NA DIRAMAKINI
NAIBU Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewasilisha vipaumbele vitano vya wizara mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bw. Qu Dongyu.

Katika kikao na Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dongyu, Mheshimiwa Mavunde amewasilisha vipaumbele ambavyo vinalenga kuifikia Agenda 10/30 na kutaka kuendelea kuimarisha ushirikiano na FAO katika kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Mavunde ameangazia upande wa kukuza uwezo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kutimiza malengo yake ya utafiti na uvumbuzi wa mbegu bora na kanuni bora za kilimo ili kuwawezesha wakulima wa Tanzani kulima kwa tija.

Pia Mheshimiwa Mavunde ameangazia uwekezaji kwenye Kilimo cha Umwagiliaji ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua ambacho kimekuwa kikiathiriwa sana na mabadiliko ya tabia nchi.
Sambamba na kuimarisha huduma za ugani kwa kuwezesha mafunzo maalum ya zao moja moja ili kuongeza umahiri wa maafisa ugani katika kuwahudumia wakulima na kuwasaidia kulima kwa tija.
Kipaumbele kingine ni mpango wa ushirikishwaji wa vijana katika kilimo kupitia mfumo wa mashamba makubwa ya pamoja (block farms).