SUZA yatoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyotolewa na mwanahabari, Jabir Idrisa kwenye Mkutano wa Rais wa Zanzibar alipokutana na wanahabari Machi 30,2022

SUZA-Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) unakanusha taarifa zilizotolewa na mwanahabari, Bw. Jabir Idrisa zilizouhusisha uongozi wa SUZA na masuala makuu matano aliyoyazungumza mbele ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, alipokutana na waandishi wa habari Jumatano ya Machi 30,2022.

Taarifa hizo, zilizotolewa kwa nia ovu, zimesababisha taharuki isiyo ya lazima kwa umma wakiwemo wasomi, wadau wa elimu, wanajumuiya wa SUZA, wapenda maendeleo pamoja na uongozi mzima wa Chuo.

Katika taarifa yake, Bw. Jabir Idrisa alieleza kuwa ametumwa kuyasema hayo na wanajumuiya wa Chuo na pia alifanya uchunguzi yeye mwenyewe. 

Kwa masikitiko makubwa, Uongozi wa Chuo unashangazwa na kauli hiyo na kutilia mashaka weledi wa Mwanahabari huyo kwa kutoa taarifa hizo bila kufuata misingi ya utoaji wa habari. 

Kwa bahati mbaya sana, katika hicho alichodai kuwa ni uchunguzi wake, hajawahi hata mara moja kufika Chuoni na kuonana na uongozi wa Chuo au waratibu wa miradi husika ili kupatiwa ufafanuzi wa hayo aliyoyasema. 

Taarifa hizo zimekiuka miiko ya uandishi wa habari kwa kuwa ni mawazo binafsi yaliyokosa uwiano (balance) wa upande wa pili. 

Ni jambo la aibu kwa mwanahabari kutumia jukwaa la habari, lililoandaliwa na Mkuu wa nchi, kutoa taarifa za kughushi kwa kisingizio cha kutumwa na wajumuiya wazalendo. 

Ni dhahiri kuwa Bwana Jabir amejificha katika kichaka cha ‘jumuiya na uzalendo’ akielewa kuwa anachokifanya ni ukiukwaji wa maadili ya fani ya habari na kutaka kujenga mazingira ya kujihami juu ya alichokilenga. 

Uongozi wa Chuo unaamini kuwa taarifa hizo ni zake na wala sio za wanajumuiya wa Chuo na hivyo yeye binafsi alipaswa kutimiza wajibu wake na kujiridhisha kuwa ni za ukweli hata kabla ya kuzitoa.

Kufuatia kutolewa kwa taarifa hizo za upotoshaji, uongozi wa Chuo unapenda kutoa ufafanuzi wa hoja hizo kama ifuatavyo:

1. Matatizo ya Utendaji wa Chuo na Uzorotaji wa Maendeleo ya Chuo

Tarifa iliyotolewa ilimhusha Mkuu wa Chuo na Makamu Mkuu wa Chuo pamoja na watendaji wake na matatizo ya utendaji wa Chuo na uzorotaji wa maendeleo haikuwa na mashiko.

Shughuli za chuo zinaendelea kwa kasi kubwa na hakuna shughuli iliyokwamishwa na viongozi ama uongozi wa Chuo. 

Shughuli kuu za Chuo zimeendelea kama kawaida zikiwemo za kitaaluma kama vile usomeshaji, usimamizi wa wanafunzi kwenye tafiti na mambo mengine yanayohusu kazi za kitaaluma kwa kutumia mzunguko wa kitaaluma wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

2. Mradi HEET USD$ Milioni 300 unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo SUZA ni miongoni mwa wanufaika.

Taarifa iliyotolewa kuwa utekelezaji wa mradi huu unasikitisha sio ya kweli. Uongozi wa SUZA unaujuilisha umma kuwa mradi huu hauna masikitiko yeyote na hatua zake zinaendelea vizuri. 

SUZA ni miongoni mwa vyuo vikuu vilivyomo kwenye orodha ya taasisi za elimu ya juu zitakavyopata ufadhili wa mradi wa HEET (Higher Education Economic Transformation) ambao unadhaminiwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MOEST). 

Mradi huu haujaanza kutekelezwa, isipokuwa upo katika hatua za matayarisho kwa taasisi zote za elimu ya juu ambazo zitafadhiliwa. Matayarisho hayo yanahusisha taasisi za Elimu ya juu vikiwemo Vyuo, MOEST na Benki ya Dunia.

SUZA kama taasisi nyingine zote za elimu ya juu zitakazofadhiliwa na mradi huo, inaendelea na matayarisho ya hatua kwa hatua kama inavyoelekezwa na MOEST kulingana na melekezo ya Benki ya Dunia. 

SUZA imeshakamilisha kiasi kikubwa cha matayarisho ya msingi. Matayarisho hayo yanalenga kupata uidhinishwaji wa utayari wa matumizi yanayohitaji manunuzi “no objection” kwa kazi zinazotaka kufanywa. 

Hadi sasa SUZA imeshapakia kwenye mfumo wa Benki ya Dunia “Systematic Tracking of Exchanges in Procurement – STEP” vifungu vyake vikuu vinne na sasa tunasubiri majibu ya Benki ya Dunia kuhusu kukubaliwa na kupewa “no objection” au kupewa marekebisho mengine kama bado yanahitajika. 

Aidha, kwa sasa pia, SUZA inasubiri kukamilika kwa matayarisho ya mikataba ya kuingiziwa fedha, ambayo yanafanywa na MOEST kwa muongozo wa Benki ya Dunia baada ya kukubaliana kipengele kwa kipengele, hatua ambayo ndio iliyofikiwa na vyuo vyote vitakavyofadhiliwa na mradi huu ikiwemo SUZA. 

Kwa mtiririko wa maelezo haya yaliyo sahihi, ni dhahiri kuwa muwasilishaji alimpotosha Mhe. Rais wa Zanzibar pamoja na umma wa Wazanzibari kuhusu utekelezaji wa mradi huu wa HEET kwa upande wa SUZA.

3. Mradi wa DALILA EURO 120,000:

Taarifa zilizotolewa kuwa kuna fedha kiasi ya EURO 120,000 zimetolewa kwa mradi wa DALILA hazikutumika hivyo zinataka kurejeshwa kwa wafadhili kwa kuwa muda wa matumizi umeisha na uongozi ndio ulisababisha. 

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa mradi wa DALILA haujatolewa matangazo ya nafasi za masomo kwa walimu. 

Uongozi wa chuo unaufahamisha umma kuwa, taarifa hizo hazipo sahihi na hazielezi ukweli wa mradi husika na mandeleo yake.

Taarifa sahihi ni kwamba mradi wa DALILA uliopo SUZA wenye udhamini wa Umoja wa Ulaya una thamani ya EURO 134,000, tofauti na ilivyoelezwa. 

Mradi huu una maeneo mawili makuu ya utekelezaji, ambayo ni ununuzi wa vifaa vya maabara na kupitia mtaala ili kuingiza masomo ya “renewable energy”.

Hadi sasa SUZA imeshaingiziwa EURO 74,000 sawa na USD 78,000 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara. 

Fedha hizo zimetumika kwa ununuzi wa vifaa hivyo. Chuo kilifuata utaratibu wa kutangaza zabuni ambapo zabuni ya kwanza ilitangwazwa tarehe 23/09/2020 na walipatikana wasambazaji watatu kama taratibu zinavyotakiwa, tarehe 23/10/2020 Bodi ya Zabuni ilikaa na kutaka Zabuni itangazwe tena baada ya wazabuni wote watatu kuwa na bei ya juu kuliko bajeti. Msambazaji wa kiwango cha fedha cha chini kabisa ilikuwa takribani Bilioni 1.7. 

Zabuni ilitangazwa tena tarehe 03/02/2021 kwa mfumo wa kuwatumia wasambazaji sita na kati ya hao wasambazaji wanne walirudhisha na akateuliwa mmoja aliyekidhi vigezo kwa ajili ya kusambaza vifaa hivyo. 

Kutokana na mripuko wa UVIKO 19 kulitokezea kuchelewa kwa upatikanaji wa vifaa vilivyohitajika hivyo kusababisha vifaa kutopatikana kwa wakati. 

Wakati vifaa hivyo vimepatikana, kupitia msambazaji ilibanika kuwa baadhi ya vifaa vilivyopokelewa havikukidhi vigezo kama vilivyokuwa vimeagizwa. 

Hali hii ya kutokidhi vigezo ilijulikana baada ya wataalamu wetu kuvihakiki na kutoa taarifa, tulijiridhisha kuwa baadhi ya vifaa vilivyoletwa ikiwemo mashine kuu ya kufanyia majaribio, sivyo tulivyoagiza. 

Kutokana na kasoro hiyo, iliyoplekea kukataliwa vifaa hivyo, kumesababisha pesa zilizoingizwa kwa ajili ya manunuzi ya kifaa hicho zisilipwe kwa msambazaji na kuagizwa abadilishe kifaa hicho. 

Kwa vile msambazaji ameshindwa kubadilisha, baada ya mazungumzo alikubali fedha hizo asilipwe na atafutwe msambazaji mwengine. Kwa sasa ameshatafutwa msambazaji mwingine kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na utaratibu unaendelea.

Aina 29 za vifaa vilivyonunuliwa viligharimu shilingi milioni 164,740,000 ambapo kifaa kilichokataliwa kinagharimu shilingi milioni 46,500,000 na ndio kifaa mama cha mradi. 

Matumizi yote ya mradi yanaripotiwa kwa mfadhili kama yalivyo makubaliano ya matumizi hayo. 

Kwa mazingira halisi ya mradi huu, hakuna pesa ambayo imepita muda wa kutumika ambayo inahitaji kurejeshwa. 

Aidha, hakuna fedha ya kusomeshwa wafanyakazi ambayo haijatumika au imepotea kwa kuwa mradi huu hauna kipengele cha kuwasomesha wafanyakazi kama ilivyoripotiwa.

Kwa upande wa mapitio ya mitaala menejimenti ya chuo kupitia kamati yake Kitaaluma na Maktaba ilishakamilisha jukumu lake ambapo kamati ilitoa mapendekezo ya maboresho ya uhakiki wa mtaala mara tatu na kufanyiwa kazi na Idara husika. 

Kamati iliridhia kiwango cha maboresho na kuupendekeza mtaala kuwasilishwa Seneti kwa kuidhinishwa. Seneti iliidhinisha mtaala huo wenye maboresho madogo tarehe 24/03/2022.

Kwa mtiririko huu wa utekelezaji, ni wazi kuwa menejimenti ilitekeleza wajibu wake wakati wote ilipohitajika. 

Hii inadhihirisha kuwa taarifa iliyoripotiwa ya kuwa muda wa utekelezaji unakaribia kwisha na kinachotakiwa kufanywa na chuo hakijafanyika na kutia hofu kuwa fedha za mradi zanataka kurudishwa, ni taarifa ya upotoshaji.

Aidha, kwa wale wanaopitia mitandao yetu ya kijamii wataona kulikuwa na shughuli inayohusiana na mradi wa DALILA iliyofanyika tarehe 24/03/2022 kampasi yetu ya Maruhubi ambayo ni miongoni mwa utekelezaji wa mradi huu.

4. Mradi wa DANIDA na World Bank wa mwaka 2016

Ilielezwa katika taarifa hio kuwa kuna mradi wa DANIDA na World Bank ambao mwaka 2016 vilipatikana vifaa vya kisasa vya maabara ya SUZA vyenye thamani kama bilioni 4, ambavyo mpaka leo hii tangu 2016 vimefungiwa havitumiki. Uongozi wa Chuo unaufahamisha umma kuwa taarifa hio sio sahihi na wala haijafanyiwa uchunguzi wowote.

Taarifa sahihi ni hakuna vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa na Mradi wa DANIDA na World Bank mwaka 2016, ambavyo vimefungiwa havitumiki. 

Vifaa vilivyopo vya BADEA vilinunuliwa mwaka 2017, na ni vifaa vilivyonunuliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali – WEMA kupitia mradi huo wa BADEA, ambavyo vilikuwa ni vifaa vidogo vidogo vya masomo ya fizikia, kemia na biolojia. 

Aidha vifaa vikubwa vilivyonunuliwa mwaka 2016 na mradi wa Badea vilikuwa ni “Liquid chromatography–mass spectrometry – LCMS”, “High Performance Liquid Chromatography – HPLC”, “UV machine”, “STIR machine”, “Scintillation Counter – SC” na “Seed germinator –SG”. Kwanza vifaa hivi vilisimamiwa na WEMA, ambapo katika masharti yake, alihitajika msambazaji kuja kuvifunga na kutoa mafunzo ya utumiaji kama ilivyo kawaida. 

Hivyo, wizara ilivinunua na kuvileta tu hakukuwa na muendelezo wa ufungaji. Pili, kuhusu SG, wizara ilijuilishwa kuwa kifaa hakikufuata sifa zilizotolewa ikiwa ni pamoja na kununuliwa kifaa kipya, ambapo kifaa kilicholetwa kilikuwa kimeshatumika “second hand”. Wizara ilijulishwa na kuwasiliana na mwenyewe, ila hadi leo hajaja kukichukua, na SUZA haina taarifa kama muhusika alilipwa na wizara au la.

Vifaa vilivyonunuliwa na Benki ya Dunia vilinunuliwa mwaka 2012, ambavyo vilikuwa ni “Gas Chromatography - GSMS”, “Atomic absorption spectroscopy – AAS”, “Laminar flow”, “microscope” pamoja na vifaa vidogo vidogo vya kemia na fizikia.

Uongozi wa Chuo ulitembelea maabara za Skuli ya Sayansi Asili na Sayansi Jamii mwezi Januari 2022, baada ya kukabidhiwa Chuo kukisimamia mwezi Novemba 2021 kwa lengo la kuangalia mazingira halisi na kubaini matatizo na changamoto zilizokuwepo ili kupanga vipaumbele katika utekelezaji wa usimamizi wa shughuli za chuo. Ziara hizi zilifanyika kwa Skuli zote na kampasi zote za Chuo. 

Vifaa hivi vilionekana kuwa vipo kwenye matumizi katika maabara husika. Kilichofanyika ni kubadilishwa vifaa vilivyonunuliwa na Benki ya Dunia 2012 kwa vifaa vilivyonunuliwa na BADEA 2017 kwa kuwa vinafanya kazi zinazofanana. 

Aidha, ni kwamba kuna changamoto zilizowasilishwa na wataalamu wa maabara, miongoni mwao ikiwa ni ukosefu wa taaluma ya kutosha ya kuzitumia vifaa hivyo. Hii imetokana na kuwa mafunzo yanayotolewa na wasambazaji yanakuwa ya muda mfupi na hayatoshelezi mahitaji ya kupata utaalamu wa kutosha, hususan kwa kuwa vinatumia teknolojia kubwa ya kisasa.

Kwa kuiona changamoto ya baadhi ya vifaa kutotumika kwa ufanisi, Uongozi wa Chuo unaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha vifaa hivyo vinaweza kutumika. Uongozi ulifanya mawasiliano na kuonana na Mkurugenzi wa Tropical Pestside Research Authority (TPRA) tarehe 21 Februari, 2022 kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kubadilishana wataalamu na kupata nafasi wataalamu wetu kujifunza utumiaji wa vifaa hivyo. 

Mazungumzo hayo yamekua na ufanisi mkubwa na hivi sasa SUZA na TPRA tupo katika mpango wa kuandaa MOU kwa maudhui hayo. 

Aidha Mkuu wa Skuli ya Sayansi Asili na Sayansi ya Jamii SUZA ametembelea National Laboratory Association of Tanzania (NLAT) kwa lengo la kuweza kupata wataalamu watakaowapa mafunzo wataalamu wetu ili vifaa vyote viweze kufanya kazi kwa uwezo unaotakiwa. Hatua ambayo inatarajiwa kuwa ni ya mafanikio.

Kwa kuzingatia jukumu la uongozi na jukumu la waratibu wa miradi katika kutoa huduma ya utawala katika kuendesha miradi, ni wazi kuwa haitokua sahihi kudai kuwa uongozi wa Chuo hautekelezi majukumu yake. 

Kutumia hoja ya vifaa vya 2016 kumuandama Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wake na uongozi wote uliopo hivi sasa, mbali ya jitihada wanazochukua kuimarisha mazingira bora ya utendaji, ni kitendo cha hujuma za makusudi dhidi ya uongozi chenye lengo la kuupaka matope uongozi na Chuo na kuchochea mivutano.

5. Kiongozi Mmoja Amekwepeshwa Kuona Eneo Fulani Wakati wa Ziara

Ilitolewa taarifa kuwa kuna kiongozi mmoja amekwepeshwa kuona maeneo fulani ya SUZA wakati Mheshimiwa mmoja alipotembelea SUZA na waliomkwepesha ni waliomuandalia ziara hiyo.

Hakuna ukweli wowote wa ukwepeshwaji wa kutembelea eneo lolote la SUZA. Viongozi wote wanaofika SUZA wanapewa uhuru wa kuonana na kuona eneo lolote. Yumkin Bwana Jabir alikusudia kutoa taarifa ya ziara, kwa bahati mbaya sana hakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya alichokiwasilisha. Badala yake aligubikwa na utashi wa mawazo binafsi ambayo hajayathibitisha.

Kiongozi aliyetembelea mara ya mwisho SUZA ni Makamu wa Kwanza wa Rais Wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, ambae alitembelea tarehe 22 Machi, 2022. Ziara hii hakuandaliwa na kiongozi yeyote wa SUZA, bali ni ziara iliyoratibiwa na ofisi yake na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutembelea sekta ya elimu kwa upande wa kisiwa cha unguja iliyoanza tarehe 21 hadi 25 Machi, 2022. 

SUZA ilipokea taarifa ya ziara hio kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali tarehe 18 Machi, 2022. Taarifa hiyo haikuainisha maeneo ambayo Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais atatembelea bali kila taasisi ilitakiwa kujipanga kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa. Mhe Makamu alifika SUZA kwa ziara, iliyopangwa kufanyika kwa muda wa saa moja tu.

Wakati wa muendelezo ya kikao kati ya Mhe. Makamu na menejimenti ya SUZA, menejimenti ya SUZA ndiyo iliyopendekeza kwa Mhe. Makamu wa Kwanza wa Rais na kumuomba atembelee maeneo matatu kati ya manne ambayo ni maabara zilizopo Jengo la Sayansi, Maabara ya ndege zisizo na rubani “DRONE” na SUZA TV na CDL zilizopo jengo la Kompyuta. 

Timu ya protokali ya Mhe. Makamu, ndiyo iliyomshauri Mhe. Makamu kuwa kutokana na muda uliobakia na ratiba ilivyo, muda hautatosheleza kutembelea maeneo yote haya na waliamuru asiendelee kutembelea maeneo mengine kwa vile tayari amekuwa nje ya muda na alitakiwa kuendelea na ziara yake katika tasisi nyengine. Hivyo alipata nafasi ya kutembelea CDL tu. 

Ingawa alikuwa tayari yupo nje ya muda, na aliweza kutoa mapendekezo yake mazuri juu ya uendelezaji wa utoaji wa huduma katia eneo hilo. Kwa mustakbali huo, ni wazi kuwa taarifa iliyowasilishwa ya kukwepeshwa Mheshimiwa mmoja alipotembelea SUZA ni ya kubuni na ni yenye kupotosha umma.

Uongozi wa Chuo umesikitishwa sana na maelezo ya upotoshaji mkubwa aliyoyatoa mwanahabari Jabir Idrisa mbele ya Mh. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar. 

Kutoa taarifa za upotoshaji mbele ya Mhe. Rais, ni kitendo cha ukosefu wa maadili ya kazi ya uandishi wa habari. Jamii ingetarajia kwa mwandishi wa habari, kuzithibitisha taarifa alizozipata kwa kupata maelezo kutoka upande wa uongozi ama wasimamizi wa miradi aliyoitaja. 

Uongozi wa chuo unamshauri na kumkumbusha mwanahabari Jabir Idrisa kufuata misingi ya taaluma ya uandishi kwa kutoa habari za uchunguzi na zenye ukweli kutoka kwenye vyanzo sahihi vya habari pamoja na kuzithibitisha kabla ya kuzisambaza.

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar unapenda kuarifu umma na kuutoa hofu na mashaka yaliyotokana na taarifa hizo zisizo na ukweli. 

SUZA ni Chuo cha Umma kinachomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinafanya kazi zake kwa kutumia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya uendeshaji. 

Chuo kina uongozi makini ulioaminiwa kufanya kazi zake kwa uhuru kwa kutoa huduma zilizo bora na zenye kuleta maendeleo ya kielimu nchini ili kufikia malengo makuu ya serikali. 

Tunawaomba wadau wote wa elimu na wapenda maendeleo ya kweli kuzipuuza taarifa za upotoshaji na kuwa na imani ya Chuo chao. Uongozi wa Chuo unaendelea kukabilina na kuondoa changamoto zilizopo, ambazo zote zimesharipotiwa katika ngazi husika na zinaeleweka, kwa lengo la kutengeneza ustawi bora wa Chuo utakaojenga misingi ya maendeleo. 

SUZA ipo tayari muda wowote kushirikiana na kila mdau katika kukuza maendeleo yake na ya taifa kwa ujumla.

Hakuna chochote kilichozorota, shughuli zote za Chuo zipo kwa mujibu wa kalenda ya matukio. Na harakati za maendeleo ya Chuo zinaendelea lwa kasi. 

Kwa uchache wa mifano, kuanzia mwezi Januari hadi Machi Chuo kimeongeza program nne za masomo baada ya kufikia ubora unaohitajika na kupata ithibati ya kufundisha Master of Business Administration in Finance, Master of Science in Banking, Bachelor of Science in Medical Laboratory Sciences na Bachelor of Arts in Mass Communication program zote hizo zitaanza kudahili wanafunzi kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023. 

Kwa upande wa miradi Chuo inaendelea kutekeleza miradi iliyopo na kinaendelea kutafuta miradi mipya ambapo kwa kipindi cha mwezi Febuari na Machi miradi mipya mitatu imepatikana na tayari imeanza kazi.

Wito wa uongozi wa Chuo kwa umma ni kuendelea kuwa pamoja na kuunga mkono jitihada za Mkuu wa Chuo, ambae kwa bahati njema ndio Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, za kuleta maendeleo katika sekta ya elimu nchni, na kuunga mkono juhudi za wasaidizi wake kupitia ngazi mbali mbali ikiwemo menejimenti na Baraza la Uongozi la SUZA na kupuuza uchochezi wa wachache wenye sifa za kupaka matope kila zuri linalofanywa.

SUZA Kichocheo cha Mabadiliko ya Jamii

Imetolewa Aprili 4,2022 na,

Prof. Moh’d Makame Haji
Makamu Mkuu wa Chuo, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news