NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kutoa ufadhili wa elimu ya juu (scholarships) kwa wanafunzi watakaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi.
Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma alipokutana na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambapo amesema ufadhili huo utatolewa kwa asilimia mia moja kwa wanafunzi wachache na watasomeshwa ndani na nje ya nchi.
Amesema lengo la Serikali ni kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu na kuhamasisha watoto wengi kupenda kusoma masomo ya Sayansi.

"Kilio cha watu wengi kwa sasa ni ajira na sehemu ambayo ajira ni rahisi zaidi ni kwenye ufundi na ujuzi hivyo ni vizuri kujiandaa. Hili tunalisema mapema ili wanafunzi watakaoomba katika kipindi hicho wajue pia katika vyuo vya ufundi kuna fursa ya kupata mikopo," amesema Prof. Mkenda.
Mhe. Mkenda ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka bilioni 464 hadi kufikia bilioni 570, kuondoa adhabu ya asilimia 10 ya wanaochelewa kurejesha mikopo na kufuta asilimia 6 ya kulinda thamani.
Aidha Waziri Mkenda ametoa wito kwa wanafunzi wanaoomba mikopo ya elimu juu kutoa taarifa zote zinazotakiwa kwa ukamilifu na kwa wakati ili waweze kupata mikopo hiyo bila changamoto.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kwa sasa Wizara imejipanga kuhakikisha Watanzania wengi wanapata fursa ya kusoma elimu ya juu kwa kuwezesha kufanya hivyo kulingana na malengo ya Taifa letu.

