NA GODFREY NNKO
MFANYABIASHARA ndogo ndogo maarufu kama Machinga, Bw.Tumaini Saimon Mkono aliyechukuliwa vitu vyake jana na mgambo amefika nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi Robert Gabriel akiwa na Mbunge Stanslaus Mabula wa Jimbo la Nyamagana leo.
Hatua hiyo, imepongezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Innocent Bashungwa.
"Nampongeza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel Luhumbi kwa kuchukua hatua ndani ya saa 24 niliyomuagiza. Kitendo hicho cha kikatili na cha kukosa utu kilinikwaza sana ningekuwa Mwanza mtu angekula hedi.
"Wakuu wa mikoa endeleeni na zoezi la kutenga maeneo rafiki kwa biashara ya Machinga, kuyawekea miundombinu rafiki, kuwapanga kwenye maeneo kwa utaratibu unaoheshimu utu, kuwapa elimu ya biashara na kuwaunganisha na bima na taasisi za fedha, na kuepuka kuendesha opereshi zinazoepuka uharibifu wa mali,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.
Aprili 16, 2022 Waziri Bashungwa alitoa maagizo akiwawataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya za mkoa huo kujitathmini iwapo wanastahili kuendelea kuwepo kwenye nafasi zao akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel kufuatilia wahusika wa tukio hilo na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Muda mfupi baada ya Waziri huyo kutoa maagizo, RC Gabriel alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana (DC), Amina Makilagi kuwachukulia hatua mgambo saba wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo pamoja na kumsimamisha kazi mratibu wa Jiji la Mwanza wa upangaji wa wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake
“Namuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kuwaondolea hadhi ya kuwa askari wa jeshi la akiba kikosi chote kilichohusika katika tukio hilo mara moja kuanzia muda huu ikiwa na maana kwamba hawataweza kufanya kazi tena kama jeshi la akiba. Pili namsimamisha majukumu yake mratibu wa Jiji la Mwanza wa zoezi la upangaji wa machinga kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake,”amesema.
Wakati huo huo,Mkuu huyo wa Mkoa amelaani vikali kitendo hicho cha mgambo kuwasumbua wafanyabiashara wadogo.