya kutambua mchango wao kwetu na hivyo kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa pindi tutakapokuja huku kwa mara nyingine,"amesema.