NA GODFREY NNKO
BAADA ya dakika 45 za kwanza kutamatika huku ubao ukisoma sifuri kwa wenyeji Simba SC na wageni wao Orlando Pirates vivyo hivyo katika mtanange wa nguvu wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, Simba kipindi cha pili waliamua kufanya yao.
Ni kupitia mtanange wa aina yake ambao umepigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam leo Aprili 17,2022.
Mambo yalikuwa hivi, dakika 45 za kwanza wageni walimiliki mpira kwa asilimia 41 huku wageni wenyeji Simba SC wakimiliki kwa asilimia 59.
Wekundu wa Msimbazi walikoleza kona nne wakati Orlando Pirates wao wakipiga kona moja ndani ya kipindi cha kwanza cha mtanange huo.
Aidha, hakuna aliyeweza kuotea kwa timu zote mbili ndani ya kipindi cha kwanza ingawa Simba SCwameonekana kukosa utulivu eneo la mbele katika kumalizia nafasi ambazo wanazipata.
Kipindi cha pili cha mtanange huo, simba ikiwa tayari imeshasoma ramani yote ya Orlando Pirates, ndipo beki matata Shomari Kapombe alipiga penalti moja tamu, ikatumbukia moja kwa moja katika nyavu.
Ni wazi kuwa, Simba SC imeendelea kuutendea haki uwanja wake wa nyumbani, kwani imekuwa ikifanya vizuri kwenye michezo mingi wakiwa nyumbani.
Wekundu hao watawafuata Orlando Pirates katika mechi ya marudiano ambayo itapigwa Aprili 24, 2022 nchini Afrika Kusini.
Haji Manara
Awali aliyewahi kuwa Msemaji wa Simba SC, Haji Manara ambaye kwa sasa anaitumikia Klabu ya Yanga yenye maskani yake pale Jangwani jijini Dar es Salaam aliiombea klabu hiyo dua njema.
"Mdogo wangu...hatujawahi kuwa maadui Mimi na wewe. Toka mwanzo mimi na wewe ni kama ndugu, nimeondoka huko umekuwa muujiza umekaimu nafsi yangu. Ahmed Ally all the best dogo langu leo pale kwa Mkapa Stadium. Ni do or die.Mpaka fainali,"ameandika Haji Manara.