NA FRESHA KINASA
SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, limetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa muda wa siku tatu kwa wasichana waliokimbia ukatili wa kijinsia wanaohifadhiwa katika Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu.
Shirika hilo chini ya Mkurugenzi wake, Rhobi Samwelly, linamiliki vituo viwili vinavyotoa hifadhi kwa wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni, ambapo kwa Wilaya ya Butiama ni Kituo cha Nyumba Salama (Safe House) kilichopo Kiabakari na Serengeti Kituo cha Nyumba ya Matumaini.
Mafunzo hayo yametolewa kuanzia Aprili 4- hadi Aprili 6, 2022, ambapo wameweza kufundishwa juu ya namna ya uendeshaji wa biashara ndogo ndogo, utengenezaji mafuta ya kupakaa, sabuni za miche, sabuni za maji, shampoo katika kuwawezesha kupata ujuzi thabiti wa kutengeneza bidhaa hizo.
Mkuu wa Kituo cha Nyumba ya Matumaini Mugumu (Hope House), Daniel Misoji amesema kuwa, elimu hiyo itawasaidia kwa kiwango kikubwa mabinti hao Katika utengenezaji wa bidhaa hizo wakiwa kituoni hapo, ambapo wataweza kuziuza na kujipatia kipato kwa manufaa yao na Jamii kwa ujumla.
Misoji ameongeza kuwa, Shirika hilo kupitia vituo vyake mbali na kuwaendeleza kielimu wasichana ambao hukimbia vitendo vya kikatili kutoka katika familia zao wakiwa wanasoma, pia limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Wasichana ambao hawako katika mfumo rasmi wa elimu wanafundishwa ujasiri mali, ushonaji, na kuwaendeleza ambao huwa wamehitimu kodato cha nne katika vyuo mbalimbali nchini.
"Wasichana ambao wamekuwa wakikimbia ukatili katika familia zao ni kuona wanafikia ndoto zao. Kwa wale ambao ni wanafunzi tumekuwa tukiwapokea na kuwasimamia vyema sambamba na kuwapa mahitaji yote na wanaendelea na masomo yao, watimize ndoto zao.
"Kwa wale ambao sio wanafunzi tunawafundisha ujasiriamali na stadi mbalimbali za maisha, ambao tayari wamehitimu kidato cha nne lakini hawakubahatika kuendelea mbele tunawapekeka vyuoni Mkurugenzi Rhobi Samwelly amekuwa akiyafanya haya kwa ufanisi kwani mtu akiwa na uchumi imara vitendo vya ukatili vitapungua katika jamii,"amesema Daniel.
Daniel ameiomba jamii kutokumbatia mila potofu na pia amesisitiza kila mmoja kwa nafasi yake kushiriki kikamilifu kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani vinarudisha nyuma juhudi za maendeleo, huku akisisitiza kuwafichua mbele ya sheria wale wanaobainika kufanya vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Kwa upande wake mgeni rasmi aliyehudhuria katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, Isack Mwankusye ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti amelishukuru Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kushirikiana vyema na Serikali katika Kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kutetea haki kwa manufaa ya jamii na taifa pia.
Amesema, vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vimekuwa vikikwamisha juhudi za maendeleo zikiwemo mila kandamizi ambazo huwakandamiza Watoto wa kike wasitimize ndoto zao, ameomba ziachwe na suala la elimu litiliwe mkazo hususan elimu ya vitendo ikiwemo ufundi na ujuzi kutokana na fursa katika kutatua changamoto ya ajira kupitia kujiajiri.
"Hope for Girls and Women in Tanzania mnafanya kazi nzuri sana kusaidia mapambano ya ukatili na kusukuma mbele maendeleo, wasichana hawa mngeweza kukaa nao hapa kituoni na kuwarejesha kwao bila elimu yoyote wanapoondoka hapa, mmekuwa mkiwapa ujuzi, kuwaendeleza kielimu na kusimama pamoja nao. Serikali pia inatoa mikopo ya asilimia 10 kwenye Halmashauri Kupitia Maendeleo ya Jamii hii ni fursa jamii waitumie kama ambavyo amekuwa akisisitiza Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan,"amesema.
Pia, amewataka wasichana hao kujitambua, kujithamini na kuitumia vyema elimu waliyoipata katika kujikwamua kiuchumi na amewaomba waendelee kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kutojiingiza katika vitendo vya mahusiano ya kimapenzi kwa kukurupuka kwani wasichana wengi hutelekezwa na kupata matatizo mengi.
Kwa upande wake, Rehema Gidioni aliyehitimu mafunzo hayo amelishukuru Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuendelea kuwapa hifadhi wasichana wanaokimbia ukeketaji pamoja na kuwaendeleza kielimu na kuwapa mafunzo ya ujasirianali na stadi za maisha kwa faida yao.
"Nalishukuru Shirika la Hope, kwani mbali na kutupa hifadhi wasichana tuliokimbia vitendo vya ukatili wa Kijinsia katika familia zenu bado wametupa zawadi ya mafunzo haya ambayo yatatusaidia kwa kiwango kikubwa hata baada ya kuondoka hapa tutajitegemea kiuchumi kupitia maarifa haya ya utengenezaji wa sabuni na bidhaa nyingine tulizofundishwa,"amesema Happines Elias Mhitimu wa mafunzo.
Catherida Robert, ni Mwalimu wa ujasiriamali aliyewafundisha wasichana hao, ambapo amewataka kuwa walimu kwa wengine ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo, huku akiwataka kinamama wengine kuchangamkia fursa za ujasiriamali kwani zinamanufaa makubwa kiuchumi.