*Kumenyana nao Aprili 17 jijini Dar es Salaam
NA GODFREY NNKO
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa, Simba SC wanatarajiwa kumenyana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wekundu hao wa Msimbazi wataanzia nyumbani Aprili 17, kabla ya kusafiri kwenda Houghton jijini Johannesburg kwa mchezo wa marudiano Aprili 24, 2022.
Aidha,mechi nyingine za Robo Fainali ni baina ya timu za Libya tupu, Al-Ittihad dhidi ya Al-Ahli Tripoli, Pyramids ya Misri dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al-Masry ya Misri dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Hata hivyo, mechi zote za kwanza zitachezwa Aprili 17, 2022 na marudiano Aprili 24, mwaka huu.
Simba SC walifanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya US Gendamarie ya Niger kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Simba inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pablo Franco Martin yalifungwa na kiungo, Sadio Kanouté dakika ya 63, mshambuliaji Mkongo Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 68 na 78 na kipa Saidu Hamisu aliyejifunga dakika ya 84 katika harakati za kuokoa.
Bernard Morrison alifanikiwa kuseti mabao mawili ya kwanza baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza ambacho wawili hao walienda mapumziko bila kitu.
Kwa nyakati tofauti mashabiki wa Simba SC wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, Orlando Pirates wanapaswa kuwauliza US Gendamarie kilichowakuta pale Benjamin Mkapa kwani, wao wana jambo moja tu la kuhakikisha wanasonga mbele.