NA DIRAMAKINI
NAIBU Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Deogratius Ndejembi amesema watumishi wa umma 1,477 wamesimamishwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia nidhamu katika utumishi wa umma.
Ndejembi ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 11, 2022 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi.
Kunambi ameuliza namna mashauri yanayoendelea kusikilizwa na Tume ya Utumishi wa Umma yanachukua muda mrefu sana.
“Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa mashauri haya yanakamilika kwa wakati?,”amehoji Kunambi.
Akijibu swali hilo, Ndejembi amesema watumishi 1,477 wanatakiwa kuchukuliwa hatua za nidhamu na tayari watumishi 598 wamekata rufaa katika tume ya utumishi wa umma.
Amesema rufaa 411 zina maelezo yaliyokamilika na rufaa 187 hazina vielelezo ambazo zimerudishwa kwa waajiri kwa mamalaka za nidhamu ili ziweze kufanyiwa kazi.
“Rai yangu hawa wanaopeleka mashuri hayana vielelezo yaweze kuwa yanawasilishwa na vielelezo kamili ili haki ambayo ameizungumzia mheshimiwa Kunambi iweze kupatikana kwa haraka zaidi,”amesema.
Katika swali la msingi, Kunambi alihoji ni watumishi wangapi wamesimamishwa kazi tangu mwaka 2015 hadi 2022 ambao mashauri yao hayajaisha.
Akijibu swali hilo la msingi, Ndejembi amesema waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni, taratibu na Miongozo inayosimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma.
“Mashauri haya yapo katika hatua mbalimbali za mamlaka za nidhamu ambazo ni waajiri mbalimbali na mamlaka za rufaa ambazo ni Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Walimu na Ofisi ya Rais,”amesema.
“Nichukue fursa hii kuwakumbusha Waajiri au Mamlaka za Nidhamu kuongeza kasi ya kuhitimisha mashauri ya nidhamu yaliyopo kwa kuzingatia taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu,”amesema. (Mwananchi)