Rais Samia: Haikuwa kazi rahisi, asanteni Watanzania

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais ameishukuru timu ya waandaji wa filamu ya Tanzania The Royal Tour kwa kuikamilisha kwa ufanisi huku akisisitiza kwamba,haikuwa kazi rahisi kukamilisha filamu hiyo ambayo imerekodiwa ndani ya siku nane.

Pia amewashukuru Watanzania waliotoa michango yao kwa moyo ili kuhakikisha utengezaji wa filamu hiyo unafanikiwa.
Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 28,2022 katika Ukumbi wa Simba uliopo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha ambapo ameshiriki kuizindua filamu hiyo kwa mara ya kwanza hapa nchini.

Uzinduzi wa awali ulifanyika Aprili 18, 2022 jijini New York, na Aprili 21, 2022 katika jiji la Los Angeles nchini Marekani ambapo kote huko Mheshimiwa Rais alishiriki filamu hiyo ambayo yeye ndiye muongozaji mkuu.

"Nalishukuru sana kundi la production, haikuwa kazi rahisi, waliniambia weka urais wako ofisini, ukija huku ni tour guide...wewe ni actress. Urais sisi hatuna habari nao, action moja naifanya mara kumi na mara nyingine nakasirika wanasema..no, no...Samia you have to do it, nikimaliza anasema unatakiwa kurudia.

"Kwa Tanzania tumeanzia uzinduzi Arusha kwa sababu ndani ya Arusha ndiko utalii ulikojikita baada ya hapa tutaenda Zanzibar na Dar es salaam,"ameeleza Mheshimiwa Rais Samia.

Awali Mheshimiwa Rais Samia akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Marekani amesema akiwa nchini Marekani amefanya mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na wameahidi kuipa Tanzania fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

"Tumefanya mazungumzo na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) nao pia mambo mazuri tumekubaliana vizuri na kuna fedha kama ile tuliyoleta tukaipeleka kujenga vituo vya afya, madarasa na mengine, tunatarajia nyingine inakuja ya aina ile ili iende kwenye maendeleo,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, filamu ya Royal Tour imefanywa kwa kutumia michango ya watanzania na hakuna fedha ya Serikali iliyotumika kwa ajili ya maandalizi hadi uzinduzi.

“Pesa yote mpaka tumekwenda Marekani na kurudi ni pesa iliyochangwa na Watanzania. Kwa hiyo kama tunazungumza the real star katika hii filamu ni Watanzania wote,”amesema.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amesema wakati wa uandaaji wa filamu hiyo wapo watu mitandaoni walisema amejigeuza Rambo au Arnold Schwarzenegger badala ya kufanya kazi, lakini amesema faida ya filamu hiyo ni kubwa zaidi ya wanachofikiria.

"Wakati nafanya hili jambo kuna wadogo zangu, wanangu kwenye mitandao wakawa wanasema, huyu Mama badala ya kufanya kazi amejigeuza Rambo au Schwarzenegger anafanya mafilamu huko anaigiza, lakini nikasema ngoja tuone kitakachotoka.
"Tumeanza kuizindua Marekani, tulipoanza New York ile siku salamu za watu laki tatu na zaidi wakawa wanapongeza, Los Angeles nako tukapata mrejesho mzuri sana, kufanya jambo kama hili kunahitaji kujitoa, nimetumia siku nane nje ya ofisi na siku nane kukaa nje ya Ofisi ya Rais ni muda mrefu sana,"amefafanua Mheshimiwa Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news