NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameagiza kamanda wa jeshi la polisi wilayani Handeni mkoani Tanga,kuwakamata na kuwaweka ndani mtaalam wa mabwawa kutoka wizara hiyo kutokana na kumpa taarifa ambayo sio sahihi kuhusu ujenzi wa bwawa Kwenkambala.
Waziri Jumaa Aweso ametoa maagizo hayo leo kwenye ziara yake ya kukagua ujenzi wa bwawa la maji la Kwenkambala wilayani Handeni ambalo ujenzi umesimama na kusema kuwa wasaidizi wake wameshindwa kumpa taarifa sahihi wakati ni wajibu wao.
Walioagizwa kukamatwa na Waziri Aweso ni Hamisi Matunguru,mkandarasi Robert Lupinda na Mhandisi Amos Mtweve mthibiti ubora kutoka makao makuu kwa kushindwa kumpa taarifa sahihi kuhusu ujenzi wa bwawa la Kwenkambala.
Amesema kuwa, yeye kama waziri mwenye dhamana hatafumbia macho wataalam ambao bado wanahujumu miradi ya maji hata kama awe na nafasi kubwa.
"Niwaombe radhi viongozi na wananchi wa Handeni kwa hadha hii,niwahakikishie tunalifanyia kazi hili jambo na nitatoa majibu ni hatua gani nitachukua,"amesema Waziri Aweso.
Hata hivyo mwenyekiti halmashauri ya mji Handeni, Mussa Mkombati amemuomba Waziri Aweso kuwa, wananchi waliozungukwa na mradi huo wa maji walipwe fedha zao za fidia kwani mkandarasi ameshalipwa.
Mkombati ameongeza kuwa, walihisi tangu awali wao kama madiwani uwezo wa mkandarasi ni mdogo,ila walidharauliwa na kuambiwa wanaleta siasa kwenye jambo hilo.