*Mheshimiwa Mchengerwa asema mambo mazuri yanakuja
NA OR- TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaelekeza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo kinapewa kipaumbele sawa na vitengo vingine na kukiwezesha ili kiweze kuwahudumia Watanzania katika halmashari zote.
Waziri Bashungwa amesema hayo leo Aprili 6, 2022 jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kuridhia kuanzishwa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo na kumuagiza Katibu Mkuu OR-TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa kuanzishwa kitengo hicho kipya cha utamaduni, sanaa na michezo.
Akifunga kikao kazi hicho, Waziri Bashungwa amewaelekeza watendaji wote wanaohusika na utekelezaji wa mabadiliko ya muundo wa kada za Maafisa Utamaduni na Maafisa Michezo ulioidhinishwa kutekelezwa haraka iwezekanavyo ifikapo Julai 1, 2022.
“Niwahakikishie, maelekezo ya Waziri Mkuu aliyayatoa hapa wakati wa kufungua kikao kazi hiki tutayatelekeza pamoja na maazimio yanayohusu utekelezaji kwa upande wa TAMISEMI ninaahidi yatafanyiwa kazi na kutolewa taarifa kila baada ya miezi minne kama ilivyo kwa taasisi nyingine ili tunapokutana katika kikao kazi kingine, tuwe na taarifa ya jumla ya utekelezaji na tusonge mbele zaidi,” amesema Waziri Bashungwa.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, wizara yake inashirikiana kwa karibu na OR-TAMISEMI katika kutekeleza majukumu na maelekezo ya viongozi ili kufikia azma ya Serikali.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema kuwa, wizara hiyo ni nguvu laini (soft power) ya nchi, hivyo maafisa hao wametakiwa kuweka uzalendo na utaifa mbele ili sekta hizo ziweze kuwa na tija kwa taifa na wananchi wake kwa maendeleo endelevu.
