Wabunge wanawake waelimishwa fursa zilizopo Sekta ya Madini

NA TITO MSELLEM-WM

MWENYEKITI wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Shally Raymond amewataka wabunge hao kuwahamasisha wanawake nchini kushiriki katika uchumi wa madini ili waweze kupambana na tatizo la ukosefu wa ajira kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi za uwekezaji zilizopo katika sekta hiyo. Ameyasema hayo Aprili 23, 2022 wakati akifungua Semina kwa Wabunge Wanawake Tanzania iliyofanyika katika Ukumbi wa Msekwa bungeni Dodoma na kuratibiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iliyolenga kuwajengea uwezo wabunge hao kutambua fursa zilizopo katika Sekta ya Madini, kujua namna shughuli za sekta zinavyofanyika na hatimaye kuwa sehemu ya wahamasishaji na kushiriki katika uchumi huo.

Ameongeza kuwa, semina hiyo itawasaidia wabunge hao kuitazama Sekta ya Madini kwa jicho la tofauti na kuwataka kuifikisha elimu waliyoipata katika ngazi zote kuanzia kwenye familia, jamii na maeneo wanayowawakilisha wananchi.
‘’Wanawake ni viungo muhimu katika serikali na jamii, naomba tutumie elimu hii kuwaelimisha wananake kushiriki katika uchumi wa madini ili kuepukana na tatizo la ukosefu wa ajira na kujipatia vipato,’’amesisitiza.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuipongeza wizara kutokana na kuendelea kuimarika kwa mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa ambapo amesema kuwa, katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021, mchango wa Sekta ya Madini umeongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 6.5 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema wizara imeona umuhimu wa kuujengea uelewa umoja huo ili kutoa hamasa kwa wanawake kushiriki katika uchumi wa madini baada ya kuona kuwa shughuli nyingi katika Sekta ya Madini bado zinafanywa na wanaume.
Amesema kutokana na tofauti hiyo, Serikali kupitia wizara ya madini inaendelea kuchukua hatua ili wanawake wengi waweze kushirikki katika shughuli hizo na kuongeza kuwa, tayari Rais Samia Suluhu ameweka mazingira ya kuwawezesha wanawake kushiriki katika uchumi wa madini.

‘’Mfumo katika Sekta ya Madini ulimweka mwanamke kama mtu duni, Rais amekwisha weka msukumo wa wanawake kushiriki uchumi wa madini na sisi kwa upande wetu tunaendelea kuwahamasisha na tunashukuru wapo wachache wanashiriki na wanafanya vizuri kwenye shughuli hizi,’’ amesema Dkt. Biteko.
Wakiwasilisha mada katika semina hiyo, taasisi za fedha zikiwemo benki za CRDB na NMB zimeleezea kuhusu aina ya mikopo inayotolewa na benki hizo ambazo wachimbaji na wadau wa madini wanaweza kuzitumia katika kupata mikopo na kuendeleza shughuli zao na kuwataka wadau wa madini kuzitumia.

Akizungumza katika Semina hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Benki ya NMB Aikansia Muro amesema tayari benki hiyo imetoa kiasi cha shilingi bilioni 15 kama mikopo kwa wachimbaji wadogo hadi sasa na kuongeza kwamba, benki hiyo haina pingamizi lolote kwa wote wanaotaka kufanya shughuli zinazohusisha mnyororo mzima wa shughuli za madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Serikali Benki ya CRDB Noelina Kivaria, amesema kuwa benki hiyo inazo huduma mbalimbali za mikopo ikiwemo ya Malkia ambapo hata wadau wenye mitaji ya chini kabisa wanaweza kuitumia kupata mikopo kuendeleza shughuli zao za madini na hivyo kuwahamasisha kuitumia benki hiyo.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse akitoa mada katika semina hiyo, amewaeleza wabunge hao kuwa, tayari shirika hilo limepata Cheti cha Ithibati kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa ajili ya mradi wake wa makaa ya mawe ya kupikia ambapo shirika hilo lilikuwa likisubiri matokeo ya sampuli za makaa hayo kabla ya kusambazwa kwa walaji.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini hivi karibuni, Dkt. Mwasse aliieleza kamati kuwa, mtambo wa majaribio wa uzalishaji wa makaa hayo umesimikwa katika eneo la TIRDO Dar es Salaam na una uwezo wa kuzalisha tani 2 kwa saa.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Sambamba akizungumzia fursa zilizopo katika Sekta ya madini, amesema asilimia 95 ya nchi ya Tanzania ina viashiria vya madini ya aina mbalimbali hali ambayo inachochea uwepo wa fursa nyingi katika sekta ya madini na kuwaeleza wabunge kuwa, wananchi na wadau wanaweza kuzitumia kupitia nyaja nyingi ikiwemo kupitia biashara ya madini, uongezaji thamani madini , uchimbaji na nyingine nyingi.

Akifunga semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula ameipongeza STAMICO kwa hatua iliyofikia ya kupata ithibiti tayari kwa kuzalisha makaa hayo na kuongeza kuwa, ni mradi muhimu ambao utasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira kwa kutokukatwa miti kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

Mbali na wabunge hao, semina hiyo imehudhuriwa na watumishi wa bunge, wawakilishi wa Benki za CRDB na NMB , viongozi waandamizi wa wizara na taasisi zake na wataalam wa sekta kutoka wizara na taasisi zake ambapo pia, mada kuhusu shughuli za uongezaji thamani madini imetolewa na Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Daniel Kidesheni
Pia, katika semina hiyo, wanawake kutoka Chama Cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania (TAWOMA) wametoa ushuhuda wa namna serikali kupitia STAMICO inayoweka jitihada za kuwaendeleza kufanya shughuli zao kwa tija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news