OR-TAMISEMI:Hotuba yote ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2022/23

HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, MHESHIMIWA INNOCENT LUGHA BASHUNGWA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

A. UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu,mwingi wa rehema, kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

2. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa likubali kupokea na kujadili, Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Fungu 56), Tume ya Utumishi wa Walimu (Fungu Na. 2) na Mafungu 26 ya Mikoa ikijumuisha Halmashauri (184) kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Aidha, naomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Bajeti ya Ofisi ya
Rais - TAMISEMI (Fungu 56), Tume ya Utumishi wa Walimu Fungu (Na. 2) na Mafungu 26 ya Mikoa ikijumuisha Halmashauri (184) kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

3. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa ninampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari na vituo shikizi, fedha hizi zimewezesha kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.

Aidha, jitihada hizo zimewezesha pia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa
mabweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi, ujenzi wa majengo ya wagonjwa mahututi, majengo ya kutolea huduma za dharura, nyumba za watumishi katika sekta ya afya, mashine za mionzi, mitambo ya kuzalisha hewa ya Oksijeni, kituo cha matibabu cha magonjwa ya kuambukiza na ununuzi wa magari ya kubeba wagonjwa kwa kila Halmashauri na magari ya usimamizi katika ngazi ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mikoa na Halmashauri.

4. Mheshimiwa Spika, natoa pole kwako, Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na wapendwa wetu Mheshimiwa Elias Kwandikwa, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Mbunge wa Jimbo la Ushetu; Mheshimiwa William Tate Olenasha aliyekuwa Naibu Waziri wa Uwekezaji (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro; na Mheshimiwa Khatibu Said Haji aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Konde Zanzibar).

Aidha, napenda kutumia fursa hii kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa wa marehemu, marafiki na watanzania wenzangu kwa kuondokewa na wapendwa
wao. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi, Amina.

5. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Spika Mheshimiwa Hassan Mussa Zungu Mbunge wa Jimbo la Ilala kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuongoza Mhimili wa Bunge. Tunakuahidi kukupa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yako.

6. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Wenyeviti wa Bunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb) na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb) kwa kuendelea kukusaidia katika kutekeleza majukumu ya kuongoza Bunge lako.

7. Mheshimiwa Spika, kipekee napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI).

Ninamshukuru pia kwa kuendelea kuwaamini Mheshimiwa Dkt. Festo John Dugange,
Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe na Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Jimbo la Tunduma kuwa Naibu Mawaziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara. 

Aidha, namshukuru Mheshimiwa Rais kuendelea kumuamini Katibu Mkuu, Profesa Riziki Silas Shemdoe, Naibu Makatibu Wakuu; Dkt. Grace Elias Magembe (Afya), Bw. Gerald Geofrey Mweli (Elimu) na kumteua Dkt. Switbert Zacharia Mkama kuwa Naibu Katibu Mkuu (TAMISEMI).

8. Mheshimiwa Spika, tunamuahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watanzania kuwa tutaendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, ubunifu, uaminifu na utiifu kwake, na kwa nchi yetu, katika kumsaidia kusimamia shughuli za utawala na maendeleo katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, hususan kwa kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaongeza ubunifu kwa kuongeza vyanzo vipya, kuimarisha vyanzo vilivyopo, na mbinu katika ukusanyaji wa Mapato ya Ndani, bila kusababisha kero
kwa wananchi.

Aidha, Mapato hayo yatumike katika kutekeleza vipaumbele vilivyowekwa,
ikijumuisha Miundombinu ya huduma za Afyamsingi na Elimumsingi, barabara, Majengo ya Utawala, Makazi ya Viongozi na watumishi, Ununuzi wa Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi,na kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo. 

Vilevile, tutaongeza jitihada za kusimamia matumizi ya fedha za umma katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

9. Mheshimiwa Spika, kipekee, nampongeza Mheshimiwa Abdallah Jaffari Chaurembo,
Mbunge wa Jimbo la Mbagala, kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa Denis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati, pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa mchango wao mkubwa, katika kuchambua utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais– TAMISEMI (Fungu 56), Tume ya Utumishi wa Walimu (Fungu Na. 2) na Mafungu 26 ya Mikoa ikijumuisha Halmashauri 184 kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Aidha, Kamati ilijadili kwa kina Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mafungu yote 28, kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 na kupitisha kwa kauli moja. Vilevile, Kamati imekuwa ikitoa ushauri ambao umesaidia kuboresha utendaji wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Tume ya Utumishi wa Walimu na Taasisi nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

10. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kusimamia kikamilifu, kwa dhati na kwa umakini mkubwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na Malengo Endelevu ya Maendeleo (2030).

B. UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2021/22

11. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Taasisi zake, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa iliidhinishiwa kukusanya Maduhuli na Mapato ya Ndani, jumla ya Shilingi bilioni 916.44.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 52.36 ni ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Taasisi zake, Shilingi milioni 220.68 ni Maduhuli ya Mikoa, na Shilingi bilioni 863.85 ni Mapato ya Ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, hadi Februari 2022 jumla ya Shilingi bilioni 615.61 zimekusanywa, sawa na asilimia 67.17 ya bajeti iliyoidhinishwa.
 

12. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Fungu56), Tume ya Utumishi wa Walimu (Fungu Na. 2) na Mafungu 26 ya Mikoa ikijumuisha Halmashauri 184 iliidhinishiwa bajeti ya jumla ya Shilingi trilioni 8.56, ambapo Shilingi trilioni 4.72 ni Matumizi ya Kawaida, yakijumuisha Mishahara Shilingi trilioni 3.97, Shilingi bilioni 755.85 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo, na Shilingi trilioni 3.84 ni Fedha za Maendeleo (Kiambatisho Na. 1).

13. Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022 Mafungu 28 ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI,
yamekusanya na kupokea kiasi cha Shilingi trilioni 5.33, sawa na asilimia 62.26 (Kiambatisho Na. 1). Mchanganuo kwa kila Fungu ni kama ifuatavyo: -

Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Taasisi zilizo chini yake (Fungu 56)

14.Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Taasisi zilizo chini yake, iliidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.04.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 57.51 ni mishahara, ambapo Shilingi bilioni 10.27 ni za Ofisi ya Rais – TAMISEMI Makao Makuu,na Shilingi bilioni 47.23 ni za Taasisi; Shilingi bilioni 11.37 ni za matumizi mengineyo ambapo Shilingi bilioni 10.05 ni kwa ajili ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI Makao Makuu na Shilingi bilioni 1.31 ni za Taasisi.

Aidha, Shilingi bilioni 973.82 ni za miradi ya maendeleo ambapo fedha za ndani ni Shilingi bilioni 773.66 na fedha za nje ni Shilingi bilioni 200.15.

15. Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022 Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Fungu 56) imepokea jumla ya Shilingi bilioni 670.36. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 38.17 ni kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 66.38 ya fedha zilizoidhinishwa.

Aidha, Shilingi bilioni 8.83 ni matumizi mengineyo, sawa na asilimia 77.66, na Shilingi bilioni 623.35 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sawa na asilimia 64.01. Vilevile, Fedha za Maendeleo zinajumuisha Shilingi bilioni 526.13 fedha za ndani na Shilingi bilioni 97.22 fedha za nje. (Kiambatisho Na. 1)

Tume ya Utumishi wa Walimu (Fungu Na.2)

16. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 14.86, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 7.76 ni kwa ajili ya mishahara, Shilingi bilioni 6.60 ni matumizi mengineyo, na Shilingi milioni 500.00 kwa ajili ya mradi wa maendeleo.

17. Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022 Tume ya Utumishi wa Walimu (Fungu Na. 2) imepokea jumla ya Shilingi bilioni 9.51, sawa na asilimia 64.01 ya fedha zilizoidhinishwa.

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 5.25 ni kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 67.69, Shilingi bilioni 3.75 matumizi mengineyo sawa na asilimia 56.95, na Shilingi milioni 500.00 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume Makao Makuu Dododma sawa na asilimia 100 ya fedha zilizoidhinishwa (Kiambatisho Na. 1).

Mafungu 26 ya Mikoa ikijumuisha Halmashauri 184 Tawala za Mikoa

18. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Mikoa iliidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 242.84. 

Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 71.26 ni mishahara, Shilingi bilioni 57.44
matumizi mengineyo, na Shilingi bilioni 114.12 miradi ya maendeleo ambayo inajumuisha Shilingi bilioni 90.32 fedha za ndani, na Shilingi bilioni 23.79 fedha za nje.

19. Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022 Mikoa ilipokea jumla ya Shilingi bilioni 173.99, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 45.58 ni kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 64.34, Shilingi bilioni 48.03 matumizi mengineyo, sawa na asilimia 83.62, na Shilingi bilioni 80.37 kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 70.42, ambapo fedha za ndani ni Shilingi bilioni 71.41 na fedha za nje ni Shilingi bilioni 8.95 (Kiambatisho Na. 1).

Halmashauri 184

20. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Halmashauri ziliidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 7.26, kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 3.83 ni kwa ajili ya mishahara, Shilingi bilioni 680.42 ni Matumizi Mengineyo yakijumuisha Shilingi bilioni 147.65 ruzuku kutoka Serikali Kuu, na Shilingi bilioni 532.77 Mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Aidha, Shilingi trilioni 2.75 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo Shilingi bilioni 957.51 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu, Shilingi bilioni 331.08 ni Mapato ya Ndani ya Halmashauri na Shilingi trilioni 1.46 ni fedha za nje.

21. Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022 Halmashauri zimepokea jumla ya Shilingi trilioni 4.47, kati ya fedha hizo Shilingi trilioni 2.64 ni kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 68.96, Shilingi bilioni 492.66 sawa na asilimia 72.41 ni matumizi mengineyo, yakijumuisha Shilingi bilioni 122.70 ruzuku kutoka Serikali Kuu, na Shilingi bilioni 369.96 Mapato ya Ndani ya Halmashauri.

Aidha, Shilingi trilioni 1.34 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sawa na asilimia
48.75 zikijumuisha Shilingi bilioni 696.25 ruzuku ya Serikali Kuu, Shilingi bilioni 216.11 Mapato ya Ndani ya Halmashauri, na Shilingi bilioni 429.10 ni fedha za nje (Kiambatisho Na. 1).

Fedha za Nyongeza za Miradi ya Maendeleo

22. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliidhinishiwa fedha za nyongeza Shilingi bilioni 686.55 ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 512.14 zimetokana na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO- 19 (TCRP); Shilingi bilioni 93.00 zimetokana na Tozo za Miamala ya simu; Shilingi bilioni 7.76 kutoka kwenye Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (SRWSS); Shilingi bilioni 17.25 kutoka Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R).

23. Mheshimiwa Spika, fedha nyingine za nyogeza ya bajeti ni Shilingi bilioni 12.62 kutoka Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa ElimuMsingi Awamu ya Pili (GPE-LANES); Shilingi bilioni 8.24 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA); Shilingi bilioni 2.98 kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi (walimu wastaafu); Shilingi bilioni 9.19 kwa ajili ya utoaji wa chanjo; na Shilingi bilioni 22.87 ni kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

24. Mheshimiwa Spika, hadi Februari, 2022 zimepokelewa jumla ya Shilingi bilioni 535.07 ambapo Shilingi bilioni 360.66 ni kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO - 19 (TCRP); Shilingi bilioni 93.00 ni za Tozo za Miamala ya simu; Shilingi bilioni 7.76 kutoka kwenye Programu Endelevu ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (SRWSS); Shilingi bilioni 17.25 kutoka Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R).

25. Mheshimiwa Spika, fedha nyingine zilizopokelewa ni Shilingi bilioni 12.62 kutoka Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa ElimuMsingi Awamu ya Pili (GPE-LANES); Shilingi bilioni 8.24 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA); Shilingi bilioni 2.98 kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi (walimu wastaafu); Shilingi bilioni 9.19 kwa ajili ya utoaji wa chanjo; na Shilingi bilioni 22.87 ni kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2021/22
26. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Halmashauri zimetekeleza shughuli zifuatazo: -

HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI

27. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliidhinishiwa Shilingi bilioni 28.20 kupitia ruzuku ya Serikali Kuu kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa maboma 564 ya Zahanati katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hadi kufikia Februari 2022, zimepokelewa Shilingi bilioni 23.32 sawa na asilimia 82.69 ya fedha zilizoidhinishwa. Ukamilishaji wa ujenzi upo katika hatua mbalimbali (Kiambatisho Na. 2).

28. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Shilingi bilioni 110.60 ziliidhinishwa kupitia ruzuku ya Serikali Kuu kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya 304. 

Kati ya hivyo, Vituo 52 vilianza kujengwa Mwaka wa Fedha 2019/20 na Vituo 252 vimeanza kujengwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ambapo Vituo 18 vimejengwa kwenye Halmashauri zenye Mapato madogo na Vituo 234 vimejengwa katika Tarafa zisizo kuwa na Vituo vya Afya na Kata za Kimkakati kupitia tozo za miamala ya simu.

Hadi Februari, 2022 Shilingi bilioni 108.05 zimepokelewa sawa na asilimia 97.69 ya fedha zilizoidhinishwa na ujenzi unaendelea (Kiambatisho Na. 3).

29. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Serikali ilitenga Shilingi bilioni 81.10 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali 68 zilizoanza kujengwa mwaka 2018/19, Hospitali 31 zilizoanza kujengwa mwaka 2019/20 na kuanza ujenzi wa Hospitali mpya 28.

Hadi Februari, 2022 Shilingi bilioni 66.80 sawa na asilimia 82.36 zilikuwa zimepokelewa na ujenzi upo katika hatua mbalimbali (Kiambatisho Na. 3).

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliidhinishiwa Shilingi bilioni 11.30 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa Hospitali 31 za Awamu ya Pili zilizoanza kujengwa katika Mwaka wa Fedha 2018/19. Hadi Februari, 2022 zimepokelewa Shilingi bilioni 5.83 sawa na asilimia 51.59 ambapo fedha hizi zimepelekwa kwenye Halmashauri kumi na moja (11) kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaa tiba (Kimbatisho Na. 3).

Utekelezaji wa Miradi kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19

31. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuimarisha huduma za Afya ya Msingi, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepokea Shilingi bilioni 52.16 kati ya Shilingi bilioni 203.14 sawa na asilimia 25.67 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya afya kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

32. Mheshimiwa Spika, fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa majengo 28 ya wagonjwa mahututi (ICUs); majengo 80 ya dharura (EMDs), nyumba 150 (3 in 1) kwa ajili ya watumishi wa Afya zinazoendelea kujengwa katika maeneo ya pembezoni; ujenzi wa kituo cha matibabu ya magonjwa ya mlipuko katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu; ajira 150 za mkataba kwa watumishi wa sekta ya Afya pamoja na uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO - 19.

Utekelezaji wa ujenzi upo katika hatua mbalimbali na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei,2022.

33. Mheshimiwa Spika, vilevile, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilipokea Shilingi bilioni 9.19 kutoka Shirika la Global Alliance for Immunization (GAVI) kwa ajili ya utoaji wa chanjo ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO – 19 ambapo mafunzo kwa watoa huduma za afya, utoaji wa chanjo kwa njia ya mkoba na tembezi, uhamasishaji wa jamii na usimamizi wa usambazaji wa chanjo za UVIKO – 19 ulifanyika katika Mikoa yote 26 na Mamlaka za Serikali za Mitaa 184.

Huduma za Ustawi wa Jamii

34. Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai 2021 hadi Februari 2022 mashauri 57,088 ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa. Kati ya hayo, mashauri 38,464 sawa na asilimia 67 ni ukatili dhidi ya wanawake na 18,624 sawa na asilimia 33 ni ukatili dhidi ya watoto.

Mashauri 53,199 yalitatuliwa na Ofisi za Ustawi wa Jamii ngazi ya Halmashauri
na mashauri 3,889 yalifikishwa mahakamani ambapo mashauri 1,501 sawa na asilimia 39 yametolewa hukumu.Endelea kwa kupakua hotuba yote hapa>>>

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news