Rais Samia atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa kuhusu Mfumo wa M-MAMA

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Wakuu wa Mikoa katika Halmashauri ambazo mfumo wa M-MAMA utatekelezwa, kutenga fedha zitakazoongeza nguvu kwenye huduma ya mama na mtoto mchanga.
Rais Samia amesema hayo leo wakati akizindua mfumo wa usafirishaji wa dharura wa wajawazito na watoto wachanga (M-MAMA) iliyoratibiwa na kampuni ya simu ya Vodacom katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Rais Samia amesema, lengo la mfumo huo ni kuhakikisha kuwa wakina mama zaidi ya milioni moja ambao ni walengwa wanafikiwa na kunufaika na huduma hii katika kipindi cha miaka mitano.

Aidha, Rais Samia amesema tangu kuanza kwa majaribio ya mfumo wa M-MAMA katika Wilaya ya Sengerema na mkoani Shinyanga mwaka 2013, wanawake na watoto 12,000 wameshahudumiwa na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya kina mama vinavyotokana na ukosefu wa usafiri.

Vile vile Rais Samia ameitaka Kampuni ya Vodacom kuufanya mfumo huo uwe endelevu na uwafikie wananchi wengi na kutoa wito kwa kampuni zingine zilizopo nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali.

Rais Samia amesema, pamoja na jitihada zilizofanywa na Serikali, bado zipo changamoto ambazo husababisha vifo vya mama na mtoto kabla au baada ya kujifungua kutokana na kukosekana kwa mawasiliano ya haraka na usafiri wa uhakika wa kumwahisha mama mjamzito kufika katika kituo cha afya.

Kwa upande mwingine, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa M-MAMA ili zikusanywe, kuchakatwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zinazokubalika Kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news