NA HAPPINESS SHAYO-WMU
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameahidi kushirikiana na watendaji na watumishi wa wizara yake katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya wizara hiyo.
Ameyasema hayo leo Aprili 2,2022 alipowasili katika ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii zilizopo Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kuapishwa.
“Niwahakikishie
kwamba niko tayari kuchapa kazi pamoja nanyi, imani kubwa ambayo Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametupa
hatutamuangusha,” Mhe. Chana amesisitiza.
Aidha, ameweka bayana kuwa yuko tayari kufanya kazi kwa saa 24 bila kikwazo chochote.
"Mimi
kama Waziri wenu milango iko wazi saa 24, hakuna wakati sitapatikana
iwe ni usiku, iwe asubuhi hata iwe sikukuu na ndio maana ya kuwa
mtumishi wa umma,” amesisitiza.
Naye,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) ameeleza kuwa
Wizara imepata mtu sahihi wa kuitoa ilipo na kuisogeza mbele na kwamba
Mhe. Pindi Chana yuko na timu ya watendaji mahiri na wachapakazi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja
(Mb) amemkaribisha Waziri Pindi Chana na kumpongeza kwa kuteuliwa
kushika wadhifa huo.
“Tunakukaribisha
sana katika Wizara ya Maliasili na Utalii na kukupongeza sana kwa
kuteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Maliasili na Utalii,”amesema Mhe.
Masanja.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameanza kazi leo kwa mara ya kwanza mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.