Rais Dkt.Mwinyi asisitiza namna bora ya kuwafundisha vijana Quran Tukufu

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema jitihada za kufundisha vijana Quran Tukufu zinapaswa kulenga katika mafundisho ya tafsiri ya aya zinazofundishwa.
MSHINDI WA KWANZA WA MASHINDANO YA QURAN AFRIKA NI VIANNE HUNNA KUTOKA KONGO BRAZAVILLE ALIYEPATA ZAWADI YA SHILINGI MILIONI 20.
 
Alhaj Mwinyi amesema hayo akiwa mgeni rasmi katika mashindano ya Kuhifadhi Quran tukufu yaliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo makubwa zaidi ya Quran tukufu Afrika, yaliowashirikisha vijana 22 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, yameandaliwa na Jumuiya ya Al-Hikma Foundation.

Akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema ufahamu wa aya zinazosomwa ni jambo la msingi katika utekelezaji wa maamrisho ya Mwenyezi Mungu sambamba na waumini kujiepusha na makatazo yake.

Amesema, kufanyika kwa mashindano hayo ya kuhifadhi Quraan na kuzishirikisha nchi mbalimbali za Afrika kumeleta mwamko mkubwa kwa waislamu katika kukisoma kitabu cha Mwenyezi Mungu, jambo ambalo linaleta faraja.

Amesema, kufanyika kwa mashindano hayo makubwa katika Afrika hapa nchini, yanalipa heshima kubwa Taifa na kuitangaza vyema Tanzania kwani yanaonekana duniani kote kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.

Amesema, Watanzania wote wana wajibu wa kuipongeza Jumuiya ya Al-hikma na kuiunga mkono kwa kuandaa mashindnao hayo ili yaendelee yadumu na kuendelea kufanyika kila mwaka ili malengo ya kuundwa kwa Jumuiya hiyo yaweze kufikiwa.

Aidha, aliwataka waislamu wajitahidi kukithiririsha kuisoma Quraan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani pamoja na kuweka mazingatio katika mafundisho yake kwa kuwa kuna fadhila nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza washiriki, walimu na wazazi kwa mjuhudi kubwa waliyofanya hadi kuwafikisha vijana hao mahala walipofikia katika ngazi ya Kimataifa.

Aliwashukuru na kuwapongeza watu mbalimbali pamoja na taasisi zilizoshiriki kuchangia na kufanikisha mashindano hayo, ikiwemo PBZ, huku akitoa wito kwa taasisi mbali mbali kuiga mfano wa PBZ na kujitolea kuchangia katika masuala ya heri.

Sambamba na hayo, Alhaj Mwinyi alipongeza kwa dhati Jumuiya ya Al-Hikma Foundation kwa kuandaa mashindano hayo na kumualika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Hassan, na akatumia fursa hiyo kuwambusha watu waliojaaliwa kuwa na uwezo kutoa sadaka zao kwa watu wenye mahitaji.

Nae, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Jumuiya ya Al-hikma Foundation Sheikh Nurdin Kishk aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali kwa kuunga mkono kufanyika mshindano hayo kila mwaka, huku akilishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), TFF, Wizara ya michezo pamoja na Klabu ya Simba kwa kutoa ridhaa ya kutumika uwanja huo uliopangwa kufanyika mashindano makubwa ya Afrika.

Aidha, aliwashukuru wadhamini wote waliochangia kufanikisha mashindano hayo, ikiwemo mdhamini mkuu Benki ya Wananchi wa Zanzibar (PBZ) na kusema Benki hiyo ni salama, sambamba na kuwashukuru wadhamini wengine ikiwemo Dar Fresh, GGB na wengineo.

Mkurugenzi Mkuu wa PBZ (Mdhamini mkuu wa mashindano hayo), alisema Benki hiyo haiko kwa ajili ya Zanzibar pekee, bali iko nchini nzima na tayari imesambaza huduma zake kwa kuweka matawi katika maeneo mbali mbali ya Mikoa ya Tanzania Bara, huku akibainisha lengo la Benki hiyo kuifanya kuwa miongoni mwa benki kubwa hapa nchini.

Katika hatua nyingine, kwa nyakati tofauti Mufti wakuu wa nchi za Uganda, Burundi, Rwanda na Zanzibar, wakitoa salamu zao kwa washirki wa mashindano hayo waliishukuru Jumuiya ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindnao hayo kwa vijana, ikiwa ni hatua muhimu katika kuitangaza Quraan, hususan katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mufti hao waliwatakia kheri wananchi wa Tanzania na kusema kufanyika wka mashindano hayo hapa nchini ni hatua inayongeza kheri na kuleta ushirikiano miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Hakuna jambo zuri analolipenda Mwenyezi Mungu kama kukitumia kitabu chake kwa kuisoma na kuihifadhi quraan, natumia fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Al-hikma kwa kuwaendeleza vijana kupitia mashindano haya,” alisema Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Swaleh Omar Kaab.

Vile vile, Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Dk. Abubakar Zubeir alisema mashindnao hayo ni fursa adhimu ya kuangalia vipaji kwa vijana wa Afrika, hali inayotoa ishara ya kufanyika mambo makubwa siku zijazo.

Mapema, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa aliwapongeza washirikia wa mashindano hayo kutoka nchi mbali mbali Barani Afrika na kuwahakikishia kuwa Tanzania ni mahala salama, huku akiwatakia kheri waislamu ya mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhan pamoja na sikukuu njema ya Pasaka kwa Wakristo kote nchini. 

Hii ni mara ya 22 kufanyika Mashindano haya makubwa zaidi ya Quraani tukufu Afrika, ambapo mwaka yamezishikisha nchi 22.
Kufuatia mashindano hayo yaliohudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Mabalozi, Masheikh na watu wengine mashuhuri, Alhaj Dk. Mwinyi alimtunuku zawadi ya mfano wa Hundi ya shilingi Milioni 20 mshiriki kutoka Congo Brazaville baada ya kuibuka mshindi wa kwanza , huku washiriki watano walioshika alama za juu zaidi walitunukiwa zawadi mbali mbali, sanjari na mshiriki aliebainika kuwa na sauti nzuri zaidi pamoja na yule mwenye umri mdogo zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news