Waziri Bashungwa:Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi, asasi za kiraia kuwahudumia Watanzania

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Taasisi na Asasi za Kiraia katika jitihada za kuwahudumia Watanzania na kuisaidia jamii kwa kutoa huduma mbalimbali.
Ameyaeleza hayo leo Aprili 9,2022 mjini Bukoba, Kagera katika maadhimisho kumbukumbu na kuenzi maisha na Utumishi wa Hayati Baba Askofu Dkt.Samson B Mshemba (Mushemba Day) aliyekuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi na kuweka bayana shughuli za taasisi ya Mushemba Foundation kwa jamii ya Watanzania na kuzindua bweni la wanafunzi wa Shule ya Mushemba Trinity.
“Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Mushemba Foundation na Mushemba Trinity School kuhakikisha tunaendeleza kazi nzuri inayofanywa ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kusaidia jamii hususani watoto waishio katika mazingira magumu na kutoa elimu kwa jamii juu ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI,”amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa, marehemu Baba Askofu Dkt.Samson Mushemba ameacha alama kubwa ndani ya jamii yetu ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Mushemba Foundation iliyoanzishwa kwa lengo la kusaidia watoto waishio katika mazingira magumu na kuanzisha Shule ya Mushemba Trinity School.

Aidha, ameeleza kuwa, Shule ya Mushemba Trinity inaunga mkono jitihada za Serikali kwa kutoa elimu bila malipo ambapo mpaka sasa Serikali imepeleka jumla ya shilingi trilioni 1.43 kwa ajili ya kugharamia Mpango wa Elimu msingi bila Malipo.

Wakati huo huo, Bashungwa amemuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa Kagera kupitia barabara ya mita 700 inayoelekea shuleni ili iwekwe katika bajeti na itengenezwe kwa viwango ili kurahisisha watoto wanaosoma katika shule hii kupata elimu bora.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mshemba Fondation Tanzania, Diacon J. Mushemba amesema, taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2007, lengo kubwa likiwa ni kuendelea kuyaishi kwa vitendo maneno, mahubiri, ushauri, mtazamo na miongozo ya Baba Askofu Dkt. Samson Mushemba.
Vile vile, ameeleza mwaka 2012 ilianzishwa Shule ya Mushemba Trinity kwa malengo ya kutimiza azma ya taasisi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu bora kwa jamii hasa watoto wa familia masikini, wasiojiweza na yatima wanaoishi katika mazingira magumu ambapo mpaka sasa shule ina wanafunzi 417 wa darasa la kwanza hadi la saba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news