TPDC kushiriki Michezo ya Mei Mosi 2022 mkoani Dodoma

NA MWANDISHI MAALUM

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo ndilo Shirika la Mafuta la Taifa, linatarajia kushiriki katika Michezo ya Mei aa kitaifa mkoani Dodoma kuanzia Aprili 16,2022 hadi Aprili 31,2022 ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani.
TPDC inakuwa moja ya Mashirika ya Umma ambayo yanashiriki michezo hii kama sehemu ya kuimarisha afya na mahusiano kwa watumishi wake ili kuhakikisha linaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika sekta ya mafuta na gesi.

Si mara ya kwanza kwa TPDC kushiriki katika michezo hii ambapo katika Michezo ya Mei Mosi 2021 iliyofanyika jijini Mwanza, timu za TPDC zilishika nafasi ya tatu kwa upande wa mpira wa miguu wanaume, mshindi wa tatu kuvuta kamba wanaume, mshindi wa pili kuvuta kamba wanawake na mshindi wa kwanza karata wanaume.

Akizungumzia kuhusu maandalizi ya TPDC katika kushiriki michezo hiyo, Meneja wa Michezo wa TPDC bwana David Kidenya alisema kwamba, TPDC imejiandaa vizuri na wanatarajia kusafiri kwenda mkoani Dodoma siku ya Aprili 16,2022 ambapo wanaamini watataoa upinzani mkali kwa wapinzani wao na hatimaye kutwaa vikombe katika michuano hiyo. 

Bwana Kidenya alisema “michezo ni furaha, michezo ni amani na tunakwenda kushindana kwa lengo la kutwaa vikombe lakini pia kujifunza kwa wenzetu na kutengeneza mahusiano yatakayosaidia kuboresha zaidi utendaji wetu wa kazi kila siku pamoja na Shirika kwa ujumla”.

Bwana Kidenya aliendelea kwa kusema kuwa, TPDC itaendelea kutumia michezo hiyo kama sehemu ya kujitangaza zaidi kwa umma kwa lengo la kuufahamisha umma kuhusu shughuli za Shirika hilo pamoja na mchango wake katika ujenzi wa Taifa.

Aidha Bwana Kidenya alimalizia kwa kusema kwamba, TPDC itapeleka wachezaji katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba (wanaume na wanawake), baiskeli (wanaume na wanawake), karata (wanaume na wanawake), mchezo wa bao wanaume na wanawake pamoja na riadha kwa wanaume na wanawake.

Kwa upande wake, nahodha wa timu ya mpira wa miguu ya TPDC, Bwana Dalushi Shija, alisema kwamba mwaka huu wamejiandaa vyema na wana uhakika wa kufanya vizuri zaidi. “Wachezaji wapo katika hali nzuri, tunaendelea na mazoezi na tunaamini kwa mazoezi tunayoendelea nayo na mbinu anazotupa mwalimu, tutafanya vizuri zaidi,”alisema Bwana Shija. TPDC imepangwa kundi moja na vigogo wa Tamisemi pamoja na Ulinzi katika kundi C kwenye mchezo wa mpira wa miguu.

Kwa upande wake Bi. Elinaike Naburi ambae ni nahodha wa timu ya TPDC mpira wa pete (wanawake) alisema kwamba michezo ya mwaka huu licha ya wapinzani wao kujiandaa vizuri, anaamini TPDC itatoa upinzani mkali kwa timu zote itakazokutana nazo na hatimaye kuibuka washindi.

Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi 2022 anatarajiwa kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo timu 21 kwa upande wa mpira wa miguu, 23 mpira wa pete pamoja na timu 14 katika mchezo wa Kamba zinatarajia kutoana jasho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news