NA FRESHA KINASA
NAIBU Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Mheshimiwa Haji Mtete amewataka Watumishi wa Kituo cha Afya cha Bweri kilichopo katika manispaa hiyo, kufanya kazi kwa weledi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Mheshimiwa Mtete amesema kuwa, yapo baadhi ya malalamiko yamekuwa yakitolewa na wananchi wakilalamikia huduma katika kituo hicho ikiwemo lugha zisizofaa ambazo hutolewa na baadhi ya watumishi kwa wagonjwa wanapofika kutibiwa kituoni hapo na kupelekea baadhi ya watu kutokwenda kutibiwa katika kituo hicho pindi wanapougua jambo ambalo halifai.
"Wapo wagonjwa wanakuja na kadi za CHF zilizobooreshwa, lakini wanaambiwa kadi zao hapa hazifanyi kazi. Serikali inatumia nguvu kubwa kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF kama kadi ya mgonjwa ina tatizo, umeigundua mwambie kwa lugha nzuri sio kumfokea. Tumieni lugha zinazofaa kwa wananchi, na pia uongozi wa kituo uwe haraka kutoa taarifa ngazi husika pale kunapokuwa na upungufu wa vifaa au jambo lolote badala ya kukaa kimya hadi wananchi wanaanza kufikisha malalamiko yao ngazi za juu wakati uongozi wa kituo umekaa kimya,"amesema Mheshimiwa Mtete.

Kwa upande wake Dkt.Magreth Shaku ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, alipongeza hatua za Naibu Meya kukaa pamoja na watumishi hao na kuwakumbusha wajibu wao, huku pia akiwasisitiza kuzingatia misingi yao ya kazi sambamba na kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
"Niwasihi Watumishi fanyeni kazi kwa nidhamu na pia tusichafua image nzima ya halmashauri yetu, hivi karibuni tilifanya kikao tukakumbushana juu ya uwajibikaji,lakini bado. Mtumishi ukitoa kauli mbaya kwa mgonjwa lawama zinaelekezwa serikalini jambo ambalo halifai, toeni kauli njema kwa wagonjwa ili kusudi kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi juu yenu. Muwe na hofu ya Mungu mnapotekeleza majukumu yenu ili mtoe huduma bora,"amesema Dkt. Shaku.
Diwani wa Kata ya Bweri, Mheshimiwa Nickson Mwandala alibainisha kwamba, amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakilalamikia baadhi ya watumishi kufanya kazi kinyume cha taratibu.
"Haipendezi mgonjwa anapofika kutibiwa aondoke kwa manung'uniko, niwahimize sana ndugu zangu hakikisheni mnawatendea haki wananchi wanaofika kupata matibabu, haipendezi kituo kiwe na sifa mbaya lindeni heshima ya kituo hiki na mzidi kusifika kwa wema kwani wananchi wanawapima kwa kile mnachokifanya,"amesema Mheshimiwa Mwandalala.