Wataalamu kutoka OR-TAMISEMI wabaini kasoro Buhigwe

NA OR-TAMISEMI

TIMU ya ufuatiliaji kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) na nyumba ya watumishi katika Hospitali ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma.
Ujenzi huo unatekelezwa kupitia fedha za mkopo wenye masharti nafuu wa IMF wenye lengo la kupunguza athari zitokanazo na ugonjwa wa UVIKO -19.
Timu hiyo imeielekeza timu ya usimamizi wa shughuli za Afya ngazi ya Wilaya (CHMT) kuhakikisha inafuatilia kwa karibu na kuimarisha usimamizi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Akizungumza Aprili 25, 2022 Mkurugenzi wa Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii OR-TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa ,wamesikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji iliyopo wakati halmashauri hiyo ilipokea fedha toka Novemba 2021.

“Tulitegemea ujenzi huu ukamilike kwa wakati, lakini bado hali ya utekelezaji hairidhishi kabisa, hakikisheni mnashirikiana ili kumaliza ujenzi huu kwa wakati, tukimuachia Mkurugenzi au Mganga Mkuu wa Wilaya hatutakamilisha kwa wakati, tushirikiane kwa pamoja,”amesema Dkt.Ntuli.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe, Essau Ngoroka amesema halmashauri hiyo ilipokea fedha shilingi milioni 390 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura pamoja na nyumba ya watumishi, ameihakikishia timu hiyo kuwa ifikapo Mei 21, 2022 ujenzi huo utakuwa umekamilika.

Timu hiyo ilikagua ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Kakonko na imempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa kusimamia vizuri utekelezaji huo na kumtaka kuendeleza juhudi hizo kwa miradi mingine .
Naye Dkt. Sonda Shaaban,Msimamizi wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za Afya (OR-TAMISEMI) ameshauri ukarabati wa Kituo cha Afya Mtendeli utekelezwe kupitia Mapato ya ndani ya Halmashauri au kusubiri fedha za awamu nyingine, fedha zilizotolewa shilingi milioni 500 zitumike kujenga kituo kipya cha kutolea huduma ya afya katika eneo jingine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news