NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Tanzania imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi nne wanachama wa Jumuiya ya Afrika, Karibiani na Pasifiki (Organization of African, Caribbean and Pacific States-OACPS) zitakazonufaika na Programu ya Ufadhili wa Umoja wa Ulaya wenye thamani ya Euro milioni 11.1 (shilingi bilioni 30) katika Sekta ya Madini.
Programu hiyo inayoitwa OACPS-EU Development Mineral Programme inalenga kuboresha mazingira ya uchimbaji madini na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo hususani vijana na wanawake katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022-2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mwasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, uamuzi huo umetangazwa na Sekretarieti ya OACPS ambayo ina makao makuu Brussels nchini Ubeligiji.
Mbali na Tanzania, nchi zingine tatu za Jumuiya ya Afrika, Carribean na Pacific zilizofanikiwa kuchaguliwa kwenye programu hiyo ya awamu ya pili ni Burkinafaso, Jamhuri ya Kongo na Suriname.