*Ukaguzi huo umezifikia taasisi za Serikali Kuu 31, taasisi za umma 35 na mamlaka za Serikali za Mitaa 44
NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Jenista Mhagama amewataka watumishi wa umma nchini kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma kwa ustawi bora wa taasisi na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo ameitoa leo Aprili 2,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
"Pia nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanasimamia haki na stahili za watumishi wao ili kupunguza kama si kuondoa kabisa malalamiko yanayotolewa na watumishi wa umma kutokana na kutopata au kucheleweshewa stahili zao ikiwemo stahiki za likizo, upandaji wa madaraja, kuthibitishwa kazini na kupitishiwa barua mbalimbali.
"Kwa kufanya hivyo, waajiri na watumishi wa umma tutakuwa tumeunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kujenga mazingira wezeshi ya utumishi wa umma,kuendelea kuwa injini ya maendeleo ya nchi yetu na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati wa juu,"amesema Waziri Mhagama.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Pia Mheshimiwa Jenista Mhagama ameilekeza Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema, upo umuhimu mkubwa wa kufanya ukaguzi kwenye taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi kama za afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.
Mheshimiwa Waziri Mhagama amesema, ukaguzi wa rasilimali watu una faida kubwa kwa Serikali, waajiri, watumishi wa umma na Watanzania kwa ujumla ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake.
Pia ameongoza kuwa, unazisaidia pia taasisi zilizokaguliwa kurekebisha kasoro za kiutendaji ambazo zimebainishwa wakati wa ukaguzi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri amesema, ukaguzi huo unaiwezesha Serikali kufahamu hali ya utendaji kazi iliyopo katika taasisi za umma na kuziwezesha mamlaka husika kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa taasisi zote za umma.
Aidha,amesema ukaguzi huo unaipa fursa Tume ya Utumishi wa Umma kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya namna bora ya kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili iwe na tija kwa umma na taifa kwa ujumla.
Wakati huo huo, akizungumzia kuhusiana na migogoro ya kiutendaji inayojitokeza kwenye baadhi ya taasisi, Mheshimiwa Mhagama amesema, taasisi hizo zikitekeleza maelekezo ya tume baada ya kufanyiwa ukaguzi zitaepusha migogoro kwa kiasi kikubwa.
Hata hiyo,Tume ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu kwenye taasisi za umma 110, hivyo taarifa ya ukaguzi huo inaandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua stahiki.
Idadi hiyo inajumuisha taasisi za Serikali Kuu 31, taasisi za umma 35 na mamlaka za Serikali za Mitaa 44 ambapo tume inafanya ukaguzi kwenye maeneo saba.
Maeneo hayo ni ajira mpya na mbadala,upandishwaji vyeo,mafunzo kwa watumishi,uendeshaji wa mchakato wa nidhamu,likizo ya mwaka,likizo ya ugonjwa na upimaji wa wazi wa utendaji kazi.