NA GODFREY NNKO
DAWA za kulevya zimekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike.
Kutokana na janga hilo, familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya Taifa imepotea, kwani dawa hizo zina madhara makubwa, ambayo yanaathiri maisha ya wananchi, uwezo wa rasilimali watu na maendeleo endelevu ya nchi.
Ni kutokana na utumiaji wa kemikali hizo ambazo ziingiapo mwilini huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia kuwa na matendo, hisia, fikra na muonekano tofauti na matarajio ya jamii.
Kemikali hizi hutokana na mimea na madini ambayo ni mali ghafi muhimu kwa mahitaji mengine ya mwanadamu.
Dawa hizi huingia mwilini kwa njia kuu tatu ikiwemo kwa njia ya kunywa au kula,kuvuta na kujidunga sindano.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inashirikisha wananchi na wadau wote kuanzia mijini hadi vijijini ili kuifanya Tanzania kuwa salama bila dawa za kulevya.
Kwa kutambua athari zitokanazo na dawa za kulevya, Serikali imeendelea kupambana na tatizo hilo kwa kuzuia biashara, kuimarisha utoaji wa elimu pamoja na upanuzi wa tiba kwa waathirika wa dawa hizo.
Aidha, ushirikiano katika mapambano hayo umezidi kuimarishwa kitaifa, kikanda na kimataifa kwa kuwa tatizo hili ni mtambuka na linaathiri jamii yote na kuvuka mipaka ya nchi yetu.
Ilani
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025 inatambua umuhimu wa kupambana na tatizo la dawa za kulevya, kwa kuwa tatizo hilo linaathiri Watanzania katika nyanja zote muhimu ikiwemo afya, jamii, uchumi, mazingira, diplomasia pamoja na ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Kwa muktadha huo, Ibara za 83(t) na 244 (a) hadi 244 (l) zinasisitiza kuimarisha udhibiti na mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
Jitihada zinazofanyika kwa kwa sasa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) ni pamoja na kuvunja mitandao mikubwa ya wafanyabiashara ya dawa za kulevya na kufanya operesheni za ukamataji kuanzia nchi kavu, baharini na angani.
DCEA ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Sheria
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha Novemba 8, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, Machi 24,2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi Septemba 15, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu Februari 17, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
Licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kufanya na Serikali ili kuhakikisha biashara na utumiaji wa dawa za kulevya nchini hauna nafasi, bado ushirikiano unahitajika zaidi kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha janga hilo ambalo limewasababishia maumivu vijana, watumishi, jamii na Taifa kwa ujumla linatokomezwa.
Athari hasi
Kuna Watanzania wengi ambao dawa za kulevya zimegeuza historia nzuri ya maisha yao katika jamii, utumishi wa umma na familia kuwa mbaya na hatari, lakini baada ya kujutia na kujirudi wamejikuta kuwa walimu wazuri ambao wanaokoa wengine katika janga hilo, miongoni mwao ni Bw.Twaha Amani.
Twaha Amani ni nani?
Bw.Amani ni mzaliwa wa Pasua Mkoa wa Kilimanjaro ambaye alizaliwa Aprili 13,1983 katika Hospitali ya KCMC, alipata elimu ya msingi na kufaulu kwenda sekondari na baadae kidato cha tano na sita ya Singe High School iliyopo wilayani Babati Mkoa wa Manyara.
Bw.Twaha Amani akionekana katika sura tofauti moja ikiwa ya kudhoofika (kushoto) wakati akitumia dawa za kulevya na kulia ni muonekano wake baada ya kuamua kuacha kutumia dawa za kulevya. (Picha na Twaha Amani).
Akiwa kidato cha pili, Bw.Amani alijikuta ni mtumwa wa matumizi ya bangi mpaka kidato cha nne na hata alipomaliza na kufaulu kidato cha tano bado aliendelea kuvuta bangi.
Katika mahojiano na DIRAMAKINI anasema kuwa, bangi ilikuwa ndiyo kila kitu kwenye maisha yake ya kila siku na bila bangi mambo hayawezi kwenda sawa, hasa kabla ya kuanza kusoma au kufanya chochote mpaka alipomaliza kidato cha sita.
"Wakati nikiwa nyumbani ninasubiri matokeo kwa ajili ya kwenda chuo, niliamua kuanza kazi ya kunyoa nywele, kwani ni kazi ambayo niikuwa na uzoefu nao hapo awali.
Kinyozi
"Nikiwa kwenye hiyo kazi ya kinyozi, nilinunua mashine nikawa pia ninamkodishia jamaa mmoja eneo la jirani, hivyo jioni nikifunga nilikuwa ninapitia kwake kuchukua fedha zangu, basi siku moja nikiwa ninaenda pale kwa jamaa yangu, nilikuta jamaa ambaye alikuwa ana tabia ya kufika pale saluni ya yule jamaa akiwa na dawa aina ya Heroine na akawa anazitengenezea pale pale na kuvutia hapo hapo,"anasema Bw. Amani.
Lakini wakati akiwa hapo, Bw. Amani anasema, kwenye hiyo saluni akamuona jamaa akiwasha huo unga na kuvuta na yeye akajaribu kuwasha bangi yake yule mwenye saluni alimzuia jambo ambalo lilimshangaza kwa nini yeye akiwasha anakatazwa.
"Lakini huyu wa unga hakatazwi, ndipo nilianza kuuliza na kufuatilia na kutaka kujua huu unga ni wa aina gani, kwani unanukia kama sigara, nikajaribu kumuuliza akaniambia si nijaribu kuvuta, hilo ndilo likaniponza la kutaka kudadisi.
Safari ya Heroine
"Kweli siku ya kwanza alinipa nikavuta kama pafu mbili...tatu nikajisikia mtu wa tofauti nikapata msisimko ambao sijawahi kuupata katika maisha yangu yote siku hiyo sikulala kabisa, kulivyokucha nikapata mshangao na kutaka kuwe usiku haraka ili niende saluni kuchukua hela yangu, lakini lengo langu nimuone huyo bwana.
"Siku ya pili nilipomsogelea karibu akajua tayari nimeupenda huo unga ikabidi anipe niwashe mwenyewe akanitegeshea unga mwingi mbele (roketi), akanipa nikawasha nikavuta pafu moja...mbili akaninyang'anya haraka, nilijisikia wa tofauti sana.
"Kesho yake akanipa kidogo na aliniambia nimchangie mia sita ili tuchukue na kuvuta wote kweli tulivuta wote na safari yangu ya unga ilianzia hapo na wakati nikifanya huo uvutaji ilikuwa mwaka 2006, nilikuwa nimeshamaliza kidato cha sita na matokeo ya chuo yalishatoka nilipata divisheni three,"anafafanua.
Heroine ni nini?
Ni aina ya dawa ya kulevya inayotengenezwa na kemikali ya asili inayoitwa ‘morphine’ ambayo inapatikana kwenye utomvu ‘opium’ wa tunda la mmea wa afyuni ‘opium poppy’ unaolimwa zaidi kwenye nchi za Afghanstan, Myanmar na Laos.
Hapa nchini, kwa mujibu wa DCEA, heroine inashika nafasi ya pili kwa matumizi baada ya bangi, na inatumiwa kwa njia ya kuvuta ikiwa imechanganywa na kiasi kidogo cha bangi na sigara au kwa njia ya kunusa na kujidunga.
Aidha, heroine ni kati ya dawa za kulevya zinazoongoza kwa kusababisha uteja haraka, vifo vinavyotokana na kuzidisha kiasi cha matumizi au maradhi mbalimbali, pia ni dawa ambayo ina watumiaji wengi wanaohitaji tiba.
Heroine hujulikana kwa majina ya mtaani kama unga, ngada, teli (cocktail), msharafu, white, kijiwe, brown ambapo utumiaji wa dawa hizi huweza kusababisha madhara mbalimbali kwa wahusika ikiwemo kiafya, kijamii na kiuchumi.
Sheria inasemaje?
Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kujihusisha na heroine kwa namna yoyote katika taifa letu ni kosa la jinai.
Kwa hiyo, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kuuza, kuhifadhi, kusambaza, kutumia na kutengeneza heroine ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.
Utamsaidiaje mtumiaji?
Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Wanaweza kupatiwa tiba ya methadone inayopatikana kwenye baadhi ya vituo vya afya.
Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi na huduma nyingine. Vilevile, nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ huwasaidia kwa kuwapitisha kwenye hatua 12 za upataji nafuu.
Ajira TANESCO hadi Polisi
"Wakati huo matokeo ya chuo yalishatoka nikivuta unga, nilipata ajira ya muda ya kusoma mita za umeme TANESCO, ndipo unga uliendelea maana tayari nina fedha na wakati huo nilikuwa na mpenzi wangu ambaye alinishtukia akiniuliza mbona nimebadilika kwenye mwili wangu ila nilikuwa namkwepa kwepa bila kumwambia ukweli,"anafafanua Bw.Amani wakati akifanya mahojiano kwa kina na DIRAMAKINI.
Bw. Amani anasema, akiwa mtaani alikuja mjomba wake mmoja, "Unajua sisi tulikuwa na kama undugu na Said Mwema (aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania) maana mama yake yeye ni wa Machame na mama yangu anatokea huko, hivyo kukitokea shida tunasaidiana ni kama ndugu, hivyo Anko yangu akawa ameongea na Said Mwema kuwa, kuna kijana wangu kamaliza form six (kidato cha sita), yuko nyumbani kama kutatokea nafasi za polisi asiniache.
"Baada ya kuongea, Anko wangu akanielekeza kwa Said Mwema nikaenda mpaka kwa mama yake akaanza kuniuliza maswali na baadae akaandika kikaratasi kwenda kwa RPC Ngoboko (Lucas Ngoboko) kwa sasa ni marehemu, akamwambia kesho nije na vyeti vyangu tayari kwa kuingia depo, nikiwa navuta unga (heroine) na sio bangi tena ilikuwa 2007.
"Nilipoingia Depo CCP (Chuo cha Polisi Moshi) 2007 naendelea kuvuta, lakini nikaanza kuwa taiti na mazoezi, lakini Ijumaa, Jumamosi na Jumapili nilikuwa lazima nivute unga wangu, niko free na kulikuwa na viongozi wangu ambao tuliingia wote uaskari walikuwa wanavuta bangi sana,
"Hivyo nikawa ninatoroka naenda kuwaletea bangi za Arusha wakiwa na imani za Moshi na Arusha ni kali sana, kwani wao walikuwa ni watu wa Mbeya ambazo walikuwa wanavuta wao na mimi sivuti bangi, navuta unga walikuwa wananiwekea chakula, nakuja nimechelewa na mimi nawaletea bangi nyingi.
Uaskari Tabora
"Basi nilimaliza Depo yangu nikapangiwa kazi Tabora ambapo wakati naingia Tabora unga (herone) ni wa shida sana, hivyo nilibeba mwingi sana ili unisogeze mwezi mzima, lakini nilishindwa niliumalizia Igunga wote kabla sijafika huko na nilipofika Tabora nilikaa mwezi mzima bila kuvuta ikabidi niwe mpole, niko taiti na kazi na majukumu yangu ya uaskari.
"Kuna siku moja, ilikuwa siku ya sikukuu nikiwa kwenye majukumu yangu ya kiuaskari kituoni alikamatwa kijana mmoja akaletwa, alikamatwa na mirungi na alikuwa ni rafiki yangu maana alikuwa ananiuzia bangi alipofikishwa hapo akaachwa hapo, waliomleta wakaondoka mimi nikachukua hiyo mirungi nikaiweka mfukoni nikamuuliza shida ni nini akanieleza.
"Tukiwa kwenye kupiga stori za hapa na pale nikajaribu kumuuliza wapi wanauza unga akanipeleka moja kwa moja wanapouza unga, wakaniuzia japo hawakuniamini kwa haraka walijiuliza na kunishangaa kwamba na huyu askari ananunua au anatuchora, lakini kutokana na nilivyojieleza ikabidi waniuzie tu, na mimi nikatoa vidhibiti vyake polisi nikavipoteza na yeye akaondoka zake huyo kijana.
Uvutaji uliopitiza
"Kwa kuwa nilikuwa sijavuta muda mrefu, nilivuta nyingi nilitapika sana siku hiyo maana nilikaa siku nyingi bila kuvuta, hivyo tangu wakati huo 2008 nikaendelea kuvuta unga na mambo yakazidi kuwa mabaya, kwani nimeshafahamu sehemu ya kupata huduma,na pesa zipo maana napokea elfu 50 katikati ya mwezi na mwisho wa mwezi napokea kama laki tatu na nusu hivi.
"Lakini kwa miaka hiyo kulikuwa na changamoto, kwani Mkoa wa Tabora ulikuwa bado haujakuwa, hivyo kupelekea unga kuwa haupatikani kwa uharaka na biashara hizo zilikuwa shida mnaweza kukaa siku tatu nne bila kupata unga,"anafafanua Bw. Amani ambaye ni Askari polisi aliyehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka miwili na kufukuzwa kazi.
Akutana na Mtumishi wa Posta
Bw.Amani anaendelea kufafanua kuwa, wakati huo, "Kuna jamaa yangu nilimkuta huko Tabora anaitwa Kamanda alikuwa anafanya kazi Posta na yeye alikuwa anavuta bangi akiwa Dar es Salaam, hivyo tulijuana na kuwa kama kitu kimoja tukawa tunajichanga hela na kumpa 'Mzungu' anaagiza Dar, lakini mambo yanakuwa yale yale inatumwa kwenye treni ila inakaa siku tatu mpaka ufike Tabora, hivyo tukawa tunateseka sana.
Twaha Amani afukuzwa kazi
"Mambo yaliendelea ikafika mwaka 2009 nikafukuzwa na kazi nikavuliwa upolisi na kupelekwa jela, lakini."
ITAENDELEA