*Kwa kushirikiana na Voice of Empowered Women Foundation inakusudia kupanda miti zaidi ya 28,000 katika maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro
NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KAMPUNI ya mtandao wa simu za mkononi ya Tigo, imeadhimisha siku ya wajinga duniani kwa kufanya kampeni ya kupanda miti waliyoiita kuwa mjanja panda mti kuifanya Aprili ya kijanja na kurejesha theluji ya Mlima Kilimanjaro.
Tigo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Voice of Empowered Women Foundation (Voewofo)inakusudia kupanda miti zaidi ya 28,000 katika maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro, lengo likiwa ni kulinda theluji ya mlima huo mrefu barani Afrika.
Akizungunza leo Aprili Mosi, 2022 wakati wa kampeni hiyo katika Kijiji cha Kwasadala Wilaya ya Hai,mkoani Kilimanjaro Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya, amesema wataendekea na jitihada za kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya kuzunguka mlima Kilimanjaro.
"Tarehe Mosi Aprili inafahamika kama siku ya wajinga, lakini sisi kama Tigo tunasema kuwa mjanja panda mti kuifanya Aprili ya kijanja na kurejesha theluji ya mlima Kilimanjaro, na katika kulifanikisha hili tumepanda miti leo na tutaendelea kupanda miti maeneo mbalimbali ili kuulinda mlima Kilimanjaro,"amesema.
Ameongeza kuwa, "Tutapanda miti zaidi ya 28,000 kwa mwaka huu na tunawaomba wananchi watuunge mkono kulifanikisha hili na kuwezesha kuyafikia malengo ya kuyafanya mazingira kuwa ya kijani".
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Voewofo, Julius Ezekieli amesema, wanashirikiana kwa kwa karibu na Tigo kuendesha kampeni hiyo kuhakikisha wanalinda theluji ya Mlima Kilimanjaro.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matowo Kijiji cha Kwasadala, amesema katika kuhakikisha miti inayopandwa inakuwa na kustawi, wameweka kijana wa kuitunza na kutunga sheria ndogo ambayo itawabana wale wote watakaoingiza mifugo na kuharibu miti.
"Tumeweka sheria kali, ng'ombe mmoja akikamatwa katika eneo hili la miti adhabu yake ni faini ya shilingi 100,000, na lengo letu si kupata fedha, tumeweka adhabu kali ili kuwafanya wananchi waogope na kudhibiti mifugo yao kufanya uharibifu,"amesema.