NA DIRAMAKINI
WAKAZI wa Kata ya Ulowa iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu mkoani Shinyanga wamesema wanakabiliwa na changamoto ya kuwepo kwa tetemeko la ardhi ambalo limekuwa likitokea kwa sauti kubwa ya mlipuko chini ardhini, mara kwa mara hali inayowafanya waishi kwa hofu juu ya usalama wa maisha yao.
‘’Sisi wakazi wa Ulowa kutokana na tetemeko hili kila linapotokea limekuwa likitoa sauti ya mlipuko mkubwa chini ya ardhi na kutufanya baadhi yetu wenye nyumba zisizo kuwa imara kulala nje kwa kuhofia usalama wa maisha yetu,"alisema mmoja wa wakazi hao.
Wamesema kuwa, tetemeko hilo la ajabu limeanza kutokea kidogo kidogo tangu mwezi Agosti mwaka 2021 na limekuwa likiongezeka siku kwa siku na hadi sasa mtikisiko wake na mlipuko umezidi kuongezeka na kuleta taharuki kwa wakazi wa Ulowa.
Donard Shija mkazi wa eneo hilo alisema kuwa, tetemeko na mlipuko huo unapotokea hutoa sauti kama milipuko ya ulipuaji wa miamba na kwa sasa imekuwa ikitokea kwa siku mara 10.
“Matetemeko ya ardhi nayafahamu toka mwaka 1984, lakini hili linalotupata hapa kwetu Ulowa kwa siku nyingi na kujirudia mara kwa mara limekuwa si la kawaida kutokana na kutoa mlipuko chini ya ardhi, kwa hiyo tunaiomba serikali kufanya uchunguzi kujua hali hiyo,"amesema Shija.
Shija alisema, wanaiomba Serikali kuleta wataalamu wafike na kufanya uchunguzi ili wananchi waweze kuwaondolea hofu na kuwafanya waishi kwa amani na kuondokana na hofu waliyonanayo iliyozolotesha shughuli zao za uzalishaji mali kufuatia tetemeko hilo.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokaji wa Wilaya ya Kahama, Hanafi Mkilindi alisema huenda eneo hilo likawa ni mkondo wa njia ya tetemeko la ardhi kutokana na kuwa linatokea mara kwa mara na kwa mlipuko chini ya ardhi.
Afisa Madini Mkazi wa Kimkoa wa Madini wa Kahama, Jeremiah Hango alisema kuwa walifika katika eneo hilo na kusikia mitikisiko na kuongeza kuwa katika Wizara ya Madini kuna kitengo ambacho kinahusika na mambo hayo cha G ST na wataalamu watakuja kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya hali hiyo.
Mkuu Wilaya ya Kahama, Kiswaga alisema tayari Serikali ilishapokea tatizo hilo la wananchi wa Ulowa na itatuma wataalamu wake ili kufanya uchunguzi juu ya tetemeko hilo pamoja na kutoa elimu itakayowaondolea hofu wananchi hao.