Sekondari ya Wasichana ya Jokate Mwegelo yakabiliwa na uhaba wa maji

*Pia uzio wahitajika kwa ajili ya kuimarisha usalama shuleni
 
NA AHMAD NANDONDE

SHULE ya Sekondari ya Wasichana ya Jokate Mwegelo iliyopo Kata ya Kibuta Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani inakabiliwa na kikwazo cha maji, hali inayosababisha wanafunzi kutumia muda mwingi wa kujisomea wenyewe kupata huduma hiyo.
Aidha, shule hiyo pia ina uhitaji wa uzio kutokana na mazingira iliyopo ili kuweka ulinzi kwa watoto wa kike wanaosoma katika shule hiyo.

Kutokana na hali hiyo uongozi wa shule pamoja na wanafunzi wameiomba Serikali kuangalia kati na kutafuta namna ya kutatua kero hizo ili kuwalinda wanafunzi na madhara yanayoweza kujitokeza.

Wakizungumzia vikwazo vya shule hiyo, mkuu wa shule pamoja na wanafunzi wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa,shule hiyo ina mazingira rafiki ya kujisomea, lakini kutokana na suala la uzio na vyanzo vichache vya maji Serikali inatakiwa kuingilia kati kuvitatua.
Mkuu wa shule hiyo, Mariam Mpunga amesema, Sekondari ya Wasichana Jokate Mwegelo licha ya kuwa na mazingira mazuri ya kujisomea kwa wanafunzi wa kike suala la kujenga uzio na kuongeza vyanzo vya maji ni vitu vya muhimu.
Mpunga ameahidi shule hiyo kuwa na ufaulu wa juu katika mitihani yake ya kitaifa kutokana na eneo ilipojengwa na wanafunzi wake kujikita zaidi kwenye masomo wanayofundishwa.
Irene Sebastian na Husna Hamad ni wanafunzi wa shule hiyo ambao wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, pamoja na kuwa na uhitaji mkubwa wa maji, lakini suala la uzio ni la muhimu kwani shule imezungukwa na vichaka.

Akijibu changamoto zilizoainishwa afisa elimu vifaa na takwimu, Hassan Mathias amesema shule hyo ni mpya na bado kuna maeneo yanendelea kufanyiwa marekebisho na kwamba upo mradi wa DAWASA utapita katika eneo la shule hiyo na kumaliza kero iliyopo.

Kwa mujibu wa Ofisa elimu huyo Serikali inatambua vikwazo hivyo na iko kwenye mikakati ya kushughukiwa, na kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri ameahidi kupeleka matenki kwa ajili ya kuvunia maji wakati utaratibu wa maji ya DAWASA ukiendelea.
Shule ya Sekondari Jokate Mwegelo ilianzishwa mwaka 2020 kufuatia ndoto ya viongozi ya kuhakikisha wanafunzi wa kike wanaondokana na kikwazo cha kukatisha malengo yao kielimu kutokana na umbali wa shule ambao umekuwa ukisababisha baadhi yao kupata ujauzito.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news