*Aomba bunge kuidhinisha shilingi bilioni 148.9 kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2022/23
NA GODFREY NNKO
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuunda jopo la wataalam ili kufuatilia kwa kina taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo nchini.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Aprili 6,2022 jijini Dodoma wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023.
Amesema, Serikali imezingatia katika upandishaji wa bidhaa kwa kutumia sheria namba 8 ya 2003 ambayo inazuia kupanda kwa bidhaa kwa ajili ya kusaidia wananchi kupunguza makali ya maisha ikiwemo kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma.
“Ninawasihi wazalishaji na wafanyabiashara kuuza bidhaa kwa bei zinazotakiwa na pale itakapobidi kwa watakaopandisha bei ya bidhaa muhimu pasipokuendana na bei halisi, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
"Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Tume ya Ushindani ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini na zile zinazotumia malighafi kutoka nje ya nchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na upandaji huo wa bidhaa muhimu ikiwa ni pamoja na usimamiaji wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya Mwaka 2003 ambayo inazuia kupanga bei.
"Hatua nyingine ni Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada, Serikali inawaelekeza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko ikiwa ni pamoja na kutotumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei,"amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema, katika mwaka 2021, mfumuko wa bei ulikua kwa wastani wa asilimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2020.
Amesema, kuongezeka kwa mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo atahari za UVIKO-19, kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia amesema, mfumuko huo ulikuwa ndani ya lengo la muda wa kati ya asilimia 3-5 ambapo wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) usiozidi asilimia 8 na ndani ya wigo 17 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa kati ya asilimia 3 - 7.
Pia, Waziri Mkuu ameliomba bunge kuidhinisha shilingi bilioni 148.9 kwa ajili ya matumizi ya ofisi yake na taasisi zake kwa mwaka 2022/23, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 101.36 zitaenda kwenye matumizi ya kawaida na zaidi ya shilingi bilioni 47.5 zitaenda kwenye miradi ya maendeleo.
Aidha, kwa upande wa Bunge, Waziri Mkuu ameomba kuidhinishiwa zaidi shilingi bilioni 132.7 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge kati ya fedha hizo shilingi bilioni 127.3 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 5.4 ni kwa ajili ya maendeleo.