Uber yasitisha kwa muda huduma zake Tanzania

NA DIRAMAKINI

KAMPUNI ya Uber imesema imechukua uamuzi mgumu wa kusitisha kwa muda huduma za UberX, UberXL na UberX Saver nchini Tanzania ambapo huduma hizi hazitapatikana kuanzia leo Aprili 14, 2022.
Uber wametuma ujumbe kwa Wateja wao mbalimbali unaosomeka "Kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hii zimejenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yetu, hadi pale muafaka utakapopatikana, hatutaendelea kutoa huduma za usafiri wa UberX, UberX Saver na UberXL nchini Tanzania.

"Nauli elekezi iliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesababisha changamoto kubwa kwa mifumo kama Uber kuendelea kutoa huduma kwa wateja wetu, inakuwa ngumu kwetu kuendelea kutoa huduma, hatutaweza kutoa huduma mpaka pale mazingira yatakapokuwa rafiki kwa sisi kuendelea kutoa huduma.

"Tunapenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa dhati kwa kuchagua mfumo wetu kufanya safari zako jijini Dar es Salaam ambako tumekuwa tukitoa huduma zetu kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, huu ni wakati mgumu kwetu sote, lakini hii haina maana kwamba ndio mwisho wa kila kitu.

"Tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija na kujenga mazingira wezeshi na tutarudi na kuendelea na kukupa usafiri wa kutegemewa na wa uhakika ambao umekuwa ukiitumia, baada ya kujiridhisha kwamba mazingira ya kibiashara ni rafiki, tunafahamu kwamba hiki ni kipindi kigumu na usumbufu unaotokana na uamuzi huu na tunapenda kukuhimiza uwasiliane nasi kupitia kwenye app ikiwa una maswali yoyote,"amefafanua.

Uber ni nini?

Uber ni jukwaa ambalo wale wanaoendesha na kusafirisha mizigo wanaweza kuunganishwa na wanunuzi, walaji na migahawa.

Katika miji ambako Uber inapatikana, unaweza kutumia programu ya Uber kuomba usafiri.

Wakati dereva aliye karibu anakubali ombi lako, programu huonyesha muda uliokadiriwa wa kuwasili kwa dereva anayeelekea eneo lako la kukuhudumia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news