Polisi aliyefutwa kazi, kunusurika kifo kwa utumiaji dawa za kulevya alivyogeuka kuwa nuru kwa Waraibu Tanzania-2

NA GODFREY NNKO

KATIKA chapisho lililopita la Aprili 19, 2022 tuliona namna ambavyo,Bw.Twaha Amani baada ya kuanza kazi ya uaskari mkoani Tabora mwaka 2008 alivyoendelea kujihusisha na uvutaji wa dawa za kulevya aina ya heroine kwa kiwango kikubwa.
"Kuna jamaa yangu nilimkuta huko Tabora anaitwa Kamanda alikuwa anafanya kazi Posta na yeye alikuwa anavuta bangi akiwa Dar es Salaam, hivyo tulijuana na kuwa kama kitu kimoja tukawa tunajichanga hela na kumpa 'Mzungu' anaagiza Dar, lakini mambo yanakuwa yale yale inatumwa kwenye treni ila inakaa siku tatu mpaka ufike Tabora, hivyo tukawa tunateseka sana.Soma chapisho lililopita hapa>>>

Twaha Amani afukuzwa kazi

"Mambo yaliendelea ikafika mwaka 2009 nikafukuzwa na kazi nikavuliwa upolisi na kupelekwa jela, lakini...Endelea sehemu ya pili... 

"Mama yangu alikuja kunitoa (Gereza Kuu la Uyui mkoani Tabora), nikawa mtaani kwetu Moshi watu hawakujua kama nimefukuzwa uaskari, nikawa naenda kwenye magenge wanakouza gongo nachukua pesa wakijua mimi ni askari.

"Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda watu wakaanza kujua kwamba nilifukuzwa kazi, nilikaa mtaani baadae nikaanza kujidunda sindano kutokana na stress (msongo) za kufukuzwa kazi huku nikiiba vitu mtaani na kukitokea kazi za kupandisha Wazungu Mlima Kilimanjaro, tunafanya huku nikichoma sindano.

"Lakini mama yangu alikuwa anafanya kazi Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, alikuwa anafahamiana na Afisa Elimu wa Mkoa, ikabidi amwambie ana kijana wake amefukuzwa kazi, anaomba amsaidie ndipo alimwambia niandike barua nikampa baba ikapelekwa na kuipiga mhuri na kutumwa Dodoma.

Aanza Chuo cha Ualimu

"Nikiwa nimetoka mlimani kupandisha Wazungu, nilikutana na majibu ya barua kwamba nimechaguliwa kujiunga na Chuo cha Ualimu Marangu nikaanza masomo mwaka 2009 mwishoni ila masomo rasmi ilikuwa 2010 nikiwa hapo chuo nilizoea mazingira nikaanza kujua wapi ninaweza kupenya kwenda kuvuta, japo mazingira ya baridi ni rahisi kuacha matumizi ya dawa za kulevya tofauti na mazingira ya joto.

"Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda baada ya wiki mbili nikaanza safari zangu za kwenda Moshi kutafuta unga (heroine) ili niweze kupata unga ila nikawa sichomi kutokana mazingira ambayo sio rafiki kwa kuchoma kama mtaani,"amefafanua kwa kina Bw.Amani ambaye ni alikuwa askari kwa miaka miwili na baadaye kuvuliwa uaskari na kufukuzwa kazi kutokana na utumiaji mkubwa wa dawa za kulevya.

Uvutaji na Wizi Chuoni

Katika mahojiano na DIRAMAKINI, Bw. Amani anasema, akiwa Chuo cha Ualimu Marangu mkoani Kilimanjaro alianza kuvuta kwa kasi heroine na kuiba usiku, "ninapita mabwenini ninaiba kila kitu iwe vitenge,pasi,vifaa vya umeme,mashuka, kanga,simu na asubuhi napanda gari Marangu Mtoni naenda Moshi kuuza na kununulia unga kisha ninavuta.

"Kuna kipindi mambo yalikuwa mabaya,mwaka wa kwanza walikuja kuanza chuo nikamuona kijana mmoja nikamwambia anikopeshe elfu kumi, akanipa nikamwambia nitamrudishia baada ya siku tatu, lakini nilijua sitamrudishia, kwa hiyo aliona siku zinaendelea kuisha bila kumrudishia kumbe pale chuo alikuwa na ndugu zake ambao walikuwa mwaka wa pili, ndipo walikuja kama watatu kundi wakaja bweni kwangu kama saa moja.

Asimamishwa Chuo

"Tulianza kuzozana na kuanza kuleta fujo tuligombana sana, nikawa nawachoma na kalamu, ninawapiga na ndoo,na ngumi japo nao walinivunja mguu,hiyo fujo ililazimika wakufunzi kupigiwa simu na kufika chuoni hapo,mimi nilivunjika mguu nilipelekwa Hospitali ya Marangu kupatiwa matibabu na nilipotoka baada ya siku mbili wakatusimamisha chuo.

"Wakati tunasimamishwa ilikuwa kipindi cha kusahihisha mitihani ya darasa la saba ambapo waliokuwa wanasahihisha walikuwa wanalipwa elfu saba kwa siku na kwa wiki elfu 50, basi nikarudi mtaani, lakini ile barua ya kufukuzwa sikumpelekea mama nilikaa stendi Moshi Mjini nikawa ninabeba mizigo mpaka wiki moja nikampa mtu barua ampelekee mama yangu.

"Sasa wale wanafunzi ambao walikuwa wanasahihisha mitihani kila wikiendi walikuwa wanakuja mjini nakutana nao stendi, ninawapiga saundi wananipa pesa, wengine wananipa elfu tano, mwingine elfu kumi kwa hiyo unakuta napata laki moja kwa siku hiyo. Mimi ninaelekea kijiweni kununua unga na kuvuta hadi fedha zinaisha,"anafafanua Bw.Amani.

Arudishwa Chuo

Bw. Amani anasema, mwaka 2011 walirudishwa chuo wakiwa na wazazi wao na masomo yakaanza rasmi na kipindi cha mtihani kikaanza ikabidi aache kuvuta ili aweze kujikita katika masomo.

"Na sikuwa na notisi wala madaftari na kila niliyekuwa ninamuomba ananikatalia, walinijua mimi mtukutu ila nilikomaa hivyo hivyo mpaka nikamaliza mtihani na tukarejea nyumbani kusubiri matokeo ya diploma ya ualimu wa sekondari.

Afaulu Vizuri

"Ila nikiwa nyumbani nasubiria matokeo yalitoka vizuri, nikiwa nimefaulu vizuri kuliko ambao sio watukutu mpaka mkuu wa chuo alimpigia mama yangu simu akinipongeza na akanitaka niende chuo ikionekana kuna zawadi anataka kunipa,basi nilikuwa mchafu siogi ila ikabidi niazime nguo safi niende chuoni na nikakutana na wakufunzi wote na mkuu wa chuo akanipa zawadi.
 
"Nilipewa shilingi elfu hamsini mbele ya wakufunzi wote wa chuo na wanafunzi wakawa wanauliza mbona nimekonda? Basi nikarudi nyumbani, kwa ajili ya kusubiri kupangwa,"anasema Bw.Amani.

Kijana huyo ambaye alikuwa askari wa Jeshi la Polisi na kufukuzwa mwaka 2009 kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya, anasema mwaka 2012 nafasi zilitoka na yeye kupangiwa kwenda kufundisha Shule ya Sekondari Kasororo huko Misungwi vijijini mkoani Mwanza.

Aanza Ualimu

"Ni huko kijijini sana, ila mama yangu alishajua ninaenda Mwanza akawa amenitengenezea mazingira mazuri akaniandalia pesa nzuri akanikabidhi, mimi nikaenda kununua unga mwingi ili niende nao Mwanza.

"Nilipofika mwanza Misungwi nikapanga gesti siku ya Jumamosi nikawa ninakula kwa mama ntilie nikaona magari ya kwenda Mwanza, nikauliza ni shilingi ngapi kufika Mwanza nikaambiwa ni elfu moja, ndipo nikaanza kuingiwa na tamaa nivute yote ili niende kununua.
 
"Nilijikuta navuta yote kesho asubuhi Jumapili nimeamka sina unga, ikabidi nipande gari chapu niende huko Mwanza mpaka stendi nikakutana mateja pale nikawauliza wakaniambia niwanunulie kwanza.

"Ndipo wanipeleke, ndipo nikamchukua mmoja akanipeleka wanapouza nikanunua yangu kama ya elfu 60 nikarudi Misungwi na yeye nikamnunulia vipakiti viwili basi. 
 
"Nilikaa nao mpaka Jumatatu na tulipaswa kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuripoti kwa ajili ya kupangiwa shule, nikipofika pale Mkurugenzi akatoka anaulizia Twaha Amani ni nani, nikasema ni mimi hapa, akasema bora kwa sababu mkuu wako wa Shule ya Sekondari Kasororo utaondoka nae maana ni mbali sana, nikasema sawa mkuu.

"Basi nikiwa namsubiri mkuu wa shule nikapanda tena gari kurudi Mwanza kununua unga (heroine) nilipofika nikavuta kama vipakiti viwili na vingine kumi nikafungiwa ili nimuwahi mkuu wa shule, ninafika nakuta na yeye ameenda mjini kununua mahitaji yake, ikabidi na mimi nimsubiri alipokuja alitambulishwa na masomo ninayofundisha ndipo tukaanza safari ni mbali sana, tulifika mahali panaitwa Misasi tukateremka kwenye Hiaice tukapanda pikipiki nauli ni shilingi 8,000 na baiskeli ni elfu tano, tukafika kijijini mwalimu akanipa nyumba.

"Baada ya muda tulipewa fedha za kujikimu ambazo tunapokea dirishani,halafu hizo pesa unaenda kufungua akaunti ya NMB, lakini mimi nikaenda zangu Mwanza kuvuta dawa, niliambulia kununua kigodoro kidogo nikajifanya kusingizia kulikuwa na watu wengi, foleni basi nikaweka kigodoro kidogo chini nikaanza maisha upya na kufundisha.

"Basi nikiwa kijijini nilimaliza pesa zote, sikufungua cha akaunti na nikawa nimeishiwa pesa nikaanza kukopa kwa watu wakinipa naenda kuvuta unga Mwanza, hatimaye nikaanza kuishi huko Mwanza nikaacha kufundisha, nikaanza kuiba na kuvuta mpaka niliweka vyeti vyangu bondi kwa shilingi 30,000,"anafafanua Bw.Amani.
 
ITAENDELEA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news