Waziri Mkuu aipa tano Simba SC, asisitiza jambo

*Pia agusia vilabu na timu nyingine Tanzania Bara na Visiwani

NA GODFREY NNKO

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameipongeza Klabu ya Simba (Simba SC) kwa kuendelea kuiwakilisha vema Tanzania katika michuano ya Kimataifa kupitia Kombe la Shirikisho barani Afrika.

"Kipekee niipongeze timu ya Simba SC kwa kupeperusha bendera ya Taifa letu katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika, mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa;
Ametoa pongezi hizo leo Aprili 6,2022 jijini Dodoma wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2022/2023.

"Nitumie fursa hii kuendelea kusisitiza umuhimu wa michezo kwa kuvipongeza vilabu vyetu vya mpira wa miguu vinavyoshiriki kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Kuu Zanzibar, hakika kwa mpira mzuri wanaocheza wanakonga mioyo ya washabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

"Niwapongeze pia wachezaji mahiri wa vilabu mbalimbali vya mpira wa miguu vikiwemo Yanga, Simba, Namungo, Azam,Biashara United, Dodoma Jiji, Tanzania Prisons na bila kuwasahau Mtibwa Sugar

"Vilevile, nivipongeze vilabu vya Zanzibar vikiwemo KMKM, Mlandege, Malindi, Mafunzo na vilabu vinginevyo,"amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Simba SC

Simba SC ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania ambao wanatarajiwa kumenyana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Wekundu hao wa Msimbazi wataanzia nyumbani Aprili 17, kabla ya kusafiri kwenda Houghton jijini Johannesburg kwa mchezo wa marudiano Aprili 24, 2022.

Aidha,mechi nyingine za Robo Fainali ni baina ya timu za Libya tupu, Al-Ittihad dhidi ya Al-Ahli Tripoli, Pyramids ya Misri dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al-Masry ya Misri dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Hata hivyo, mechi zote za kwanza zitachezwa Aprili 17, 2022 na marudiano Aprili 24, mwaka huu.

Simba SC walifanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya US Gendamarie ya Niger kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Simba inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pablo Franco Martin yalifungwa na kiungo, Sadio Kanouté dakika ya 63, mshambuliaji Mkongo Chris Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 68 na 78 na kipa Saidu Hamisu aliyejifunga dakika ya 84 katika harakati za kuokoa.

Bernard Morrison alifanikiwa kuseti mabao mawili ya kwanza baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza ambacho wawili hao walienda mapumziko bila kitu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news