NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wafanye ziara kwenye masoko na maduka ili kupata hali halisi ya bei za bidhaa na wachukue hatua kudhibiti upandaji holela wa bei hizo.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Aprili 22, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu maendeleo ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mitandao (video conference) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.
“Tumepata malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba bidhaa nyingi zimepanda bei, ninyi ni Wenyeviti wa Kamati za Bei na Kamati za Kodi kwenye mikoa na wilaya zenu. Upandaji wa bei sasa umekuwa holela. Ni jukumu lenu kufanya ufuatiliaji wa bei za mazo katika masoko yenu.”
Waziri Mkuu amesema ziko bidhaa ambazo zinazalishwa nchini kama vile nondo au saruji ambazo hazipaswi kupanda bei hasa baada ya kutolewa tamko na Waziri wa Fedha na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwamba wameshaongea na wenye viwanda na wakakubaliana kuwa bidhaa zote za ndani zinapata nafuu ya kodi.
“Sasa iweje hali iendelee kuwa vilevile?”, amehoji na kuongeza: “Vyakula vinavyozalishwa nchini kama mchele, Shinyanga mchele mwingi, Tabora mchele mwingi, Mbeya nako mchele mwingi kuna sababu gani ya kupadisha mchele wakati unazalishwa nchini?.
“Kama ni mahindi au mihogo inalimwa huko kwenu, umbali wa mazao yanakolimwa mnaujua, iweje bei zipande? Nenda mpite kwenye masoko na kwenye maduka mpate bei za kila siku za maeneo yenu. Kukaa kimya na masoko yako kwenu, na bidhaa ziko kwenu na walaji wako kwenu halafu hamchukui hatua, tutakuwa hatufanyi vizuri.”
“Ninawaagiza, fanyeni ziara kwenye masoko yenu, fanyeni tafiti na mtathmini ni kwa nini bei zinapanda. Mchicha unapandaje bei, ni kwa sababu ya nini? Zungumzeni na tuone mkianza kudhibiti hiyo hali. Na Kama kuna maeneo bei inapanda kiholela, hakikisheni bei inashuka iende kwenye bei halisi ili tuwasaidie wananchi.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao waongeze hamasa kwa wananchi ili waweze kushiriki kwa wingi kwenye Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.
“Hamasa ni muhimu kwa wananchi wa makundi yote. Tutumie wadau mbalimbali kwenye maeneo yetu kama vile Wabunge, madiwani, viongozi wa masoko, viongozi wa vilabu vya michezo na viongozi wa kijamii ili watusaide kuhamasisha wananchi.”
Amesisitiza kuwa ubunifu wa jumla wa namna ya kukamilisha suala hilo unahitajika zaidi.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na viongozi hao, Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Bw, George Simbachawene alisema asilimia 85 ya wananchi wamejengewa uelewa kuhusu anwani za makazi ambapo anwani 9,490,959 zimeainishwa na kuingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi (National Physical Addressing - NaPA).
Amesema jumla ya majengo 810,919 yameshahesabiwa nchini, nguzo 70,369 zimewekwa na vibao vya namba 31,239 vimebandikwa.
Naye, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema kazi ya kutenga maeneo ya kijiografia ya kuhesabia watu kwa Tanzania Bara na Zanzibar imekamilika kwa asilimia 100 ambapo vitongoji 64,318 na maeneo 4,313 kwenye shehia zote 388 yameshatengwa.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie Kamati za Sensa za Kata na Shehia ili zifanye kazi ya kuelimisha wananchi na kuondoa shaka iliyopo.
Wakuu wa mikoa ya Arusha, Ruvuma, Mwanza, Mtwara, Tanga, Kilimanjaro, Dar es Salaam na Njombe walitoa maoni yao na kuelezea hatua zilizofikiwa kwenye maeneo yao.