*Tuzo hizi zimefanyika baada ya ukimya wa miaka saba
NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa Watanzania waliopewa Tuzo ya Heshima kupitia Tuzo za Muziki Tanzania 2021.
Mheshimiwa Rais Samia amepewa heshima hiyo kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika sanaa na burudani ambapo ametenga zaidi ya shilingi Bilioni 1.5 kufanikisha heshima hiyo ambayo ilikosekana kwa miaka zaidi ya saba iliyopita.
Tuzo hizo zilizoratibiwa na Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zimetolewa usiku wa kuamkia leo Aprili 3, 2022 katika Ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
BASATA ni taasisi ya umma iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 23 ya Mwaka 1984 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 5 ya Mwaka 2019.
Historia inaonesha kuwa, sheria ya kuunda upya baraza hilo ilifanywa kwa kuunganishwa Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa ya Mwaka 1974 na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA) ya Mwaka 1974. Baraza liliundwa ili lisimamie maendeleo ya sanaa nchini
Aidha, tuzo hiyo ya heshima imeenda kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo,aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, marehemu Ruge Mutahaba, Fatima binti Baraka maarufu kama Bibi Kidude,staa wa muziki ndani na nje ya Tanzania ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa WCB,Nasibu Abdul Juma Issack (Diamond Platnumz).
Tuzo nyingine
Malikia aliyetwaa tuzo katika video ya mwaka 2021 ni Feven Reuben (Fevushka), Mfalme aliyetwaa tuzo katika video ya mwaka 2021 ni Selemani Masenga.
Mnenguaji bora wa kike mwaka 2021 ni Baby Drama huku kwa upande wa mnenguaji bora wa kiume akitoka Kukaye Moto Culture Centre.
Pia mwimbaji bora wa kike nyimbo za asili mwaka 2021 ni Shoninda Kilasi, mwanamuziki bora wa kiume wa muziki wa asili 2021 ni Msafiri Zaosa na wimbo bora wa asili 2021 ni Asili Yetu ya Sholo Mwamba.
Msanii bora wa kike kwa upande wa muziki wa mwambao (Taarab) 2021 ni Khadija Yusuf huku nafasi ya msanii bora wa kiume katika muziki huo akiwa ni Mzee Yusuf ambapo wimbo bora wa Taarab 2021 ni Usinifokee Jahazi Modern Taarab.
Kwa upande wa mwanamuziki bora wa Reggae/dancehall 2021 ni Badest 47 huku wimbo bora wa Reggae/Dancehall ukiwa ni Unaota wa Badest 47.
Aidha, tuzo ya mtumbuizaji bora wa kike wa mwaka 2021 ameshinda Saraphina Michael ambapo tuzo hiyo ilikuwa na washindani kama Shilole, Nandy na Maua Sama.
Nafasi ya tuzo ya mtumbuizaji bora wa kiume 2021 kwenye tuzo hizo imechukuliwa na staa wa muziki ndani na nje ya Tanzania,Rajab Abdul Kahali (Harmonize) ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Konde Music Worldwide baada ya kuwaangusha Sholo Mwamba, Alikiba,Whozu na Dulla Makabila.
Wakati huo huo, msanii bora wa kiume wa singeli wa mwaka 2021 ni Sholo Mwamba, wimbo bora wa mwaka wa singeli ni Alowee na Sholo Mwamba, hivyo ukijumlisha na tuzo ile ya wimbo wa asili wa mwaka huu ambao ulikuwa ni Asili Yetu atakuwa kazoa tuzo tatu.
Mshindi wa Tuzo ya wimbo bora wa kushirikiana 2021 ni Loyalty ya Darassa akiwashirikisha Marioo na Nandy ambapo wameiangusha Ndombolo ya Alikiba, Abdukiba, K2ga na Tommy Flavour, Shikilia ya Profesa J, Unaua vibe ya Rapcha na Lala ya Jux.
Naye mwimbaji Nandy ameshinda Tuzo ya Chaguo la Watu kwenye Majukwaa ya kidigitali mtandaoni kama mwimbaji bora wa kike 2021.Mtunzi bora wa mashairi wa mwaka 2021 ameshinda Profesa Jay kupitia Utaniambia Nini baada ya kuwaangusha Alikiba akiwa na Utu, Mi amor ya Marioo, Lisa ya Rapcha na Loyalty ya Darassa.
Wakati huo huo, tuzo ya mtunzi bora wa melody wa mwaka 2021 imeenda kwa Alikiba huku albamu bora ya mwaka 2021 ikiwa ni Only One King ya Alikiba.
Tuzo ya mwanamuziki bora wa kiume chaguo la watu kwenye majukwaa ya kidigitali ni Alikiba huku akichukua tena tuzo ya mwanamuziki bora Afrika Mashariki wa mwaka 2021
Kwa upande wa tuzo ya mtayarishaji bora wa muziki wa Hiphop 2021 imeenda kwa Zombie, huku Mr.T Touch akishinda tuzo ya mtayarishaji bora wa Bongofleva kwa mwaka 2021.
Wakati huo huo, mwimbaji wa Bongo fleva Saraphina Michael ametwaa tuzo nyingine ya msanii bora chipukizi upande wa kike kwa mwaka 2021. Huku Rapcha akitwaa Tuzo ya Msanii bora chipukizi wa kiume kwa mwaka 2021.
Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa kiume wa Bongofleva mwaka 2021 imeenda kwa Marioo, huku Young Lunya akishinda tuzo mbili ikiwemo ya msanii bora wa Hiphop na wimbo bora wa Hiphop wa Mbuzi. Naye Chemical ameshinda Tuzo ya Msanii bora wa kike wa Hiphop 2021.
Mhariri DIRAMAKINI ataendelea kuongezea maudhui na kuboresha zaidi habari hii, endelea kufuatilia