Mwinjilisti Temba aingia mstari wa mbele kufanikisha maono ya Rais Samia kupitia Royal Tour

NA GODFREY NNKO

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam, Alphonce Temba ameamua kuingia mstari wa mbele kuunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kueneza habari njema kuhusu utalii wa Tanzania, hatua ambayo anaamini kwa kufanya hivyo itawezesha kustawisha uchumi wa jamii na Taifa kupitia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
Temba kutokana na umuhimu wa sekta ya utalii na mchango wa Mheshimiwa Rais Samia katika kuutangaza utalii wa Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour ambayo ilizinduliwa Aprili 18,2022 jijini New York, Marekani, Los Angeles siku ya Aprili 21,2022 huko Marekani huku ikitarajiwa kuzinduliwa Aprili 28,2022 jijini Arusha kabla ya kuelekea jijini Zanzibar amesema, kupitia kituo chake kipya cha Redio Penuel FM chenye masafa ya 105.1 huko Marangu mkoani Kilimanjaro atahakikisha kinakuwa kipaza sauti na balozi mwema katika kuyaeneza maono ya Rais ya kuutangaza utalii wa Tanzania.

"Kwa hiyo redio hii ambayo tunasema ni ya aina yake itahamasisha Watanzania kuwa wazalendo, kupenda vitu vyao hususani maliasili na kulinda mazingira ili yaendelee kudumu vizazi baada ya vizazi.

"Kwa msingi huo ninatarajia kuwa na vipindi maalum vya kuhamasisha Watanzania kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vingine vya utalii vilivyopo ndani na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro na si kusubiri wageni tu kutoka nje.

"Hii inamaanisha nini? Dhamira ni ile ile ya kuunga mkono juhudi za Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amekuja na kampeni mahususi ya Royal Tour ikiwa imejikita kutoa hamasa ya kuwavutia watalii kuja kutembelea vivutio vyetu vilivyopo hapa nchini;

Mwinjilisti Temba ameyasema hayo leo Aprili 26, 2022 wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kuelezea namna ambavyo filamu ya Royal Tour ilivyogusa moyo wake huku akimpongeza Rais Samia kwa ubunifu ambao amesema umedhamiria kuipaisha Tanzania kupitia sekta ya utalii na uwekezaji duniani.

Pia amesema, kupitia redio hiyo wamejipanga kutoa elimu kwa jamii itakayojumuisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali kuanzia serikalini,sekta binafsi, wanajamii ili kuwa na mtazamo chanya kuhusu mali asili za Tanzania.

Amesema, hivi karibuni anatarajia kukizindua rasmi kituo hicho ambacho anaishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuwapa masafa ya 105.1 wakianzia na Marangu huku wakitarajia kuifikia mikoa na nchi jirani siku za karibuni.

Pia amesema kuwa, alipokuwa nchini Botswana hivi karibuni alipata nafasi ya kuwashauri marais wa mataifa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuzisimamia rasilimali za Taifa, kutangaza vivuto vya utalii Kitaifa na Kimataifa ili kupanua soko zaidi.

"Ninamshukuru Mungu kwa kuwa, hata yale ambayo nilikuwa ninashauri ninayaona yakitekelezwa kupitia Royal Tour ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais Samia kwa kuonesha ujasiri, uthubutu na kuingia mwenyewe pori kwa pori kuiongoza filamu hii muhimu kwa Taifa letu.

"Nitamuunga mkono kupitia redio hii katika masafa yake ya kawaida na katika vipindi vya online vitakavyoiendea Dunia yote ili kuhamasisha utalii wa Tanzania,"amesema Mwinjilisti Temba.

Pia maesema, malengo ya siku za usoni ya kituo chake hicho cha redio ni kutumia timu, klabu kubwa za soka ndani na nje ya Tanzania kuhamasisha wazawa na wageni kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vingine vya utalii.

Wakati huo huo, amesema redio hiyo itakuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa Watanzania ili kufahamu madhara ya kujiingiza katika utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.
 
Mwinjilisti Temba amesema, kwa upande wa Marangu redio zaidi ya nne zinazosikika zinatoka nchi jirani, hivyo anaamini Penuel FM ambayo ni redio ya kipekee (very unique) imekuja wakati mwafaka ikiwa imejipambanua kutoa elimu ambayo itakuwa neema kwa wasikilizaji wake.

Aidha, amesema itatoa elimu ili jamii iweze kutambua ukweli kuwa suala la uchomaji moto katika Mlima Kilimanjaro kwa namna moja au nyingine linachochewa na shughuli za matambiko na si urinaji wa asali, hivyo watatumia wataalamu wa jeshi la polisi, zimamoto, wataalamu wa maafa na wengineo ili kutoa elimu ambayo itasaidia kuondokana na hali hiyo.

"Na tutatumia kituo hiki kutoa elimu ili miti ambayo inapotea ambayo ni ya asili kutokana na majanga ya moto iweze kudumu kizazi baada ya kizazi. Tunaamini kupitia kampeni yetu ya Marangu Walking Royal Tour Marathon ambayo inatarajiwa kufanyika mwakani kwa ajili ya upandaji miti, kutunza mazingira kuwezesha barafu isipotee katika mlima Kilimanjaro pia itakuwa chanzo kikuu cha hamasa kwa watu kuthamini utalii wa ndani.

Amesema, kupitia kampeni hiyo ya Marangu Walking Royal Tour Marathon itakuwa, "Ni mahususi au njia pekee ya kusimamia na kukumbusha kilichozinduliwa kule Marekani na Mheshimiwa Rais Samia siku ya Aprili 18,2022.

"Itakuwa ni moja ya kichochea au mdau muhimu wa kuitatafsri filamu ya Royal Tour neno kwa neno, na faida yake ili Watanzania waweze kujua ukubwa wa jambo ambalo Mheshimiwa Rais ameifanya, kwa maslahi mapana ya taifa, tumeamua kufanya hivyo, kutokana na Watanzania kuwa na tabia ya kusahau baadhi ya mambo kwa muda mfupi, ni wazi, tangu uhuru hatujawahi kumpata kiongonzi mwenye maono ya namna hii katika kufanya jambo la kipekee kupitia sekta wa utalii kama hili, hongera sana Mheshimiwa Rais Samia,"amesema.  

"Nitaendelea kuheshimu maono ambayo yatastawisha taifa, kuchochea ajira kwa vijana ili kuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, kwani Kilimanjaro imejaliwa kuwa na miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara, umeme. Hivyo kupitia redio hii, tutaendelea kuibua vipaji vya vijana kwa ajili ya kuziendea ndoto zao, kwa mfano kuibua vijana ambao watashiriki katika mbio za Marathon ili kushiriki michuano ya Kimataifa ili nao waweze kuwa na mafanikio makubwa kupitia michezo hiyo.

"Vipaji hivyo vitaibuliwa kuanzia vijijini hadi mijini ikiwemo vipaji vya kuruka kamba, kucheza rede, tutajikita zaidi katika vipaji ambavyo havijawahi kuzungumziwa ikiwemo kikapu, judo, hii michezo ina fedha na wengi wanapata fedha nyingi sana kupitia vipaji hivyo mfano kina Simbu,Filbert Bayi, Juma Ikangaa, Suleiman Nyambui, Gidamis Shaganga, Mwinga Mwanjala, Nzaeli Kyomo na wengi wengine ambao walikuwa wanang’ara kwenye Medani za Kimataifa.

Mwinjilisti Temba ni kati ya watumishi wa Mungu ambao wamekirimiwa vipawa vya kipekee (unusual anointing) ambapo kati ya matukio ambayo Mungu amemtumia katika mambo makubwa ni pamoja na kumtabiria na kumuombea aliyekuwa rais wa Zambia, Frederick Jacob Titus Chiluba ambapo mwaka 2004, Mungu alimtuma kwenda Zambia nyumbani kwake Kabulonga kumuombea na kuifuta kesi iliyokuwa inamkabili chini ya utawala wa rais wa kipindi hicho,Levy Patrick Mwanawasa mwaka 2006 ambapo alimtabiria Rais Mwanawasa kuwa angeshinda Uchaguzi wa mwaka huo.
Lakini asingedumu katika Urais wake baada ya kifo cha Mwanawasa, Mwinjilisti Temba pia alifunguliwa na Mungu juu ya kiongozi wa upinzani nchini Zambia wa chama Cha PF, Michael Satta kuwa angekuwa rais baadaye na akafanikiwa kushinda urais.

Hivi karibuni, Mwinjilisti Temba alitabiri ushindi wa chama cha upinzani nchini Zambia na alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa, mwaliko kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama tawala nchini Zambia (UPND) Taifa, Stephen Katuka kilichomwingiza madarakani,Hakainde Hichilema.

Wakati huo huo, Kamati ya Viongozi wa dini nchini Zambia imempendekeza Mwnjilisti Temba kuwa miongoni mwa washauri wa rais.

Baada ya kutoka Zambia, Mwinjilisti Temba aliitwa Ikulu ya Botswana na kukutana na Waziri anayehusika na Masuala ya Rais, Utumishi na Utawala wa Umma, Mheshimiwa Kabo Neale Sechele Morwaeng.

Akizungumza baada ya kuwasili Botswana, Mwinjilisti Temba amesema, ameendelea kuitikia wito wa Mungu wa kwenda kutamka neno la uponyaji na ushindi kwa mataifa mbalimbali Kusini mwa Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news