NA FRESHA KINASA
SERIKALI mkoani Mara imewataka wananchi wa mkoa huo kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira sambamba na upandaji wa miti katika maeneo yao.

Zoezi hilo la upandaji wa miti, limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma, walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kiara.
Mheshimiwa Hapi amesema, wananchi wanawajibu wa kuunga mkono juhudi za serikali ambazo zimekuwa zikifanywa katika utunzaji wa mazingira. Hivyo amewahimiza kupanda miti kwa wingi hatua ambayo itasaidia kulinda uoto wa asili na kuvinufaisha vizazi vijavyo.
“Miti hii ambayo kivuli chake tunakipata leo, ilipandwa na wazee wetu hapo zamani na sasa ni wajibu wetu kupanda miti na kutunza mazingira,”amesema Mheshimiwa Hapi.

Meya wa Manispaa ya Musoma, Mheshimiwa William Gumbo amesema kwamba, Shule ya Sekondari Kiara imechaguliwa kuzindua zoezi la upandaji miti kutokana na sababu za kihistoria na kwamba ni miongoni mwa shule za kata ambazo zilianza kujengwa na wananachi wa Manispaa ya Musoma kwa mwitikio mkubwa na nguvu zao kwa muda mfupi.
Gumbo amesema, zoezi la upandaji wa miti linaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na uzoefu wa wananchi hao na mwitikio walio uonesha katika ujenzi wa shule hiyo.
Pia, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuungana na wananchi wa Manispaa ya Musoma kupanda miti kama sehemu ya uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti 30,000 katika Manispaa ya Musoma.
Mheshimiwa Gumbo ameeleza kuwa, zoezi la kupanda miti katika Manispaa ya Musoma ni endelevu na kuwataka wanafunzi na wananchi kuchukua miche ya miti katika kitalu cha Wakala wa Misitu (TFS) Manispaa ya Musoma na kupanda katika maeneo yao.

Agatha Jocktan ni Mkazi wa Kiara ambapo amesema, katika kuendeleza utunzaji wa mazingira wananchi wana jumu la kuondokana na shughuli za kibinadamu zisizo rafiki kwa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo na kulima katika vyanzo vya maji.
"Pamoja juhudi za upandaji miti zinazofanywa, lakini lazima miti hiyo isimamiwe vyema na kutunzwa ili kupata faida zaidi kwa baadaye, tunashuhudia mabadiliko ya tabia nchi yakizikumbwa nchi nyingi hatua mojawapo ya kukabiliana na hali hiyo ni kupanda miti kwa wingi na kutunza mazingira yetu na vyanzo vya maji,"amesema Agatha.