NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kumsimamisha kazi mkandarasi anayejenga miundombinu ya mnada wa Ndelema wilayani Handeni mkoani Tanga kwa kushindwa kufanya kazi kwa wakati.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akiongea na moja ya familia katika Kijiji cha Msomera wakati alipotembela kijijini hapo kukagua kazi ya maandalizi ya kuwapokea wafugaji kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro inayoendelea kufanyika. Mhe. Ndaki amewasihi kuwapokea wafugaji wanaokuja vizuri na kuishi nao.
Waziri Ndaki ametoa agizo hilo Aprili 23, 2022 baada ya kukagua kazi iliyofanyika katika ujenzi wa miundombinu ya mnada huo ambapo wakati anapita kukagua hakukuwa na kazi yoyote inayoendelea na mkandarasi hakuwepo kwenye eneo la ujenzi.
Pamoja na agizo hilo la kusitisha mkataba wa mkandarasi huyo, Waziri Ndaki pia ameagiza kusitishwa kwa malipo ambayo yalikuwa yapo kwenye mchakato kwa kuwa mkandarasi huyo hastahili kulipwa kutokana na kazi aliyoifanya. Aidha, amemuagiza Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo kumtafuta mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa wakati ndani ya siku 14 ili kazi hiyo iweze kuendelea.
Waziri Ndaki amesema serikali ilishatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya mnada huo inajengwa kwa lengo la kuwezeshwa wafugaji kuuza mifugo yao kwenye mazingira mazuri na kusaidia katika kuongeza ukusanyaji wa maduhuli. Hivyo amewasihi wakandarasi kuhakikisha wanafanyakazi zao kwa wakati kulingana na mikataba kwani serikali haitamvumilia mkandarasi mzembe.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchemba amesema kuwa mnada huo ni muhimu sana katika ukusanyaji wa maduhuli ya halmashauri hivyo ucheleweshwaji wa ujenzi wa miundombinu yake unakwamisha maendeleo ya mji wa handeni ambayo yangepatikana kupitia fedha ambazo zingekusanywa hapo.
Prof. Hezron Nonga ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, amesema kuwa mkandarasi huyo alishaandikiwa barua ya onyo kutokana na ucheleweshaji wake wa kazi lakini pia alishaitwa wizarani kwa lengo la kumtaka amalize kazi aliyopewa ya ujenzi wa miundombinu kwenye mnada wa Ndelema.
Katika ziara yake hiyo, Waziri Ndaki alitembelea Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga kukagua kazi zinazoendelea kufanyika kwa ajili ya maandalizi ya kuwapokea wafugaji kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro wakati alipotembelea Kijiji cha Msomera wilayani Handeni.
Waziri Ndaki amewasihi wafugaji hao kuhamia kwenye Kijiji hicho kwa kuwa mazingira yanayoandaliwa na serikali ni mazuri kwa shughuli zao za mifugo.