Mke wa Rais wa Zanzibar, Mariam Mwinyi azidi kutoa tabasamu kwa wananchi

NA DIRAMAKINI

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amewanasihi waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kuimarisha ibada pamoja na kutoa sadaka kwa wingi katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani hasa katika kumi la mwisho.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akitoa sadaka ya futari kwa wajane wazee na wenye hali ngumu huko katika kisiwa cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 wa kisiwa cha Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation alisema kuwa, mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan ndio mwezi uliosisitizwa kukithirisha ibada sambamba na kutoa sadaka.

Alieleza kwamba, katika kumi la mwisho la mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vyema waumini wakakithirisha ibada pamoja na visimamo vya usiku ili kuweza kuupata usiku wenye cheo (Laylatulqadr) ambao ni usiku wenye cheo.
Akizungumza na wananchi katika kundi la wajane wazee na wenye hali ngumu katika Shehia nne za Tumbatu huko Jongoe, Mama Mariam Mwinyi alisema kuwa Jumuiya yake imeamua kwa makusudi kuwapelekea sadaka wananchi hao wa Tumbatu kutokana na mahitaji waliyonayo.

Alisema kuwa Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation imekuwa ikitoa misaada kwa makundi mbalimbali katika jamii hapa Zanzibar wakiwemo akina mama, watoto, wazee, wasichana, wajane na wale wenye hali ngumu kwa ajili ya kufikia azma iliyowekwa na jumuiya hiyo.

Hivyo, Mama Mariam Mwinyi alitoa wito kwa wale wote wenye uwezo kuendelea kutoa sadaka zao kwa wale wasiokuwa na uwezo hasa katika kipindi hichi cha mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud alimpongeza Mama Mariam Mwinyi pamoja na Jumuiya yake kwa misaada yake hiyo ikiwemo vyakula kwa akina mama hao 110 pamoja na misahafu kwa ajili ya misikiti na madrasa za kisiwa hicho.

Mkuu wa Mkoa alisema kuwa hatua aliyoichukua Mama Mariam Mwinyi ya kutoa sadaka kwa wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa ni za kupongezwa na kuungwa mkono kutokana na imani yake hiyo ya kujali mahitaji ya watu wa makundi yote.

Aidha, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na wananchi wa Tumbatu katika kujiletea maendeleo bila ya kujali tofauti zao za kisiasa jambo ambalo limekuwa likiutia moyo uongozi wa Mkoa huo kwa kutambua kwamba siasa zina mda wake.

Mapema Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar, Tabia Makame alitoa shukurani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa uwamuzi wake huo wa kuwafikiria wajane wa Tumbatu na kwenda kuwapa sadaka ya futari katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani huku akieleza azma iliyowekwa na Jumuiya ya Wajane ya kutoa mafunzo kwa wajane wajasiriamali wa kisiwa hicho.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya akina mama hao, Sheha wa Shehia ya Tumbatu Jongoe Miza Ali Sharifu alizipongeza juhudi hizo za Mama Mariam Mwinyi na kueleza furaha yao kwa jinsi alivyowajali na kuwathamini.

Baada ya kumaliza zoezi hilo la kugawa sadaka ya futari huko katika kisiwa cha Tumbatu, Mama Mariam Mwinyi alifika kisiwa cha Uzi ambako aligawa sadaka kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 70 wa Shehia ya Uzi na Shehia ya Ng’ambwa, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika hotuba yake Mama Maria Mwinyi alieleza kwamba amechukua juhudi hizo za makusudi kupitia Jumuiya yake za kuwapa wazee hao sadaka ya futari kwa kutambua kwamba wana umhimu mkubwa katika Jamii kutokana kwamba wao ni wazazi na pia ni walezi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadidi Rashid alimpongeza Mama Maria Mwinyi pamoja na jumuiya anayoingoza kwa hatua hiyo ya kwenda kisiwa cha Uzi na kutoa sadaka ya futari kwa wazee 109 wenye umri wa kuanzia miaka 70 jambo ambalo limewapa Faraja kubwa wazee wao.

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma ambaye pia ni Mjumbe wa Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiwathamini sana wazee juhudi ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na Jumuiya hiyo.

Nao wazee hao wa kisiwa cha Uzi walitoa shukurani zao kwa Mama Mariam Mwinyi na kueleza jinsi walivyofarijika na msaada huo na kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu ampe imani zaidi ya kuendelea kuwakumbuka na kuwasaidia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news