NA LWAGA MWAMBANDE (KiMPAB)
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Kimataifa, Klabu ya Simba wamefanikiwa kuandika historia ya kusonga mbele katika kundi D kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Ni baada ya kushuka kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kuikabili US Gendarmarie ya Niger kwenye mchezo wa mwisho ya Kundi D uliobeba hatima ya kundi hilo.
Hii ni rekodi mpya kwa timu ya Tanzania, kwani tangu michuano hiyo ilivyoboreshwa mwaka 2004 hakuna timu iliyotinga hatua hiyo licha ya Yanga na Namungo kutinga makundi mara tatu.
Wanajangwani walitinga makundi 2016 na 2018 na kumaliza mkiani kabla ya Namungo FC kufuzu mwaka jana na kuweka aibu kwa kutoshinda mechi wala kufunga bao na kumaliza mkiani ikipoteza mechi sita.
Ili kupata uhondo kamili ungana na mshairi wa kisasa, Bw. Lwaga Mwambande (KiMPAB) uweze kupata maarifa mapya kama ilivyo hapa chini;
Ni usiku saa nne,
Huu ni mwezi wa nne,
Tumefunga goli nne,
Simba Robo Fainali.
Ndege tutazidi panda,
Jinsi tunazidi shinda,
Hata dau linapanda,
Simba Robo Fainali.
Wachezaji hongereni,
Na makocha hongereni,
Viongozi pongezini,
Simba Robo Fainali.
Katika ukanda huu,
Simba ndiyo timu kuu,
Katika mpira huu,
Hiyo Robo Fainali.
Siyo Kombe la Azam,
Hiyo pokea salam,
Huko kwa wataalam,
Simba Robo Fainali.
Lingekuwa goli moja,
Wangeinuka pamoja,
Sasa waishiwa hoja,
Simba Robo Fainali.
Wamepigwa Form Foo,
Magoli manne goo,
Na wenyeji wao loo,
Simba Robo Fainali.
Walikuwepo wachawi,
Wakidhania hayawi,
Wameshapakazwa kiwi,
Simba Robo Fainali.
Kesho itisha presi,
Wandugu wenye mikosi,
Hii foo jii kasi,
Simba Robo Fainali.
Amsha amsha yetu,
Tunalala roho kwatu,
Acha wenye roho butu,
Simba Robo Fainali.
Simba tunaisifia,
Heshima kwa Tanzania,
Hapo ilipofikia,
Hiyo zaidi ya dili.
Tembelea Tanzania,
Vile watutangazia,
Wengi wataangalia,
Huko Robo Fainali.
Watalii wakifika,
Uchumi ukajengeka,
Sote tunafaidika,
Simba Robo Fainali.
Ni Simba ya Tanzania,
Robo imeshaingia,
Heri tunaitakia,
Izidishe kwenda mbali.
Robo fainali CAF,
Simba timu maarufu,
Ni mpira maradufu,
Chaenea Kiswahili.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602