NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI mpya wa Bodi ya Benki ya Afrika (Bank of Africa-Tanzania), Nehemiah Kyando Mchechu ameanza kazi rasmi Aprili 5, 2022 katika benki hiyo baada ya kufika katika makao na kuzungumza na menejimenti ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Mchechu anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Dkt.Nyamajeje Weggoro aliyefariki Novemba 2021.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Benki ya Afrika (Bank of Africa-Tanzania), Nehemiah Kyando Mchechu akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya benki hiyo alipomaliza kikao na menejimenti ya benki hiyo.
Akizungumza na Menejimenti ya benki hiyo, Bw. Mchechu ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa sasa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ameitaka benki hiyo kusaidia Taifa la Tanzania kwa kupanua wigo wa huduma zake.
Amewataka kuchapa kazi kwa bidii na kuondoa changamoto zote zinazokabili sekta ya kibenki kwa kuwa mstari wa mbele kutoa ushauri wao.
Amewaahidi kuwapa ushirikiano mkubwa ili kuifanya benki hiyo kuwa na tija zaidi kwa wananchi na uchumi wan chi kwa ujumla.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Benki ya Afrika (Bank of Afrika-Tanzania), Nehemiah Kyando Mchechu akisisitiza jambo wakati akizungumza na Menejimenti ya Benki hiyo (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.
Benki hiyo imeonekana kuwa, thabiti katika kufanikisha uwekezaji uliofanywa nchini Tanzania na imeshiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo tangu 2007.
Pamoja na ushiriki wa benki hiyo katika miradi mbalimbali ya maendeleo, pia imeonyesha dhamira yake katika kusaidia biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa kubuni bidhaa na huduma za kuvutia wateja.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Benki ya Afrika (Bank of Africa-Tanzania), Nehemiah Kyando Mchechu (kushoto) akipokea baadhi ya nyaraka muhimu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Afrika (Bank of Africa-Tanzania), Adam Mihayo (kulia) muda mfupi baada ya kuwasili katika ofisi za makao makuu ya benki hiyo kujitambulisha na kuzungumzia na kuwapa watendaji wa benki hiyo muelekeo wake.
Kama benki ya biashara, benki inayo wateja waliogawanywa katika makundi ya wateja wa Rejareja, Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) na wateja wa Makampuni.
Kampuni hiyo anayoisimamia sasa ina maslahi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi kama vile sekta ya mali isiyohamishika.
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Benki ya Afrika (Bank of Africa-Tanzania), Nehemiah Kyando Mchechu (Kushoto) akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Africa (Bank of Africa-Tanzania, Adam Mihayo (kulia) muda mfupi baada ya kuwasilia katika ofisi za makao makuu ya benki hiyo.
Uteuzi wa Bw.Mchechu ulitokana na uzoefu wa kibenki aliyo nao wa zaidi ya muongo mmoja na amefanya kazi na benki tatu za kimataifa na benki moja ya kikanda katika majukumu mbalimbali ya usimamizi hadi nafasi za juu kabisa.