*Lita ni shilingi 6000 kutoka 3000 za Kitanzania nchini Finland
NA GODFREY NNKO
WATANZANIA wanaoishi katika mataifa mbalimbali duniani wamesema kuwa, vita kati ya Urusi na Ukraine imechochea kwa kiwango kikubwa mfumuko wa bei za vyakula na mafuta, hivyo wananchi kulazimika kuingia mifukoni zaidi ili kupata huduma hizo.
Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakielezea madhila ambayo mataifa mbalimbali duniani yanapitia kwa sasa tangu vita hiyo ianze mwezi Februari, mwaka huu ambapo, mambo yamezidi kuwa magumu zaidi baada ya Urusi kuwekewa vizuizi mbalimbali na mataifa ya Ulaya.
Finland
Bw.Edwin Ndaki ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Finland amesema kuwa, vita ya Ukraine na Urusi imesababisha madhara makubwa katika bidhaa ya mafuta nchini humo.
Amesema, mafuta nchini humo yamepanda ghafla kutoka shilingi 3000 ya Kitanzania hadi shilingi 6000 za Kitanzania ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kipindi kifupi.
"Moja ya jambo ambalo linaumiza wakazi na wananchi wa Finland ni ongezeko kubwa la mafuta, kabla ya vita ya Urusi na Ukraine bei ya mafuta hapa ilikuwa shilingi 3000 ya Kitanzania kwa maana ya Euro moja na senti ishirini, lakini leo hii, mpaka jana, tunaongelea shilingi 6000 kwa lita, hii ni sawa na Euro mbili na senti thelathini na kuendelea.
"Kwa hiyo unaona kuna tofauti ya shilingi elfu tatu nzima ndani ya muda huu mfupi, mbali na hilo tunaona kwamba wakulima wa nchi hii wanakwenda kupitia kipindi kigumu sana, ikizingatiwa kuwa Urusi ni moja wa wazalishaji wakubwa sana wa mbolea ambazo zinatumiwa na mataifa mengi barani Ulaya.
"Kwa hiyo moja ya madhara mengine ambayo wanayapitia kwa sasa ni ongezeko la gharama za uzalishaji na kilimo kwa ujumla, kwa hiyo unamuangalia Urusi ambaye ni mzalishaji mkubwa wa mbolea ya potash, phosphate na nitrogen kwa kufanya hivyo basi wakulima sasa hivi wanapitia katika kipindi kigumu mno.
"Lakini, vile vile ukienda kwenye maduka kununua vyakula na vitu vingine, vyakula vinaanza kupanda bei kwa sababu ya hali na madhara yatokanayo na hii vita, na hii ni kwamba kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Masuala ya Kiuchumi cha hapa Finland kinaitwa, Pervo wanasema kwamba kwa takribani raia wa Finland wanatumia asilimia 11 ya pato lao katika mahitaji ya chakula, lakini kutokana na vita ianayoendelea wameambiwa wajiandae, tafiti zinaonesha kwamba itaenda mpaka asilimia 20.
Watatumia mpaka asilimia 20 ya pato lao,kutokana na gharama za maisha kupanda kutokana na vita vinavyoendelea, ikumbukwe Taifa la Urusi na Ukraine, ni miongoni mwa mataifa makubwa yanayoongoza kwa uzalishaji wa bidhaa ya ngano, kwa hiyo ngano inapopanda kuna bidhaa ikiwemo mikate na vitu vingine, huduma na vyakula mbalimbali vinapanda.
"Kwa kifupi, ukiangalia madhara na madhila ya vita hivi ni pigo kubwa kwa Taifa hili na Dunia nzima, kwa hiyo inapokuja nyumbani Tanzania,ongezeko la bei ya mafuta, kama alivyosema Mheshimiwa Rais Mama Samia, si kwamba ni kwa Tanzania tu, hili ni suala la kidunia, kwa hiyo ni wakati wa Watanzania ambao tunaelewa hili jambo kwa upana, kuwaeleza wenzetu kwa lugha nyepesi na rahisi.
"Kwamba gharama za maisha zinazotokea kwa sasa, kupanda kwa vitu bei na mfumuko wa bei na kupanda bei za mafuta si suala la Serikali iliyopo madarakani, hili ni suala la Dunia na ni madhara yanayotokea kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine,kwa hiyo watanzania tuendelea kuwa wamoja, tuendelee kuchapa kazi kwa bidii, tuendelee kushirikiana na Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kulijenga Taifa letu,"amesema.
Washington DC
Naye Mwanadiaspora, Loveness Mwamuya ambaye ni Mtanzania anayeishi jijini Washington DC nchini Marekani amesema kuwa, vita kati ya Urusi na Ukraine imesababisha hali ya maisha nchini humo kuwa ngumu.
"Sasa hivi Marekani vitu vimepanda sana, kutokana na vita inayoendelea ya Ukraine na Urusi,Marekani maisha yamekuwa magumu sana, vitu vimepanda bei sana, mafuta mpaka ninaondoka kwa galoni siyo kwa lita ilikuwa dola tano na senti hamsini, ambapo tulikuwa dola mbili, dola moja. Kwa hiyo, ongezeko limekuwa kubwa sana.
"Kwa hiyo gharama za maisha zimepanda kwa ujumla, vitu masokoni, kwenye maduka vimepanda mara tatu. usafiri umepanda. Kila kitu kimekuwa juu zaidi kutokana na vita vinavyoendelea.
"Maisha ya Tanzania nilivyoona kwa wiki hizi mbili ambazo nilikuwepo kidogo ninaona angalau afadhali, maana vitu havijapanda sana kama sisi tuliopo nje, tunavyoshuhudia. Kikubwa ambacho, tunapaswa kukifanya hili kuweza kupambana na hii changamoto ni kumuomba Mungu ili vita hii iweze kwisha, na maisha yaweze kurejea kama kawaida, kwa kweli maisha kwa Marekani yamekuwa magumu sana maana vitu vimepanda sana.
"Na hii changamoto si Marekani tu, niliweza kufika Dubai wiki mbili kabla, mambo napo yalikuwa hivyo hivyo, hivyo tunapaswa kushirikiana hususani kipindi hiki cha mfungo kwa ndugu zetu Waislamu na Wakristo kumuomba Mungu aweze kutuondolea hii changamoto,"amesema.
Ujerumani
John Jackson ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Ujerumani amesema kuwa, vita ya Ukraine na Urusi imesababisha gharama za gesi na mafuta ya kupikia kupanda kwa kasi.
"Sasa hivi, kumekuwepo changamoto ya mfumuko wa bei kutokana na vita ya Urusi na Ukraine vita hii imepelekea hapa Ujerumani vitu kadhaa kupanda bei, sasa hivi kuna changamoto ya gesi, kama unavyofahamu nchini nyingi hapa Ulaya zinategemea gesi kutoka Urusi,
"Na gesi hiyo ndiyo inayosababisha ongezeko la joto kipindi cha baridi nyumbani, ambapo kunakuwepo na heater, kwa hiyo gesi imepanda bei sana kwa maana ya matumizi ya nyumbani na matumizi ya magari,lakini wakati huo pia mafuta ya kupikia yamekuwa changamoto kubwa sana na wakati mwingine hayapatikani kabisa, kwa sababu mafuta hayo yanapatikana kutoka Ukraine na Urusi.
"Pia bei ya vyakula vya mifugo imepanda kwa asilimia 50, hapa ninamaanisha vyakula vya wanyama vimepanda kutoka asilimia moja hadi asilimia 50 kwa ghafla.
"Mfumuko wa bei si wa Tanzania tu, tena huenda Tanzania haujawa mfumuko wa bei sana kama sisi huku tunavyokabiliana nao, bidhaa zimepanda bei kwa asilimia 50, huu ni mfumuko wa Dunia kwa ujumla, mfano kwa sasa hivi mikate pia imepanda bei, na imefikia hatua watu wananunua vitu wanaweka ndani, jambo ambalo si salama sana,kikubwa tuendelee kuchapa kazi na kushirikiana na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili tuweze kuyafikia malengo ya kuliletea Taifa letu maendeleo,"amesema.
Sweden
Naye Norman Jasson ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Sweden amesema, vita kati ya Urusi na Ukraine imesababisha bei ya mafuta kupaa kwa kasi nchini humo.
"Hapa Sweden kwa sasa mafuta yamepanda bei sana,bei sasa hivi inakwenda kati ya shilingi za Kitanzania 5,100 hadi 5,800 kwa lita moja, sasa unaweza kulinganisha, sisi tupo karibu zaidi na Urusi, lakini bei imepanda zaidi ya mara mbili tofauti na Tanzania.
"Sababu kuu ya bei za mafuta kupanda ni hii vita kati ya Urusi na Ukraine,"amesema huku akisisitiza kuwa kuna baadhi ya mafuta yanayotumika zaidi nchini humo kuendeshea magari ya kisasa yanayotumia Diesel nchini humo, lakini yameadimika ambapo licha ya kupanda bei mara dufu hayapatikani.
Ametumia nafasi hiyo, kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbai ikiwemo bidhaa za mafuta.
"Na inawezekana kuna gharama ambazo Serikali inazibeba, lakini hatuzijui. Bei ya mafuta imepanda Dunia nzima,bahati mbaya kwa hapa Sweden kama nilivyosema, bei ya mafuta imepanda, lakini nauli ipo pale pale, mishahara ipo pale pale,na gharama nyingine zipo pale pale, tuwe wavumilivu, haya ni mambo ya kupita na ninaamini yatapita na tutarejea katika hali yetu ya kawaida kama ilivyokuwa awali,"amesema.
London
Kwa upande wake, Bw.John Warioba ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Uingereza anasema kuwa, vita kati ya Urusi na Ukraine imeongeza maumivu makubwa katika bei ya mafuta, kwani bei zimeongezeka kwa asilimia 30 hadi 50.
Marekani
Naye Afisa Mkuu wa Fedha wa Jimbo la Connecticut nchini Marekani, Bw.Lunda Asmani ametaja sababu kuu tatu ambazo zimechangia bei za bidhaa hususani mafuta kupanda kwa kasi duniani.
"Kusema kweli, bei ya mafuta imepanda, na imeanza kupanda kwa kasi sana Duniani kote, lakini kuna sababu kuu tatu za kiuchumi ambazo zimechangia bei ya mafuta kupanda.
"Kwanza, itakumbukwa kuwa, kipindi kile cha UVIKO-19 imepamba moto, watu wengi mizunguko ilikuwa imepunguzwa sana, wafanyakazi walikuwa wanafanya kazi kutoka majumbani, usafiri wa anga, usafiri wa barabara ulikuwa umepungua sana, hivyo ule uhitaji wa mafuta ulikuwa umepungua, yaani ile demand (uhitaji) ya mafuta ilikuwa imeshuka sana,"amesema Bw.Asmani.
Amefafanua kuwa, kwa wastani wanasema, Marekani mtumiaji wa kawaida wa mafuta alikuwa amepunguza matumizi ya mafuta kwa karibu asilimia 50, kwa sababu ya kutozunguka na watu walikuwa wanafanya kazi nyumbani, na mizunguko ya safari ilikuwa imepungua kutokana na janga la UVIKO-19.
"Sasa unakuta katika hali hiyo, wakati uhitaji wa mafuta ulikuwa umpungua pia kiuchumi na bei ya mafuta huwa inashuka yaani 'supply and demand' kipindi hicho kutokana na uhitaji wa mafuta kuwa mdogo,"amesema.
Bw.Asmani amesema jambo la pili ambalo linalingana na hilo,ni kwamba kipindi hicho wakati uhitaji wa mafuta umepungua na uzalishaji pia, wazalishaji wa mafuta wenye walipunguza uzalishaji,kwa sababu uhitaji ulikuwa mdogo.
"Kwa hiyo kama wangeendelea na uzalishaji kabla wakati ule wa UVIKO-19, wangejikuta kwamba wana malighafi ambayo haina mnunuzi, kwa hiyo na wao walipunguza sana uzalishaji wa mafuta, kwa hiyo hali hiyo ikatengeneza hali ya uhaba.
"Kama mnavyofahamu katika uchumi, panapokuwa na uhaba wa kitu chochote kile, bei ya hiyo bidhaa huwa inapanda. Kwa hiyo kutokana na ule uhaba,wa uzalishaji wa mafuta kutokana na uhitaji wa mafuta kuwa mkubwa,na wenyewe sasa umeanza kuchangia kuongezeka kwa bei ya mafuta.
"Na sasa hivi, nchi zimeanza kufunguka,watu wameanza kurudi makazini, watu wameanza kusafiri na mipaka imeanza kufunguliwa, sasa unakuta ule uhitaji wa mafuta umepanda, lakini ule uzalishaji bado ulikuwa katika kile kiwango cha ule uhitaji mdogo,na bado haujafikia ule uhitaji wa sasa, sasa inapotokea katika hali hiyo,unakuta kwamba, bei ya bidhaa yoyote ile kama uhitaji ni mkubwa na uzalishaji ni mdogo itapanda bei na ndivyo ilivyo kwa bei ya mafuta,"amefafanua Bw.Asmani.
Wakati huo huo, Bw.Asmani ametaja jambo la tatu ambalo limechangia bei ya mafuta kupanda kwa kasi duniani kuwa inachochewa na vita kati ya Urusi na Ukraine.
"Jambo la tatu ni hii vita ya Urusi kuivamia nchi ya Ukraine, kwamba kutokana na vikwazo ambavyo mataifa ya Magharibi yameanza kuiwekea Urusi,kama mnavyofahamu nchi ya Urusi ni mzalishaji mkubwa wa mafuta, vile vikwazo sasa vinachangia katika kupunguza uzalishaji wa mafuta.
"Kwa sababu yale mafuta ambayo Urusi ilikuwa ikiyauza nchi za nje, nchi za nje sasa zimeacha kununua mafuta kutoka Urusi,hivyo sasa imepunguza soko, hivyo kama nilivyosema awali unapokuta soko limepungua na mahitaji yapo juu, basi bei zinakuwa zimepanda.
"Kwa hiyo kuna vitu vikuu vitatu ambavyo vimetokea kwa wakati mmoja,ambavyo vimechangia hili la bei ya mafuta kuwa juu na hii si kwa nchi moja tu, ni kwa nchi zote duniani, popote pale ulipo ukifungua gazeti au ukiangalia taarifa ya habari.
"Taarifa nyingi za habari zinaanza na hilo la bei ya mafuta, kama kawaida bei ya bidhaa au mafuta huwa inapanda na kushuka, kwa hiyo tuna imani kwamba baada ya muda hili litasawazika na bei zitarudi kama kawaida, kama tulivyozoea wananchi,"amefafanua Bw.Asmani.