NA GODFREY NNKO
MAAFISA wa Jeshi la Polisi nchini Israel wanadaiwa kuwazuia Wakristo kufika katika Kanisa la Ufufuo mjini Jerusalem ili kuadhimisha Sherehe ya Moto Mtakatifu.
Sherehe ambayo katika Kalenda ya Orthodox ni Jumamosi Kuu, siku moja kabla ya Pasaka ya Waorthodoksi.
Maelfu ya Wakristo walizuiwa kwenda kanisani. Picha na video kutoka eneo la tukio na Jiji la Kale la Jerusalem zilionesha idadi kubwa ya polisi wa Israel na vizuizi vilivyowekwa kwenye milango ya kanisa.
Maafisa wa polisi wa Israel walionekana wakiwasukuma na kuwapiga wanawake na makasisi, wakiwaweka mbali na jengo hilo.
Tukio hilo lilitokea wakati baadhi ya mahujaji walipojaribu kuvuka vizuizi kwa nguvu na maafisa wa polisi walijaribu kuwazuia. Maafisa hao walijibu kwa jeuri na video moja ikimuonyesha polisi akishika shingo ya ujaji mmoja.
Polisi hawakuripoti tukio hilo katika taarifa zao rasmi, bali walisema kwamba, "tangu asubuhi na mapema mchana, Polisi wa Israeli walichukua hatua ili kuwezesha sherehe ya Moto Mtakatifu kuwa salama ...kukamilika baada ya tathmini ya kina, kazi kubwa ya wafanyakazi, ziara ya nje, mikutano ya uratibu na viongozi wa kanisa na idhini ya mipango inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Yerusalemu."
Mamia ya polisi, walinzi wa mpaka na watu wa kujitolea walitumwa na kufanya kazi ili kudhibiti washiriki katika eneo hilo.
Sherehe hiyo ya ajabu ya milenia, ambayo inaadhimisha Ufufuko wa Yesu, imevutia maelfu ya waabudu kutoka pande mbalimbali za Dunia.
Baada ya saa za kutazamia kutoka kwa umati wa watu, Padri wa Kanisa la Orthodox la Ugiriki la Jerusalem aliingia kwenye kaburi ambalo Wakristo wanaamini kuwa Yesu alizikwa na akaibuka akiwa amebeba mshumaa uliowashwa bila kutumia kiberiti.
Ndani ya sekunde chache, nuru ilienea katika kanisa lililotiwa giza ambalo linaheshimiwa na Wakristo kama mahali pa kusulubishwa kwa Yesu, kuzikwa na kufufuka. Kengele zilishindana kupigwa huku shangwe kutoka kwa umati wa kusanyiko la watu zikitawala.
Michael Toumayan, Mkristo wa Armenia mwenye umri wa miaka 36,alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupokea nuru hiyo. Katika mahojiano na Jerusalem Post amesema kuwa, "Ni heshima," alisema. "Baba yangu amekuwa akifanya hivi tangu akiwa mtoto na ananipitisha katika mila hii."
Baada ya miaka miwili ya vizuizi vya kusafiri vya UVIKO-19, Israeli hivi karibuni imeanza kuruhusu watalii wa kigeni kurudi nchini na Wakristo walikuwa wamewasili kutoka kote ulimwenguni.
"Ilichukua imani nyingi na azimio kufanikisha hilo," alisema Alina Lord, 48, ambaye alisafiri kwa ndege kutoka Romania. Aliamka saa 5 asubuhi ili kuhudhuria na alifanikiwa kupata nafasi kwenye ufunguzi wa kaburi.
Kwa Sophia Gorgis mwenye umri wa miaka 65, ambaye alikimbia vita vya Syria hadi Sweden anasema, ilikuwa ndoto ya maisha yote kusherehekea sherehe ya Moto Mtakatifu huko Yerusalemu.
"Sina neno,"alisema, huku akihema. "Mara tu tulipopata pasipoti zetu (za Sweden), tulijiandikisha kwa safari hii,"amesema Sophia.
Wakati huo huo, mapigano yalizuka kati ya mahujaji wa Kikristo na maafisa wa Polisi wa Israeli ambao walisambazwa katika Jiji la Kale la Jerusalem ili kudhibiti wingi wa washiriki.