*Ni zile zilizopatiwa fedha kujenga shule za sekondari za wasichana
NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.David Silinde ameziagiza halmashauri zote nchini zilizopatiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kuandika taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya ujenzi wa shule hizo na kuziwasilisha Ofisi ya Rais-TAMISEMI ndani ya siku saba.
Mhe. Silinde amesema kuwa jumla ya shule za wasichana 15 zinajengwa katika halmashauri nchi nzima ambapo kila shule ilipelekewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa Mhe. Silinde amesema, hakuridhishwa na ubora wa majengo yaliyojengwa katika shule hiyo, matumizi ya fedha zilizotumika katika ujenzi huo na thamani ya fedha zilizotumika kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi sasa haijakamilika.
Mhe. Silinde amesema kuwa, hatasita kuwachukulia hatua wale wote ambao watashindwa kukamilisha ujenzi wa shule za sekondari za wasichana kwa wakati kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha elimu bora inatolewa katika mazingira bora.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt.Omary Mkulo ameeleza kuwa, kiasi cha shilingi milioni 464.5 zinahitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo ambayo hadi sasa imefika asilimia 68. 14 ujenzi na fedha iliyotumika ni shilingi milioni 993.8.