Safari ya Uchumi wa Buluu imeanza rasmi-Rais Dkt.Mwinyi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, safari ya Uchumi wa Buluu imeanza rasmi na kazi bado itaendelea.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi boti,mashine na vifaa vya uvuvi Kiongozi wa Kikundi cha Uvuvi cha Kengeja, Bw.Ali Baroo, wakati wa kukabidhi Boti Nne na Mashine za Boti 16 kwa Vikundi vya Uvuvi Pemba, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Bandari ya Shumba Mjini Wilaya ya Michewene Pemba Aprili 12,2022. (Picha na Ikulu). 

Ameyasema huko katika Bandari ya Shumba Mjini, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika hafla ya ugawaji wa boti, mashine zilizotolewa na Benki ya Amana pamoja na hundi ya shilingi milioni 192 zilizotolewa na Benki ya CRDB kwa ushirika wa Uvuvi Tumbe ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu sambamba na ahadi yake hiyo aliyoitoa.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kwamba, huu sio wakati tena wa wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi kulalamikia ukosefu wa vifaa na mitaji, kwani Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali imeshaanza kutekeleza azma ya kuimarisha uchumi wa buluu kwa kutoa vifaa mbalimbali.

Amesema, pamoja na vifaa hivyo vilivyotolewa tayari zipo benki mbalimbali na mashirika mengine kama ZAFICO wameshatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitaji ambayo itatolewa kwa wavuvi ili kufikia safari ambayo ina lengo la kuwabadilisha kimaisha.

Ametolea mfano wa benki hizo ikiwa ni pamoja Benki ya Amana iliyotenga shilingi Bilioni 10, Wizara ya Uchumi wa Buluu shilingi Bilioni 36, Benki ya CRDB iliyotenga shilingi Bilioni 31 na Kampuni ya ZAFICO iliyotenga shilingi Bilioni 7.6.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na wahisani mbalimbali yakiwemo mabenki ili kuwajengea mbinu za maendeleo wananchi ikiwemo kuwapatia nyenzo mbalimbali za kujikwamua na umasikini,”amesema.
Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, zoezi hilo la utoaji wa boti na vifaa vyake ni miongoni mwa kufikia safari ya ajira laki tatu (300,000) zilizotangazwa na Serikali ambazo miongoni mwake zitatoka katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uvuvi.

Ameeleza haja kwa benki ambazo zimeshatenga fedha kwa ajili ya kuwaezesha wananchi kufanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wengine ambao bado hawajapatiwa vifaa vya uvuvi ili kuungana na wenzao katika safari hiyo ya kutumia raslimali zitokanazo na bahari ili kufaidika na sera ya Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt.Mwinyi pia, alieleza azma ya Serikali kuirasimisha bandari hiyo ya Shumba Mjini ili iweze kufanya shughuli zake vizuri na kutoa faida zaidi kwa wananchi.

Amesema tayari imeweza kushirikiana na wahisani mbalimbali ikiwemo benki ili katika kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo vifaa vya uvuvi ili kufikia uchumi wa buluu sambamba na kutoa mitaji kwa wafanyabiashara mbalimbali.

Amewataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wananchi wanapewa fedha kutoka benki ya CRDB na Benki ya Amana kwa ajili ya shughuli zao za uvuvi kama ilivyokusudiwa na kupangwa na Serikali.

Dkt.Mwinyi ameuagiza uongozi wa Wizara ya Maji kuhakikisha Kijiji cha Shumba ya mjini kinapata huduma ya maji safi na salama haraka iwezekanavyo na kipindi atakachofika kijiji hapo hataki kusikia tena changamoto hiyo.

Aidha, alieleza kwamba hivi karibuni Wizara ya Fedha itaanza kuwalipa fidia wananchi ambao wamepisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya barabara.

Alieleza hatua na ushirikiano atakaoutoa katika kuhakikisha ZAFICO inaimarika na kuweza kuvua na kununua samaki, kusarifu kwa kujenga viwanda ikiwa ni utekelezaji wa uchumi wa buluu.

Pia, kutatolewa boti 577 za uvuvi, kujengwa kwa viwanda vya kusarifu samaki na mwani huko kisiwani Pemba.

Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu, Suleiman Masoud Makame ametoa shukurani kwa Rais Dkt.Mwinyi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.

Akitoa maelezo Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZAFIKO, Dkt.Ameir Haidar Mshenga alieleza kuwa mashine 16 za boti ni kwa ajili ya wavuvi wa Shumba Mjini na boti ni kwa ajili ya wavuvI wa Makangale na Kengeja ikiwa ni mwendelezo wa kutimiza ahadi aliyoitoa Rais hivi karibuni.

Amesema kuwa, hatua hiyo inatokana na mazungumzo waliyoyafanya kati yao na Benki ya Amana kupitia USAID ambayo hatimae yamezaa matunda, pamoja na kufanya mazungumzo na ZSSF ili kuwasajili wavuvi hao kwenye mfuko wa Hiari kwa lengo la kujiwekea hakiba ya hapo baadae.

Amesema kuwa, ZAFICO imejipanga kutoa mashine za boti kwa wavuvi 650 na kuwapatia boti na mitego wavuvi 887 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa ambapo tayari imeshaanza mazungumzo ya kuwapatia mashine 20 za boti wavuvi wa Tumbe kupitia Mpango huo kwa kuwashirikisha benki ya Amana kupitia USAID na ZSSF.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Amana, Abubakar Athman Ali alisema kuwa benki hiyo imechukuwa hatua hiyo ya kutoa vifaa hivyo ikiwa na azma ya kumuunga mkono Rais Dkt.Mwinyi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wa buluu.
Boti Nne na Mashine zake zilizokabidhiwa kwa wananchi wa Makangale boti mbili na Kengeja boti mbili,kwa ajili ya Uvuvi na Mashine za Boti 16 zilizotolewa kwa Vikundi vya Uvuvi Kisiwani Pemba,wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni Pemba.

Kwa upande wa wananchi wa Shumba ya mjini Mkoa wa Kaskazini Pemba wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa kutekeleza ahadi zake.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi pia, aligawa sadaka ya futari kwa wenye mahitaji maalum huko Micheweni pamoja na kuwagawia wananchi wenye mahitaji maalum wakiwemo yatima, wajane, walemavu huko ukumbi wa Jamhuri Wete ambapo alitoa shukurani kwa wale wote wanaoendelea kutoa sadaka zao kwa wananchi Unguja na Pemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news