Orodha ya taasisi, mashirika, wizara na wadau waliotoa salamu za Kumbukizi ya Miaka 50 ya Kifo cha Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Abeid Amani Karume


Ni miaka 50 sasa imepita tangu Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kuuawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi (ASP) visiwani Zanzibar mnamo Aprili 7, 1972.
Aidha,hadi leo hakuna ukweli thabiti juu ya kifo cha Hayati Karume maana wengine wanakihusisha na chuki za siasa na mengineyo.

Wakati fulani, mjane wa Karume, Bi. Fatma Karume aliwahi kukaririwa akisema hakuwa akifahamu kifo cha Mzee Karume mpaka alipokuja kuambiwa na mdogo wake kuwa ameona gari ya mzee imetoka bila ya kuwa na mtu ndipo alipojaribu kumpigia Kamishna wa Polisi enzi hizo Mzee Kisasi,lakini hakufanikiwa kumpata kwa kuwa naye alikuwa ameshaenda hospitalini alipokuwa amehifadhiwa baada ya kupigwa risasi.

"Akaja mdogo wangu masikini marehemu kwa sasa, akaniambia dada nimetoka huko nje kubaya kuna risasi zinalia lakini nimekuta gari ya mzee inakwenda huko, mzee hayupo kwenye gari.

"Mimi nikajikaza nikamwambia hapana mzee hawezi kutumia gari hiyo sasa hivi pengine wameteua gari nyingine kumuondosha. Nikampigia simu kisasi alikuwa Kamishna wa Polisi kipindi hicho, lakini akapokea mke wake na kuniambia mzee hayupo ameenda kwenye tukio hili lililotokea, nikamuuliza wapi akaniambia hospitali nikaingiwa na mashaka nikaanza kukumbuka aliyoniambia mdogo wangu;

Aidha, Bi. Fatma alisema alipofika katika Hospitali ya Muungano alizuiliwa kuingia ndani na wanajeshi waliokuwa wametanda eneo hilo kwa bahati nzuri mwanaye Haji Mrisho naye alikuwa ni miongoni mwa wale wanajeshi akapata wepesi wa kuingia na kumuona Karume akiwa amelazwa chini ameshafunikwa shuka.

Kwa vyovyote vile, jina la Abeid Karume haliwezi kusahaulika katika historia ya ukombozi visiwani humo kutokana na misingi aliyowajengea Wazanzibar. Uongozi wa DIRAMAKINI BLOG unaungana na Watanzania wote katika Kumbukizi ya Hayati Abeid Amani Karume, shujaa wetu ambaye atakumbukwa daima.





Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news