NA OR-TAMISEMI
TIMU ya ufuatiliaji wa shughuli za afya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeridhishwa na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika vituo vya afya unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Timu hiyo imeipongeza Halmashauri ya Ngara kwa usimamizi mzuri na kuitaka halmashauri hiyo kufanya ukarabati mdogomdogo kwenye maeneo ambayo yamebainishwa kuwa na mapungufu.
Wito huo umetolewa Aprili 27, 2022 katika ziara ya usimamizi shirikishi uliofanywa na timu hiyo kufuatilia utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika halmashauri hiyo.
Aidha, timu hiyo imeitaka Kamati Tendaji ya Usimamizi wa Shughuli za Afya katika halmashauri hiyo kufanya ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya ili kuepusha upotevu.
Kwa upande mwingine timu hiyo imewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kushirikiana na Serikali katika kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya ili kuimarisha ulinzi shirikishi, lakini pia kurahisisha utekelezaji utakaopelekea ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.