NA ROTARY HAULE
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge amefungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Madiwani Wanawake waliopo ndani ya mkoa wake na kuwataka watambue wajibu wao hasa katika kutatua kero za wananchi waliowachagua.
Mafunzo hayo yalianza kufanyika Aprili 4 na kumalizika Aprili 5,2022 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha yakiandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu kwa ufadhili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ( LHRC).
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo,RC Kunenge amesema kuwa, kitendo kilichofanywa na Mbunge huyo ni mfano wa kuigwa na kwamba amemshukuru kwa kutambua umuhimu wa madiwani hao kupewa mafunzo hayo.
Amesema kuwa, madiwani wanapaswa kutambua wajibu wao kutokana na majukumu yaliyopo katika nafasi zao ikiwemo kuzifanyiakazi kero zinazowakabili wananchi wa maeneo husika ili kusudi kufikia malengo ya kimaendeleo.
"Madiwani tambueni wajibu wenu wa kutumikia wananchi kwani mmetokana na imani ya watu na hivyo ni lazima mfanyekazi zao,kama ukishindwa kuwajibika ni wazi kuwa utakuwa umeiangusha Serikali,"amesema.
Aidha, Kunenge amesema, kama ukiona kuna mambo ya msingi ambayo wananchi wanataka yatekelezwe na diwani halafu akashindwa ni wazi kuwa hakuna jambo la kukumbukwa katika uongozi wake .
Kunenge amewataka wafanye mambo yaliyo sahihi na kwa weledi mkubwa huku akiamini wanawake wakiamua mambo yatakwenda vizuri na matokeo chanya watapata.
"Wajibu wa kila mmoja kuwa diwani bora ni yeye mwenyewe na kama kuna changamoto zipo kwa wananchi na wewe ukazifanyiakazi huna sababu kuhangaika na uchaguzi ujao kwani itapita kirahisi kulingana na kazi zako," ameongeza Kunenge.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani,Hawa Mchafu amesema kuwa, Mkoa wa Pwani bado una changamoto ya ndoa za utotoni,mimba za utotoni,unyanyasaji wa kijinsia na utoro shuleni.
Mchafu amesema,kufuatia changamoto hizo alilazimika kuandika andiko na kulipeleka katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kusaidia kutoa mafunzo kwa Madiwani Wanawake.
Amesema kuwa, baada ya kukubaliwa andiko hilo ikabidi aanze mara moja kutoa mafunzo kwa madiwani wote wanawake wa Mkoa wa Pwani katika Kituo cha Kibaha Mjini ambapo mafunzo yamedumu kwa muda wa siku mbili ikiwemo kuanzia Aprili 4 na April 5.
Mchafu pia amempongeza, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameujali Mkoa wa Pwani kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
Amesema,pamoja ujenzi wa madarasa hayo lakini bado Mkoa wa Pwani upo katika mpango wa mikoa tisa ya kupata shule ya bweni jambo ambalo wanapaswa kujivunia kwa kupata Rais mpenda maendeleo.
"Lengo la mafunzo haya ni kuendana na kile anachofanya Rais Samia pamoja na Mkuu wetu wa Mkoa wa Pwani ,kwahiyo tutaendelee kutoa mafunzo haya ili kuunga juhudi za Rais pamoja na Serikali ya awamu ya Sita kwa ujumla,"amesema Mchafu.
Mchafu ameongeza kuwa, Mkoa wa Pwani una jumla ya Madiwani Wanawake 56 na katika mafunzo hayo wameshiriki Madiwani 54 ambapo amekishukuru LHRC kwa ufadhili huo humu akiomba mafunzo mengine yalenge katika masuala ya bima.
Kwa upande wake Afisa wa Kitengo cha Jinsia,Watoto na Watu wenye Ulemavu kutoka LHRC, Getrude Dyabene amesema mafunzo hayo ya siku mbili ni njia ya kujadili namna ya kuwajengea uwezo Wanawake Madiwani namna wanavyoweza kujadili masuala mbalimbali ya kijamii.
Dyabene amesema kuwa, mbali na hilo lakini pia ni sehemu ya kujadili changamoto za kiuongozi za wanawake ambapo baada ya mafunzo hayo wataandaa mpango kazi wa kila halmashauri ambapo utahusu masuala ya kijinsia.