NA JAMES K.MWANAMYOTO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameilekeza Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kufanya ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari alipokuwa akielezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimaliwatu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma. Kulia kwake ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Mhe. Jenista amesema, upo umuhimu mkubwa wa kufanya ukaguzi kwenye taasisi zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi kama za afya, elimu, maji, kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja.
Akizitaja faida za ukaguzi wa rasilimali watu, Waziri Jenista amesema, una faida kubwa kwa Serikali, Waajiri, Watumishi wa Umma na Watanzania kwa ujumla ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Ameongoza kuwa, unazisaidia pia taasisi zilizokaguliwa kurekebisha kasoro za kiutendaji ambazo zimebainishwa wakati wa ukaguzi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia amesema ukaguzi huo unaiwezesha Serikali kufahamu hali ya utendaji kazi iliyopo katika taasisi za umma na kuziwezesha mamlaka husika kufanya maamuzi yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi wa taasisi zote za umma.
Sanjari na hayo, Waziri Jenista amesema ukaguzi huo unaipa fursa Tume ya Utumishi wa Umma kutoa mapendekezo kwa Serikali juu ya namna bora ya kuboresha Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo ili iwe na tija kwa umma na taifa kwa ujumla.
Baadhi ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuelezea uhitimishaji wa zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu katika taasisi za umma kwa mwaka wa fedha 2021/2022 lililofanywa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Kuhusiana na migogoro ya kiutendaji inayojitokeza kwenye baadhi ya taasisi, Mhe. Jenista amesema taasisi hizo zikitekeleza maelekezo ya Tume baada ya kufanyiwa ukaguzi zitaepusha migogoro kwa kiasi kikubwa.
Tume ya Utumishi wa Umma imekamilisha zoezi la ukaguzi wa rasilimali watu kwenye Taasisi za Umma 110, hivyo taarifa ya ukaguzi huo inaandaliwa kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua stahiki.