Tanzania, Uingereza mguu sawa mapambano usafirishaji haramu wa watoto

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Tanzania na Uingereza zimekubaliana kuweka mikakati ya pamoja kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto hasa maeneo ya mipakani.
Hayo yamebainika Aprili 04, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Mhe. Vicky Ford iliyolenga kujadiliana na kutafuta suluhu ya tatizo la usafirishaji haramu wa binadamu wakiwemo watoto.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema, Uingereza imeahidi kutoa jengo maalum kwa ajili ya kutoa huduma za pamoja.Lengo likiwa ni kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kupata huduma za afya, ushauri wa kisaikolojia, msaada wa kisheria na huduma za polisi katika eneo moja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi na uwajibikaji wa pamoja unahitajika kwa wataalam mbalimbali wanaohusika na kusaidia waathirika wa vitendo vya ukatili ili kusaidia kutoa huduma stahiki kwa uharaka na urahisi kwa kuokoa jamii.

"Huduma hizi zitapatikana hapa hapa katika eneo moja na hasa kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza tumekusudia kubadili mazingira na kuleta huduma za pamoja kwa wahanga wa vitendo vya ukatili katika jengo la British Council na hii itakuwa ni kwa kuanzia na maeneo haya yatasambaa kila mkoa,"amesema Dkt.Chaula.

Naye Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika, Mhe. Vicky Ford amesema, tatizo la usafirishaji haramu wa watu inaongezeka kwa kasi hasa katika mipaka hivyo kutishia ustawi wa jamii hasa watoto.

Mhe. Vicky ameeleza kuwa Uingereza ipo tayari kushirikiana na Tanzania hasa katika kuweka mipango mikakati ya kuhakikisha tatizo la usafirishaji haramu wa watu hasa Watoto linapungua kama sio kutokomezwa kabisa."Usafirishaji haramu wa watu ni shida ni tatizo kubwa hasa kwa nchi za Afrika ambazo zimekuwa njia ya kusafirisha watu kwenda nchi za Ulaya. Tudhibiti hili tuiokoe jamii yetu," amesema Mhe.Vicky.

Naye Meneja Simu ya Huduma kwa Mtoto 116, Thelma Dhaje amesema, uwepo wa vituo vya pamoja vya kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia itasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu kwa waathirika wa vitendo hivyo na kuwahakikishia upatikanaji wa haki kwa wanaofanyiwa vitendo vya ukatili.

Aidha, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Asia Mkene amesema uwepo wa kituo cha pamoja ya kutoa huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukatili itakuwa suluhisho kwa kuhakikisha huduma zote zinapatikana kwa wakati katika eneo moja na kuharakisha utoaji huduma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news