NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha bei ya bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa himilivu wakati ikiendelea kufanya tathmini kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuona namna ya kuleta unafuu.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa ili kupanga viwango vipya vya kodi vitakavyoleta unafuu kwa mlaji kama vile kupunguza kodi ya baadhi ya bidhaa.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 13, 2022) wakati akihitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2022/2023. Bunge limepitisha kwa kauli moja bajeti hiyo.
Ametumia fursa hiyo kuzielekeza kamati za bei za Mikoa na Wilaya zihakikishe zinafuatilia na kujiridhisha na uhalisia wa kupanda kwa bei za bidhaa kwenye maeneo yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameendelea kukemea vitendo vya baadhi ya wazalishaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kuamua kupanga bei, kufanya mgomo, kukubaliana katika manunuzi na kuzuia uzalishaji, mbinu ambazo wakati mwingine zimekuwa chanzo cha kupanda kwa bei ya bidhaa. “Wale wote watakaobainika kufanya michezo hiyo, hatutosita kuwachukulia hatua za kisheria,” amesisitiza.
Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inaimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani hasa bidhaa za chakula zinazoingizwa kwa wingi kutoka nje ikiwemo ngano, mafuta ya kula na sukari kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kutoa vivutio stahiki.
Waziri Mkuu amesema mbali na hatua hiyo, Serikali pia itaendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji wa ndani kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ili kukabiliana na aina hii ya mtikisiko wa kiuchumi.
Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara iendelee kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye soko na kuchukua hatua stahiki sambamba na kusimamia vema mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za bidhaa sokoni.
“Vilevile, ninazielekeza Mamlaka na Taasisi za Serikali zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu huo kikamilifu na kwa umakini mkubwa sambamba na kudhibiti vitendo vya upandishaji holela wa bei za bidhaa nchini.”
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania waendelee kuwa wamoja na wafanye kazi kwa bidii ili kuufanya uchumi wa Taifa kuwa shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu.
“Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha hakuna uhaba wa bidhaa nchini wakati ikiliangalia vizuri suala la bei na kuona namna ya kutoa unafuu kwa wananchi.”