NA MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Mara,Samwel Kiboye (Namba Tatu) amepongeza hatua ya Chama Cha Mapinduzi kumpitisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa,Abdulrahman Kinana ambapo amesema anaiona CCM mpya isiyo na makundi.
Amesema, Kinana ni miongoni mwa makada wa CCM ambao wana historia na uwezo mkubwa wa kiutendaji akiwa ndani na nje ya chama.
Kiboye ameyasema hayo leo wakati akizungumzia namna ambavyo alipokea matokeo ya ushindi wa asilimia 100 kwa Kinana kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Awali wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa CCM walimchagua Abdulrahman Kinana kuwa makamu Mwenyekiti wa CCM Bara kwa kura za ndiyo 1875. Katika mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, wajumbe waliopiga kura walikuwa 1875, kura halali 1875 na hakuna za hapana wala zilizoharibika.
"Nampongeza sana Komredi Kinana kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, namfahamu sana Kinana amepigania chama chetu kwa muda mrefu na tunamfahamu ni mtu asiyependa makundi ndani ya chama, tunaamini atamsadia kazi Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,"amesema Kiboye.
Pia Kiboye amesema kuwa, Komredi Kinana ni mtu mwenye kofia nyingi. "Ni askari aliyepitia mafunzo ya kijeshi hadi kufikia cheo cha Kanali. Ni mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
"Aidha ni miongoni mwa wabunge mahiri na baadaye Spika wa Bunge la Kwanza la Afrika Mashariki mwaka 2001.Kwa maana nyingine, Kinana ni mwanasiasa aliyewahi kushika vyeo vya kisiasa kama mbunge, Waziri na Katibu Mkuu wa chama.
"Huyu ni mtu wa mipango na mtekelezaji wa mikakati yenye manufaa mapana kwa jumuiya, kwani aliongoza kampeni nne za urais kwa mafanikio mfano mwaka 1995 na 2000 akiwa Meneja wa Kampeni mgombea w CCM, Hayati Benjamin Mkapa, pia meneja wa kampeni wa Dkt.Jakaya Kikwete mwaka 2010 kabla ya kusimamamia kampeni za Hayati Dkt.John pombe Joseph Magufuli 2015 akiwa Katibu Mkuu CCM Taifa.
"Kwa hiyo, Kinana anaweza kuvaa kofia yoyote kati ya hizo pale anapotaka au inapobidi na kuleta matokeo makubwa sana, kwa nafasi hii ya umakamu mwenyekiti wa CCM Taifa, tutarajie matokeo makubwa maana atamshauri vema na kushirikiana na Mwenyekiti wetu Taifa ili chama kiweze kusonga mbele,"amefafanua Kiboye.
Pia ameongeza kuwa,Kinana ni mmoja wa viongozi wenye wigo mpana wa marafiki ndani na nje ya nchi kuanzia marais, wafanyabiashara maarufu, wanasiasa wa vyama tawala na upinzani na watu wa kawaida ambao wamekuwa muhimu kwake kwa kumwongezea maarifa na taarifa katika majukumu yake tofauti ya kila siku.